Mamlaka ya maji safi, usafi wa mazingira kuanzishwa wilayani Rombo

Naibu waziri wa Maji, Juma Aweso

Muktasari:

Imeelezwa kuwa changamoto inayoikabili Wilaya ya Rombo ni upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, baadhi ya vijiji wananchi wanashindwa kufanya shughuli za maendeleo kutokana na muda mwingi kuutumia kutafuta maji.

Rombo. Wizara ya Maji nchini Tanzania ipo mbioni kuanzisha mamlaka ya maji Wilaya ya Rombo Mkoa wa Kilimanjaro.

Hayo yameelezwa jana Ijumaa Januari 24, 2020 na naibu waziri wa Maji, Juma Aweso wakati akizungumza na viongozi  mbalimbali wa wilaya hiyo muda mfupi kabla ya kuanza ziara ya kukagua miradi ya maji.

Naibu waziri huyo amesema changamoto kubwa inayoikabili wilaya hiyo ni upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, kwamba baadhi ya vijiji wananchi wanashindwa kufanya shughuli za maendeleo kutokana na muda mwingi kuutumia kutafuta maji.

"Wizara ina kazi ya kuangalia namna ya kuwawezesha watu wa Rombo kuongeza uzalishaji wa maji, sasa tunaangalia kufanya mradi wa haraka na tutatoa Sh1.5 bilioni ili kutekeleza mradi huo wakati tukiangalia namna ya kutekeleza mradi mkubwa wa Chala."

"Pamoja na kuongeza uzalishaji kwa mradi huo wa maji lazima  kwa eneo hili la Rombo tuwe na chombo kitakachokuwa na ufanisi wa kusimamia miradi hiyo na kama Wizara tumekubaliana tuanzishe mamlaka ya maji hapa Rombo,” amesema Aweso.