Watakaofikisha miaka 18 kabla ya Oktoba watakiwa kujiandikisha daftari la wapiga kura

Muktasari:

Wakati  uboreshaji wa daftari la wapiga kura katika mkoa wa Dar es Salaam ukianza  leo, vijana wanaotarajia kufikisha miaka 18 kabla ya Oktoba, 2020 wamehamasishwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha.

Dar es Salaam. Wakati  uboreshaji wa daftari la wapiga kura katika mkoa wa Dar es Salaam ukianza  leo, vijana wanaotarajia kufikisha miaka 18 kabla ya Oktoba, 2020 wamehamasishwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha.

Wito huo umetolewa leo Ijumaa Februari 14, 2020 na mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakati akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari Tambaza.

Uboreshaji huo umeanza leo katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam na unatarajiwa kuendelea kwa siku sita.

Makonda amesema uchaguzi wa mwaka 2020 umewalenga zaidi vijana ambao ni Taifa la kesho.

“Kama unatimiza miaka 18 mwezi Julai, Agosti hata Oktoba kabla ya tarehe ya uchaguzi nenda kajiandikishe ili upate haki yako ya kupiga kura, kwa sababu uchaguzi wa mwaka huu ni kwa ajili ya vijana.”

“Tunataka mchague viongozi mnaowataka kwa ajili ya maendeleo bora ya baadaye hivyo baada ya vipindi leo watakaopata nafasi waende kujiandikisha na wengine muende kesho au kesho kutwa,” amesema Makonda

Amesema kura za vijana ambalo ni kundi kubwa nchini zitachangia kupata viongozi waadilifu, kuondoa wala rushwa, wakandamiza haki za watu na kuwanyanyapaa.

Janeth Mazembe, mwanafunzi wa shule hiyo amesema, “kura nitakayopiga itafanya kazi ipasavyo kwa sababu nitampa kiongozi atakaye ondoa mabaya, rushwa.”

Eusebio Luhambati,  mkazi wa Mivinjeni ambaye tayari alikuwa na kitambulisho baada ya kujiandikisha amesema hatokuwa na hofu tena katika kupata baadhi ya huduma kutokana na kuwa na kitambulisho hicho.

“Kitambulisho changu kiliharibika, nikawa napata shida sana katika kupata hiduma nyingine lakini sasa nina amani na sina wasiwasi nasubiri uchaguzi na sitapata usumbufu wote,” amesema Lihambati.