Njia alizopita Fally Ipupa kwenye muziki
Muktasari:
Fally Ipupa alizaliwa Kinshasa, DRC, na tangu alipokuwa mdogo alipendelea kuimba pamoja na sanaa ya uigizaji. Jambo ambalo lilimpelekea kujitosa katika muziki wa mitaani kabla ya kuingia katika kundi la muziki ambalo lilimtambulisha mjini
Dar es Salaam. Fally Ipupa, ambaye jina lake halisi ni Fally Ipupa N’simba, ni mmoja wa wasanii wakubwa zaidi kutokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Huku akiwa ndio nyota aliyechangia kwa kiasi kikubwa muziki wa rumba kukubalika Kimataifa.
Fally Ipupa alizaliwa Kinshasa, DRC, na tangu alipokuwa mdogo alipendelea kuimba pamoja na sanaa ya uigizaji. Jambo ambalo lilimpelekea kujitosa katika muziki wa mitaani kabla ya kuingia katika kundi la muziki ambalo lilimtambulisha mjini.
Safari yake ya kimuziki ilianza rasmi mwaka 1999 alipojiunga na bendi maarufu ya ‘Quartier Latin International’ inayomilikiwa na mkongwe katika muziki wa rumba Koffi Olomidé.
Aidha katika bendi hiyo alianza kama dansa, lakini kutokana na nidhamu, kipaji na uwezo wake wa kipekee uliyowazidi wengi katika kundi hilo. Fally alipewa nafasi ya kuimba akishiriki katika ngoma kama Éternellement (Force de Frappe – 2000), Eputsha (Monde Arabe – 2004), Kamutshima (akiweka vocals), Effervescent (Effrakata –2001, ikiwa ni kolabo) na nyinginezo.
Ndani ya bendi hiyo Fally alijifunza mambo ikiwemo namna ya kutumbuiza jukwaani, utunzi pamoja na uzalishaji wa muziki jambo ambalo lilimjenga na kumfanya kuwa msanii kamili. Hata hivyo baada ya kujijenga kwa miaka kadhaa, Fally aliamua kujiondoa katika bendi hiyo na kwenda kuanza maisha akiwa kama msanii huru.
Kwakua alijizolea umaarufu kupitia kundi la ‘Quartier Latin International’ haikuwa ngumu kukubalika na mashabiki. Ambapo Albamu yake ya kwanza ya solo ilimuweka moja kwa moja kwenye ramani ya muziki Afrika na kufanya atambulike zaidi kimataifa.
Fally aliongeza ubunifu katika nyimbo zake ambapo alichanganya ladha tofauti ikiwemo rumba, R&B, Pop na Afrobeat jambo lililofanya muziki wake kupata mashabiki katika sehemu mbalimbali za dunia.
Kupitia albamu kama Droit Chemin, Arsenal de Belles Mélodies, Power “Kosa Leka”, Tokooos, Tokooos II na Formule 7, ziliendelea kumuweka katika hadhi ya msanii wa kimataifa akipata wasikilizaji zaidi Ulaya na Marekani.
Kwa sasa nyota huyo amekuwa na mafanikio makubwa huku akitamba na nyimbo kama Maria PM, Mayday, Science-Fiction na Bloqué. Mbali na hilo mwanzoni mwa mwezi huu aliandika historia na kuweka rekodi ya kuwa msanii wa kwanza wa Kiafrika kujaza Stade de France uwanja wenye uwezo wa kubeba watu 80,000. Huku akiandika historia kwa kuuza tiketi zote miezi minne kabla ya show.
Uwanja huo wa Stade de France jijini Paris, Ufaransa una uwezo wa kuchukua takribani watazamaji 80,698 katika mechi za mpira na rugby. Kwa matamasha makubwa ya muziki, uwezo unaweza kuongezeka hadi karibu watu 100,000 kutegemea mpangilio wa jukwaa na sehemu za kusimama.