Adele alivyokutana na mchumba wake Rich Paul
Muktasari:
- Akizungumza katika podcast ya Glass Half Full inayoendeshwa na Craig Melvin, Paul anasema kuwa alikutana na Adele kupitia rafiki yao mmoja, ila urafiki wao ulikuwa kwa kawaida sana na hakuna aliyekuwa na mpango huo wa kuja kuwa wapenzi.
Uingereza. Mwimbaji maarufu wa Soul na Pop kutokea Uingereza, Adele, 38, kwa muda sasa yupo katika uhusiano na wakala wa michezo kutokea Marekani, Rich Paul, 45, lakini ni kwa namna gani wawili hao walikutana hadi kuwa pamoja?
Akizungumza katika podcast ya Glass Half Full inayoendeshwa na Craig Melvin, Paul anasema kuwa alikutana na Adele kupitia rafiki yao mmoja, ila urafiki wao ulikuwa kwa kawaida sana na hakuna aliyekuwa na mpango huo wa kuja kuwa wapenzi.
“Nilikuwa nimemfahamu Adele kwa muda fulani. Unajua, unapokuwa kwenye mazingira haya ya watu maarufu, mara nyingi mnakutana kwenye mizunguko ileile ya kijamii,” alisema Paul na kuongeza.
“Lakini sikuwahi kuwa mtu wa kuvutiwa kimapenzi na watu waliokuwa kwenye mazingira hayo kwa sababu mara nyingi wanakumbana na mambo kama hayo kila wakati. Hivyo, kwangu haikuwa hivyo. Kila kitu kilikuja kutokea kawaida kabisa,” alisema.
Paul alisema walikuwa wakikutana mara kwa mara katika hafla mbalimbali, jambo lililowafanya kuzoeana zaidi.
“Sote tulikuwa kwenye mizunguko ileile ya kijamii. Tulikuwa tukikutana, kucheka na kufanya utani pamoja. Kwa kweli ulikuwa ni urafiki wa kawaida tu hadi pale ambapo nilipoanza kuvutiwa kihisia naye,” alisema.
Adele, mwanamuziki aliyetamba zaidi na wimbo wake, Hello (2015) ulioshinda tuzo tatu za Grammy 2017, alithibitisha kuchumbiwa na Paul mnano Agosti 2024 baada ya tetesi za muda mrefu.
Hata hivyo, Paula katika mahojiano hayo alisema kuwa ingawa alikuwa anazifahamu nyimbo maarufu za Adele zilizotikisa dunia, hakuwa msikilizaji mkubwa wa kazi zake zote hadi walipoanza kuwa karibu zaidi.
“Bila shaka nilikuwa nazifahamu nyimbo zake kubwa, lakini sikujua nyimbo zake nyingine kama ninavyozijua kwa sasa,” alieleza Paul.
Tetesi za uhusiano wao zilianza mwaka 2021 baada ya kuonekana hadharani pamoja kwa mara ya kwanza katika mchezo wa Ligi ya Kikapu Marekani (NBA).
Ikumbukwe kabla ya uhusiano huo, hapo awali Adele alikuwa ameolewa na Simon Konecki, ambaye katika ndoa yao walijaliwa kupata mtoto wa kiume aitwaye Angelo mwenye umri wa miaka 13 kwa sasa.
Akizungumza katika mahojiano na Oprah Winfrey mwaka 2021, Adele alimtaja Paul kama mtu mwenye ucheshi sana ambaye kila wakati anavutiwa naye.
“Paul ni mtu mcheshi sana na mwenye akili nyingi. Inanivutia sana kumtazama akifanya kazi zake,” alisema Adele.
Adele, mkali wa kibao cha Someone Like You (2011), aliongeza kuwa uhusiano wao umekuwa na utulivu na wenye furaha, na kwamba ilikuwa mara ya kwanza kwake kujipenda, pamoja na kuwa tayari kumpenda mtu mwingine na kupendwa kwa dhati.
Akiwa ameuza nakala zaidi ya milioni 120 za muziki wake duniani kote, Adele anashikilia rekodi ya kuwa msanii wa kike aliyeuza zaidi nchini Uingereza katika karne ya 21. Vilevile alitajwa kama msanii aliyefanya mauzo makubwa zaidi nchini Marekani miaka ya 2010.