Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Anko Kitime: Enzi zile kulikuwa na social evening

Muktasari:

  • Wimbo huu niliusikia kwa mara ya kwanza kupitia santuri iliyokuwa na label ya Saba Saba mwaka 1972 au 73. Maneno ya wimbo huu yalikuwa kama yafuatayo,

Dar es Salaam. Leo nimeamka kichwani kinaimba  kibao cha Chakula Kwa Jirani kilichoporomoshwa mwanzoni mwa miaka ya 70 na Tabora Jazz Band katika mtindo wao wa Segere Matata.

Wimbo huu niliusikia kwa mara ya kwanza kupitia santuri iliyokuwa na label ya Saba Saba mwaka 1972 au 73. Maneno ya wimbo huu yalikuwa kama yafuatayo,

Visa alivyotenda Wallace mama Ahhh

Sintovisahau maishani mwangu

Alinihamisha kwetu mimi ahh

Aliniambia nihame kwetu na kazi niache

Kumbe anidanganya nihame kwetu

Kisha anipe tabu mimi

Halali nyumbani Wallace sijui yu wapi?

Chakula nakula kwa jirani mimi sasa

Sabuni napewa na jirani mimi

Kulala nalala peke yangu mimi

Mafuta ya taa kwa jirani jamaa

Mwishowe jirani wamechoka sasa

Wallace kanifukuza niende kwetu

Na kazini wamekwisha nifukuza

Wimbo huu ulikuwa na utamu zaidi kwa kuwa wakati huo nilikuwa Chuo cha Ualimu Klerruu na mmoja wa rafiki zangu aliiitwa Wallace, basi ikawa kama vile ni wimbo wa kumtania yeye.

Hakika muziki zama zile ni tofauti sana na sasa, kwanza kwa aina ya utunzi wa ujumbe katika wimbo, na lililo wazi kabisa ni kuwa vyombo wakati huo vilipigwa na watu si kutengenezwa na mashine, na pia aina ya vyombo vilivyotumika, kila zama na mambo yake.

Tabora Jazz ilikuwa ni mojawapo ya bendi za Tanzania zilizoitikisa Afrika ya Mashariki na Kati. Kwa maelezo ya mwanamuziki mkongwe Dekula Kahanga Vumbi, ambaye asili yake ni Jamhuri ya Demokrasi ya Kongo,  alipokuwa mdogo alikuwa akizisikiliza nyimbo za bendi za Tanzania alikuwa akiota siku ambayo ataweza kuja Tanzania na kuziona bendi kama  Tabora Jazz Band, Mlimani Park Orchestra na JUWATA Jazz band.

Ukikumbuka kuwa huko Kongo ndiko kulikoanzia  bendi kongwe kama Negro Success, Conga Success, TP OK Jazz, Lipua Lipua, Orchestra Veve, Kamale na nyingine nyingi, na ukisikia kijana kutoka huko anawaza bendi za huku kwetu ni wazi tulikuwa na muziki uliokuwa ukivutia sana.

Lakini leo lililo kichwani mwangu si aina ya muziki, lakini ni teknolojia iliyokuweko wakati huo ambapo bendi zetu zilikuwa zinaweza kukonga nyoyo za wapenzi nje ya mipaka yetu. Kama nilivyogusia wiki iliyopita, mwanamuziki wa leo angepewa vifaa vilivyokuwa vinatumika miaka ya 60, nina uhakika ingekuwa ngumu kufanya kazi kwa maelezo kuwa vyombo hivyo havifai. Na si wanamuziki tu hata wasikilizaji wa muziki pengine nao wangedai kurudishiwa kiingilio chao, kutokana na vifaa ambavyo wangedai ni duni mno.

Nitoe mfano, nilipokuwa sekondari nusu ya mwisho ya miaka 60, kulikuweko na taratibu ya kuzikutanisha shule mbalimbali kwa shughuli iliyoitwa ‘Social Evening’ au wenyewe tuliita kifupi  tu ‘Sosho’.

Katika shughuli hiyo wanafunzi wa shule moja waliwaalika wenzao wa shule nyingine kwa ajili ya dansi. Mara nyingi shule ya wavulana iliwaalika wasichana au shule ya wasichana iliwaalika wavulana. Matayarisho yalikuwa ni mwenyekiti wa starehe na kamati yake kuhakikisha wanafanya lote liwezekanalo kutafuta mashine ya kupigia muziki ambayo kwa wakati huo ilikuwa ni ‘record player’ na pia kutafuta santuri za nyimbo zilizokuwa zinatamba wakati huo ili kufanikisha Sosho.

Record player kilikuwa ni chombo ambacho kilikuwa na uwezo wa kupiga santuri, hakikuwa chombo kikubwa na kwa miaka ya 60 chombo hiki kilikuwa kikitumia betri, maarufu kama ‘mawe ya tochi’. Player yenye kutumia betri 6 ilikuwa inaonekana ina nguvu sana. Hivyo wanafunzi walichanga pesa ya kununulia betri, na mara nyingine soda  na keki, kwa wageni tu watakaowaalika. Jambo jingine muhimu ilikuwa kutafuta pipa au mtungi mkubwa, ambao kazi yake ilikuwa ni kama amplifaya, hivyo spika ya player iliwekwa juu ya pipa au mtungi na hivyo kuongeza bezi na sauti ya spika. Spika za player zilikuwa na wastani wa watts 60. 

Shughuli zote zikiwa tayari wanafunzi mpaka kiasi cha mia 400 waliweza kuburudika kwa kucheza na kwa kutumia kaspika hako kamoja, na wengi wa enzi hizo ukiwauliza wanakumbuka hata nyimbo zilizokuwa zinapigwa katika shughuli hizo.

Siku hizi ukiangalia ukubwa wa mashine zinazotumika kwenye sherehe, unajiuliza maswali nini kimewatokea binadamu? Je wale wa zamani walikuwa na masikio bora au wa siku hizi wana masikio yenye uvumilivu zaidi? Si ajabu kumkuta mtu ana sub woofer ya watt 1000, chumbani kwake anasikiliza peke yake ili apate usingizi, hebu linganisha na zile watt 60 ambazo waliwezakucheza na kufurahi wanafunzi 400.

Shughuli za siku hizi hata kama ni sherehe ya shule ya chekechea, utakuta maspika makubwa yenye jumla ya maelfu ya watt ndio yanayotumika, na usishangae ukasikia watu wanalalamika eti hawasikii vizuri.

Vijana wengi wanavaa headphone masikioni, wanajipigia kelele hata gari lipige honi miguuni pao hawasikii, wengine wana spika kwenye magari zinawapigia kelele kuliko spika katika mikutano ya hadhara. Kitabibu tabia hii ni wazi itawaletea matatizo makubwa ya usikivu kadri umri wao unavyoongezeka.

Sifa moja ya muziki siku hizi ni kuwa muziki wenye kelele zaidi ndio unaposifika kuwa na ubora zaidi, lakini ndipo unaporudi nyuma na kujiuliza wale Tabora Jazz waliokuwa wakitumia pipa ili kupata bezi kwa muziki ambao ulikuwa hausikiki hata nyumba ya tatu, mbona sifa zao ziliweza kuvuka mipaka? Na kiukweli zinaendelea kudumu miaka zaidi ya 50 toka muziki wao umepigwa?