Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Anko Kitime: Teknolojia inavyobadili burudani ya muziki 

Muktasari:

  • Ya karne ya 19, ndipo wagunduzi wakagundua njia ya kuhifadhi sauti, na kwa mara ya kwanza. Miaka michache baadae chombo kilichoitwa gramophone kikagunduliwa na  kikawezesha  wanamuziki kuanza kurekodi muziki wao kwenye santuri  kukaanza aina mpya ya burudani ya kusikiliza muziki bila wanamuziki kuwepo

Dar es Salaam. Kwa sili watu waliburudika kwa muziki  kila kitu kikiwa mubashara. Wanamuziki walilazimika kufanya maonyesho yao mbele ya wapenzi wa burudani hiyo.  Na kabla ya matumizi ya umeme,  vyombo vilivyotumika viliweza kutoa mlio ambao haukuumiza masikio ya wasikilizaji, mfano ngoma, matarumbeta, piano na kadhalika.

Ya karne ya 19, ndipo wagunduzi wakagundua njia ya kuhifadhi sauti, na kwa mara ya kwanza. Miaka michache baadae chombo kilichoitwa gramophone kikagunduliwa na  kikawezesha  wanamuziki kuanza kurekodi muziki wao kwenye santuri  kukaanza aina mpya ya burudani ya kusikiliza muziki bila wanamuziki kuwepo.

Santuri za kwanza zilitengenezwa kwa  kemikali inayoitwa shellac. Santuri hizi zilihitaji uangalifu mkubwa kwani zilikuwa rahisi kuvunjika na kwa vile gramophone ilitumia sindano iliyokuwa ikipita juu ya santuri, hatimae baada ya kutumika sana santuri zilichubuka na kutokufaa tena. 

Teknolojia ya gramaphone ilianza kuwawezesha wanamuziki kusambaza muziki wao kwenye maeneo hata walikokuwa hawafahamiki.

Miaka michache baada ya ugunduzi wa gramophone, teknolojia ya kurusha matangazo hewani kutumia redio ikagunduliwa. Umma wa kusikiliza na kuburudika kwa muziki ukapanuka sana.  

Umuhimu wa gramophone uliendelea kwani ulimuwezesha mtu kusikiliza wimbo anaoutaka wakati anapotaka, tofauti na redio ambayo ilikuwa ikiendesha mambo yake kadri kituo cha redio kilivyopanga. Lakini ujio wa redio ulikuza biashara ya santuri kwani redio zilianza kutangaza santuri mpya. 

Wakati huohuo, iligundulika teknolojia ya kurekodi sauti katika kanda zilizoitwa  reel to reel. Kanda hizi zilikuwa zinahifadhi muziki kwa ubora kuliko santuri, na kwa kuwa mashinde za kupiga kanda hizi hazikutumia sindano, bali mawimbi ya sumaku, kadha ziliweza kuishi miaka mingi  bila kupungua ubora, lakini mapungufu ya kanda hizi ilikuwa ziliweza kukatika na pia zikikaribiana na sumaku ziliweza kufutika. 

Vyombo vya umeme vikaanza pia kuwa maarufu hasa baada ya mwaka 1920 ambapo teknolojia ya kutengeneza spika na amplifaya ilipokomaa. Sasa sauti ikaanza kuwa na nguvu zaidi japokuwa amplifaya zenyewe zilikuwa na nguvu za watt 5 mpaka 30.

Kati ya mwaka 1950 na 1960, santuri za shellac zikaanza kupotea na badala yake zikaingia santuri ndogo zilizotengenezwa kwa plastiki. Santuri hizi zilizokuwa maarufu kwa jina la ‘single’, kwani zilikuwa mviringi kama CD lakini ziliweza kupiga wimbo mmoja tu kwa kila upande. 

Ujio wake ulikuja sambamba na mashine zilizoitwa Juke Box, ambamo ndani yake kulikuwa na single nyingi, na kwa kilipia kiasi kidogo, uliweza kuchagua wimbo ulioupenda na kuusikiliza. Katika miaka ya 60 na 70, chombo hicho ndicho kilikuwa chanzo cha muziki katika baa maarufu hapa nchini.

Haikuchukua muda mrefu zikaanza kutengenezwa santuri ambazo zilikuwa na nyimbo nyingi. Santuri hizi ziliitwa Long play(LP), kwani zilipiga muziki kwa muda mrefu kutokana na uwingi wa nyimbo.

Mwaka 1927, kijana mmoja mdogo wa miaka 21, Philo Farnsworth, kwa mara ya kwanza akaweza kurusha picha hewani na kufungua ukurasa wa teknolojia ya luninga. 

Lakini ilikuwa baada ya vita ya pili ya dunia ndipo teknolojia hiyo ikaanza kuwa biashara rasmi. Mwanzoni mwa miaka ya 60 ndipo kukaanza kurushwa video za muziki. Watu wakaweza sasa kusikia na kuwaona wanamuziki kazini.  

Vyombo vya kupiga santuri (record player) viliendelea kuwa bora, kukawa na record player zilizoweza kubeba santuri nyingi kwa wakati mmoja na kuzipiga moja moja, record player hizi ambazo zilikuwa maarufu sana miaka ya sabini zilipewa jina la ‘changer’.

Mwaka 1963 kampuni ya Philips ilikuja na teknolojia mpya ya cassette (kanda za kaseti). Teknolojia hii iliboresha kanda za spool to spool, sikawa ndogo na kuwekwa katika kasha. Hakika teknolojia hii ilileta mabadiliko makubwa kwani kanda hizi zilikuwa rahisi sana kuzitunza na ziliweza kudumu miaka mingi bila kupungua ubora. 
Kanda za kaseti ziliingia nchini mwetu rasmi nusu ya pili ya miaka ya 70. Pale Arusha kulikuwako na kiwanda cha kutengeneza kanda hizo. Eneo lililokuwapo kiwanda hicho bado linaitwa Philips. 

Kanza za kaseti ziliwezesha mtu binafsi kurekodi nyimbo, tofauti na teknolojia ya santuri. Uwezo huu ukawafanya wafanya biashara waone fursa na ndipo ikaanza biashara iliyokuja kuwa kubwa sana, biashara ya kuuza kanda za muziki.

Katika miaka ya 80 kukaingia teknolojia ya Kanda za Video. Kutengenezwa video za muziki, na hakika zikaingia kanda za video za muziki kutoka kuila kona ya dunia. Kwa mara ya kwanza wapenzi wa muziki wakaanza kuwaona wanamuziki wao wakiimba na kucheza kwa staili mbalimbali. Wanamuziki nao wakajifunza mengi kutoka video hizi.

Miaka ya 90 kukaingia rasmi teknolojia ya CD. Kwa kuwa kulikuwa pia na maendeleo ya teknolojia ya kurekodi, CD zikawa maarufu kwani zilikuwa na muziki bora kuliko kanda za kaseti. Lakini CD, pamoja na ubora wa sauti, maisha yake ni mafupi kuliko kanda za kaseti. Upande wa video ukapata teknolojia mpya iliyoitwa VCD, yaani Video CD, hizi hazikudumu sana kwani ubora wake haukuwa wakuridhisha, kwa hiyo zilipoingia DVD, ukawa mwisho wa VCD.

Katika upande wa muziki wa majukwaani, maendeleo ni makubwa mno. Zilianza amplifaya za watt 30 mpaka 100, siku hizi watu hupanga spika zenye watt hata 20,000.  Si ajabu kabisha ukaingia kwenye baa ndogo lakini ina spika za watt 1000. Burudani ya kusikiliza muziki huku mnazungumza mipango inakufa taratibu, ukiingia baa nyingine jitayarishe kuharibika masikio.