Duma ataka uwekezaji zaidi

Muktasari:
- Duma alisema wasanii wengi bado hawajawekeza na badala yake wamekuwa wakitegemea malipo ya kwenye kazi za sanaa ndio maana baada ya sanaa wanakuwa tegemezi kwa jamii hata wanapofikwa na matatizo
Dar es Salaam, Mwigizaji na muongozaji wa filamu nchini, Daud Michael 'Duma' amewataka wasanii kujiwekeza kimaisha tofauti na kazi zao walizoeleka nazo ili kujikwamua na maisha ya baadae kuepuka kuwa tegemezi kwa jamii.
Akizungumza na Mwananchi, Duma alisema kuna baadhi ya wasanii hawana kazi binafsi wanazojivunia badala yake kila siku wanasema wao ni wakubwa na kusahau umaarufu wao hautoshi wanapaswa kuwa na vitu vya kujivunia maishani.
Duma alisema wasanii wengi bado hawajawekeza na badala yake wamekuwa wakitegemea malipo ya kwenye kazi za sanaa ndio maana baada ya sanaa wanakuwa tegemezi kwa jamii hata wanapofikwa na matatizo.
"Kazi hii sanaa sio ya kusema umetosheka na maisha hadi ujivunie nayo, inatakiwa wasanii kujiongeza kujiwekeza kwa vitu vingine sio kuitegemea pekee yake na msanii kujivunia umaarufu ni msala pale anapokuwa nje ya mfumo na kusumbua jamii kwa kuomba msaada.
Ni kweli msaada uwepo ila ikiwa tayari mhusika hasa masupastaa wakiwa wameshajiwekeza vya kutosha na sio kuishi kwa mazoea," alisema Duma anayetamba na kazi mbalimbali za filamu na tamthilia.