Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

EAGMA yazindua rasmi msimu wa pili, yaahidi makubwa Zaidi

Muktasari:

  • Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Julai 8, 2026, wakati wa uzinduzi rasmi wa msimu huo, Magreth alisema mafanikio ya msimu wa kwanza ulioanzishwa mwaka jana yamewapa hamasa ya kuendeleza tuzo hizo kwa lengo la kuwaunganisha wasanii wa injili, viongozi wa dini na wadau mbalimbali kutoka nchi za Afrika Mashariki.

Mkurugenzi Mkuu wa Centre Stage Group Company Limited na mwanzilishi wa East Africa Gospel Music Awards & Festival (EAGMA), Magreth Chacha, ametangaza rasmi kuanza kwa maandalizi ya msimu wa pili wa tuzo hizo, akisema zitaendelea kuwa jukwaa la kutambua na kuthamini mchango wa huduma ya muziki wa Injili katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Julai 8, 2026, wakati wa uzinduzi rasmi wa msimu huo, Magreth alisema mafanikio ya msimu wa kwanza ulioanzishwa mwaka jana yamewapa hamasa ya kuendeleza tuzo hizo kwa lengo la kuwaunganisha wasanii wa injili, viongozi wa dini na wadau mbalimbali kutoka nchi za Afrika Mashariki.

"EAGMA si tu tuzo za muziki wa Injili, bali ni jukwaa la kuujenga Mwili wa Kristo kwa kutambua, kuthamini na kuenzi ubora wa huduma za muziki wa Injili. Tunaamini kila anayemtukuza Mungu kupitia muziki anastahili kuwa sehemu ya familia ya EAGMA," alisema Magreth.

Alisema msimu wa pili utakuwa na utofauti na wa kwanza kwa kutambua na kutoa heshima maalumu kwa watumishi wa Mungu waliotoa mchango mkubwa katika kukuza muziki wa Injili, ikiwa ni njia ya kuthamini juhudi zao za kuandaa na kulea kizazi kipya cha waimbaji wa Injili.

Kaulimbiu ya msimu huu ni "Kupokea na Kukabidhi Kijiti cha Uongozi," ikilenga kuhamasisha urithishaji wa huduma kutoka kizazi kimoja kwenda kingine ili kuendeleza uinjilishaji kupitia muziki.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa, uzinduzi rasmi wa msimu wa pili pamoja na kufunguliwa kwa mapendekezo ya washiriki (nominations) utafanyika Agosti 1, 2026, katika Serengeti Hall, King Jada Hotel, Dar es Salaam. Tukio hilo linatarajiwa kuwakutanisha wasanii wa Injili, viongozi wa dini, wadau wa tasnia ya muziki, vyombo vya habari na wadhamini kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Somalia.

Aidha, Septemba 20, 2026, majina ya walioteuliwa katika vipengele mbalimbali yatatangazwa rasmi na upigaji kura kwa umma utafunguliwa, huku kilele cha utoaji wa tuzo kikitarajiwa kufanyika Novemba 14, 2026.

"Tunatoa mwaliko kwa taasisi za umma na binafsi, makampuni, makanisa, mashirika ya maendeleo, vyombo vya habari na wadau mbalimbali kuungana nasi katika safari hii ya kuendeleza Ufalme wa Mungu kupitia muziki wa Injili," alisema.

Aliongeza kuwa ushirikiano wa wadau utasaidia kukuza vipaji, kuwainua watumishi wa Mungu na kuhifadhi urithi wa muziki wa Injili kwa vizazi vijavyo.

EAGMA ilianzishwa mwaka 2025 ikiwa ni jukwaa la kutambua na kuenzi huduma za muziki wa Injili katika ukanda wa Afrika Mashariki. Msimu wa pili unatarajiwa kuwashirikisha washiriki kutoka nchi saba za ukanda huo, huku waandaaji wakiamini utakuwa mkubwa na wenye mafanikio zaidi kuliko msimu uliopita.