Getto Kids kutoka mitaani hadi kuwa nyota wa Kimataifa
Muktasari:
- Leo hii wanatajwa kuwa miongoni mwa vikundi vya watoto vinavyojulikana zaidi duniani kwa dansi, ambapo wameonekana katika video za mastaa wakubwa wa muziki, wametumbuiza mbele ya mamilioni ya watazamaji na sasa wamepata shavu la kushiriki katika fainali ya Kombe la Dunia 2026 pamoja na mwanamuziki maarufu duniani, Shakira.
Uganda. Kama kuna simulizi inayothibitisha kwamba kipaji kinaweza kubadili maisha ya mtoto kutoka mazingira magumu hadi kuwa nyota wa kimataifa, basi simulizi hiyo ni ya Getto Kids wa Uganda.
Leo hii wanatajwa kuwa miongoni mwa vikundi vya watoto vinavyojulikana zaidi duniani kwa dansi, ambapo wameonekana katika video za mastaa wakubwa wa muziki, wametumbuiza mbele ya mamilioni ya watazamaji na sasa wamepata shavu la kushiriki katika fainali ya Kombe la Dunia 2026 pamoja na mwanamuziki maarufu duniani, Shakira.
Lakini nyuma ya mafanikio hayo kuna panda shuka ambazo wamekumbana nazo ikiwamo maisha ya mitaani, changamoto katika ukuaji hadi kugeuza dansi kuwa daraja la mafanikio na sehemu ya kujipatia kipato.
Walikotoka
Getto Kids ni kundi la dansi la watoto kutoka Uganda. Kundi hilo lilianzishwa rasmi mwaka 2014 na Dauda Kavuma, akiwa na lengo la kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu hasa yatima na watoto wa mitaani waliokuwa wakiishi katika eneo la Katwe, Kampala.
Kwenye moja ya mahojiano yake Kavuma amewahi kueleza kuwa kwa miaka mingi Katwe imekuwa ikitambulika kama moja ya maeneo yenye changamoto za kiuchumi nchini Uganda. Badala ya kuwaacha watoto hao waendelea kupotea katika mazingira yasiyorafiki aliamua kuunda kundi hilo huku akitumia dansi kama njia ya kuokoa maisha yao.
Kabla ya kulifanya kundi hilo kuwa rasmi alianza kuwafundisha watoto hao kudansi tangu mwaka 2007 jambo ambalo baada ya kulizindua kama kundi rasmi mwaka 2014 hakupata changamoto yoyote ya kuwaelekeza kwani wote walikuwa wamekwiva.
Mwaka 2014 dunia ilianza kuwatambua Getto Kids baada ya kushiriki katika video ya wimbo wa ‘Sitya Loss’ wa mwanamuziki Eddy Kenzo ambaye naye ni mzaliwa wa Uganda.
Video hiyo ilitrend kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii na kuvutia mamilioni ya watazamaji duniani. Kilichowavutia wengi hakikuwa tu uwezo wao wa kucheza, bali ni vibe lao pamoja na ubunifu waliyouonesha katika video hiyo.
Umaarufu kupitia video hiyo uliwafungulia milango mipya ambapo walianza kuonekana katika majukwaa ya kimataifa wakiwa na vibe na ubunifu uliyofanya wakubalike kila kona ya dunia.
Siku zilizidi kwenda na madili kayaendelea kujipa, mwaka 2017 walionekana tena katika video ya wimbo ya Unforgettable wimbo wa rapa French Montana aliyomshirikisha Swae Lee.
Video ya wimbo huo ilirekodiwa Kampala jambo ambalo lilipelekea wimbo kuwa mkubwa zaidi na kufanikisha kukusanya zaidi ya watazamaji 1.8 bilioni katika mtandao wa YouTube huku ikiwafanya Getto Kids kuendelea kujikusanyia kijiji cha mashabiki wa kimataifa.
Kuonekana katika video hiyo kulibadilisha taswira nzima ya baadhi ya watu ambapo Getto Kids hawakuonekana tena kama watoto wa mtaani bali ni wasanii wenye uwezo mkubwa wa kufanya maajabu katika majukwaa makubwa duniani.
Kutoka Uganda hadi Britain’s Got Talent & America’s Got Talent: Fantasy League
Mwaka 2023, Getto Kids waliandika historia wakijitosa kushiriki mashindano maarufu ya vipaji ya Britain’s Got Talent. Onyesho lao lilivutia majaji na watazamaji kiasi kwamba jaji Bruno Tonioli aliwapa Golden Buzzer, hatua iliyowapeleka moja kwa moja katika hatua za juu za mashindano hayo.
Ingawa hawakushinda taji hilo, walipambana na kuishia hatua ya fainali jambo ambalo lilifanya kujiweka katika ramani ya dunia na kuthibitisha kuwa Afrika ina hazina kubwa ya vipaji vya watoto. Baada ya hapo walialikwa katika maonesho mbalimbali Ulaya, Asia na Mashariki ya Kati huku jina lao likizidi kukua.
Hata hivyo baada ya kutikisa katika Britain’s Got Talent, mwaka 2024 walishiriki katika shindano maalum la America’s Got Talent: Fantasy League. Katika mashindano hayo walifanikiwa kufika hatua ya nusu fainali (Semifinals) kabla ya kuondolewa.
Kuhusu kombe la dunia sio shida zao
Aidha wapo wengi wanaojiuliza ni kwa namna gani watoto hao wamefanikiwa kumshawishi Shakira kupanda nao jukwaani, ukweli ni kuwa kwa Getto Kids kushiriki Kombe la Dunia itakuwa si mara ya kwanza kwani waliwahi kushiriki katika Kombe la Dunia la Qatar 2022.
Kwani walihusishwa na kampeni za Kombe la Dunia Qatar baada ya video yao ya kucheza wimbo rasmi wa mashindano ‘Hayya Hayya (Better Together)’ kuvutia mashabiki wengi. Ambapo kundi hilo lilialikwa Qatar kushiriki shughuli mbalimbali za uhamasishaji zilizohusiana na michuano hiyo.
Hata hivyo kwa mwaka 2026 kilichowaokoa ni namna walivyodansi kwa weledi wimbo wa Dai Dai ambao Shakira amemshirikisha mkali wa Afrobeat Burna Boy. Jambo ambalo lilimvutia msanii huyo ambaye amewahi kutamba na wimbo wa Waka Waka’
Hatimaye nyota huyo wa Colombia alitangaza kuwa amewaalika Getto Kids kushiriki katika maonesho ya mapumziko ya fainali ya Kombe la Dunia 2026, hatua inayowapa nafasi ya kuonekana mbele ya mamilioni ya watazamaji duniani.
Ikumbukwe macho ya dunia nzima yatakuwa kwenye fainali za Kombe la Dunia ambapo mastaa kama Maddona, kundi kutoka Korea BTS pamoja na Shakira wakitarajiwa kuuwasha moto katika usiku huo.
Licha ya mafanikio yao kisanii, Getto Kids wamekuwa wakitazamwa kama alama ya matumaini kwa watoto wengi wa Afrika. Kupitia kundi hilo, mamia ya watoto wamepata nafasi ya kupata elimu, makazi na maisha bora kuliko yale waliyokuwa nayo awali.
Kila wanapopanda jukwaani, hawawakilishi Uganda pekee bali pia wanawawakilisha watoto wote wanaotoka katika mazingira magumu.
Kutoka kwenye vichochoro vya Katwe hadi kwenye jukwaa la fainali ya Kombe la Dunia, safari ya Getto Kids imekuwa ushahidi kwamba kipaji, nidhamu na fursa vinaweza kubadili maisha ya mtu.
Kwa watoto hao, dansi haikuwa burudani tu. Ilikuwa tiketi ya kutoka katika umasikini, njia ya kuonesha uwezo wao wa kupigania maisha bora. Kwa lugha nyepesi tunaweza kusema kuwa Getto Kids ni kama kombolela na wameamua kubutua mwenyewe.