Harmo kwa mashairi na 'melodi' yupo katika dunia yake

Muktasari:

Anaandika sana. Yes! Konde Boy anaandika kwa dunia ya sasa. Sioni nani mwenye uwezo huo kwa kizazi hiki. Kamsikilize kwenye 'Naogopa' ya Marioo, ‘Single’, ‘Bakhressa’, ‘Kama Unamjua’ ama rudi kwenye mipini yake akiwa bado ananata na 'biti' za 'Usafini'.

Anaandika sana. Yes! Konde Boy anaandika kwa dunia ya sasa. Sioni nani mwenye uwezo huo kwa kizazi hiki. Kamsikilize kwenye 'Naogopa' ya Marioo, ‘Single’, ‘Bakhressa’, ‘Kama Unamjua’ ama rudi kwenye mipini yake akiwa bado ananata na 'biti' za 'Usafini'. Siyo kuandika tu, hata 'melodi' zake na uwezo wa kutafuta visa vya kuandikia nyimbo zake...amejipata.

Kuandika na kutengeneza 'melodi', Harmonize anasimama peke yake juu ya mlima Kilimanjaro wasanii wenzake wa kizazi cha sasa wapo kwenye viunga vya mji wa Moshi. Wanamtazama kwa juu! Lakini kuna shida ninaiona sehemu. Tuendelee!

Washikaji wengi walishindwa kutumia muda wao vizuri. Leo wanajuta. Tatizo walipopata pesa badala ya mafanikio wakaanza kuvimba. Pesa bila usimamizi ina maisha mafupi kama funza.

Hatuwezi kulaumu wasanii tu, kama wasimamizi wa kazi zao wanaamini mafanikio ni gari. Hapa ujiulize Babu Tale na Chibu yupi ni meneja wa mwenzake? Tale anaamini Fid Q kakosa mafanikio kwa sababu hana gari. Na Mondi anawekeza pesa kwenye miradi 'deile'.

Akili za uwekezaji za Mondi hazitokani na kichwa kinachoamini mafanikio ni gari. Kaanza kununulia 'ndinga vicheche' vya mjini kabla ya utawala huu. Kama angekuwa na akili za meneja wake asingekuwa Mondi huyu tunayemuona.

Utajiuliza kwa nini Diamond ana wasimamizi wengi wa kazi zake? Hata wale tunaowaona kila siku hawatoshi. Kuna watu wengi zaidi wanaocheza mchezo wa akili zaidi. Mondi pekee kama binadamu ni taasisi, na bado anamiliki taasisi kadhaa.

Kabla ya Kiba kutangaza kurudi kwenye kiti chake. Na kudai hakuna aliyekikalia bali anafuta vumbi na kukalia upya. Tayari Mondi alikuwa maili nyingi mbele. Na 'intavyuu' moja tu ya Kiba ilizua 'bato' lililopo mpaka leo. Bila shaka timu ya Kiba ilijua kucheza karata vizuri.

Kiba alikuwa kama kaususa muziki. Ngoma kama ‘Dushelele’ aliitolea video mbovu kama zile za 'komonio' au 'kicheni pati' za uswahilini. Nyakati ambazo tayari madogo walishaanza kuvuka boda kutafuta vichupa vitamu zaidi. Ilikuwa ngoma kubwa yenye video mbovu. Kipindi hicho tayari Mondi alishadondosha ngoma zenye video kali tupu. Hajawahi kubahatisha kwenye video dogo. Na anabaki kuwa mwanamuziki pekee ambaye hajawahi kuuchezea muda hata kwa bahati mbaya.

Watu wa Kiba baada ya hapo walijua wanachofanya. Bila kuzungukwa na akili kubwa tungemuhifadhi kwenye makabrasha ya "Jamaa alikuwa mkali sana." 'Taimingi tamu'.

Ukitaka kuamini hilo tazama mafanikio makubwa ya Kiba yameanza wakati upi. Kuanzia ubora wa video na usambazaji wa kazi zake. Hapo kabla Kiba aliacha kazi zake zisambae zenyewe mitaa ya Kibira Nairobi na Mombasa. Hakuwa na timu.

Mondi alikusanya Fella, Babu Tale na Sallam. Ni kwamba wakati Said Fella na Babu Tale, walimiliki na kuyasimamia makundi ya wasanii kibao. Kama TMK Wanaume na Tip Top Connection. Mondi  aliunda kundi kubwa la mameneja wa kusimamia kazi zake.

Kuna vipaji vingi vimetoweka kwa kukosa usimamizi. Mandojo na Domokaya ni sehemu ya vipaji yatima. Ama kwa uzembe wao au fitna za 'gemu'. Kuna wale ambao waliamini pesa ndio mafanikio kamili. Walipopata senti wakaacha muda userereke kama gari bovu mtaroni.  Mafanikio siyo gari na nyumba. Hivyo ni vitu tu vya msingi kwa binadamu. Marehemu Remmy Ongala mafanikio yake hayatazamwi kwa nyumba zake za Sinza na Mbezi tu. Hizi fikra lazima ziteketezwe kwenye vichwa vya madogo hawa. Tunapoacha vijana waamini hivyo matokeo yake ndiyo kina Ferouz. Baada ya Jeep Cherokee tu, mizuka ya kazi ikaishia hapo. Akaona kishamaliza kila kitu. Ndivyo ilivyo hata kwa Juma Nature baada ya gari na kibanda cha kulala, hakutaka kusumbuka zaidi. Waandishi wakaanza kutangaza kama gari na nyumba ni mafanikio kwa msanii, wakavimba kichwawakabadili kuanzia madem, utembeaji, vyakula, viwanja vya kula bata, nywele rangi mpaka vilevi.

Unapoona Blue anaendelea kufanya kile alichofanya 2004 kwa ubora uleule. Mpe heshima yake. Tukirudi kwa Konde Boy, licha ya ubora wake wa kuandika na kutengeneza 'melodi'. Bado napata shaka na usimamizi wake wa kazi na maisha binafsi. Simuoni nje ya kuandika na 'melodi', video na studio. Simuoni kwingine akitawala.Kuendelea kusimama kisanii ni  ubora wake wa kuandika na 'melodi'. Nje ya hapo simuoni.