Harmonize na warembo damudamu
Muktasari:
- Utakumbuka Harmonize aliyetoka na ngoma yake, Aiyola (2015), ni miongoni mwa wasanii watano pekee wa Afrika Mashariki ambao video zao zimetazamwa zaidi ya mara bilioni 1 YouTube.
Dar es Salaam. Mwanzilishi wa Konde Music Worldwide, Harmonize, 32, ni kati ya wanamuziki ambao video za nyimbo zao zinapata mamilioni ya watazamaji katika mtandao wa YouTube ulioanzishwa miaka 20 iliyopita.
Utakumbuka Harmonize aliyetoka na ngoma yake, Aiyola (2015), ni miongoni mwa wasanii watano pekee wa Afrika Mashariki ambao video zao zimetazamwa zaidi ya mara bilioni 1 YouTube.
Hata hivyo, nyuma ya mafanikio hayo kuna juhudi kubwa zenye mwendelezo mzuri kati ya kazi moja hadi nyingine, pamoja na ubunifu unaozingatia mahitaji ya soko kadiri muda unavyozidi kwenda mbele.
Wakati wanamuziki na waongozaji video wakiumiza kichwa jinsi watakavyopata video vixens (warembo) wakali, kwa Harmonize ni tofauti kidogo kwani wakati mwingine huwatumia hata waimbaji wenzake katika video zake.
Mimi Mars, Feza Kessy na Abigail Chams ni baadhi ya wale waliosimama kama video vixen katika video za Harmonize na kuzitendea haki.
Je, lini na ni video za nyimbo zipi hizo?, makala haya inaendelea kuangazia hilo kama ifuatavyo.
1. Mimi Mars
Katika albamu ya kwanza yake Harmonize, Afro East (2020), kulikwa na nyimbo nyingi zilizofanyika vizuri, na mmoja wapo ni ‘Mpaka Kesho’ ambao video yake hadi sasa imetazamwa mara milioni 8.9 YouTube.
Katika video hii chini ya Hanscana, Harmonize anaonekana akipasua kuni katika mbuga ya Manyara, ndipo analetewa barua na mtoto. Barua inamjulisha kuwa mpenzi wake (Mimi Mars) anaolewa na raia wa kigeni mwenye fedha nyingi.
Lakini Mimi Mars hayupo tayari ila familia ndio inashinikiza kutokana ilishapatiwa kiasi kikubwa cha fedha kama mahari. Hata hivyo, wakati mipango hiyo ikifanyika, walikuwa wanajua binti yao yupo katika uhusiano na Harmonize.
Basi siku ya harusi, Mimi Mars anamuona Harmonize na kumkumbuka aliwahi kumpa kidani, anashika kifuani na kukikuta - kumbe alikivaa siku hiyo. Usiku wake, Harmonize anampigia simu Mars, mume wake alipoona akakasirika na kuripoti suala hilo ukweni.
Haikuchukua muda, mashemeji na baba mkwe wakaanza kumsaka Harmonize kila kona, mwishowe wakaenda kumkuta akiota moto peke yake, wakamkamata na kumfunga mikono nyuma na kumwagia maji ya baridi na kipigo kikali...!
2. Feza Kessy
Ndani ya albamu ya tatu ya Harmonize, Made For Us (2022) chini ya Konde Music, kuna wimbo unaitwa ‘Wote’ ambao video yake imefanyika Zanzibar ikiongozwa na Director Ivan.
Ndani ya video hiyo ameonekana Feza Kessy, mshiriki wa Big Brother Africa The Chase 2013, ambaye pia aliwahi kusainiwa na lebo ya rapa AY, Unity Entertainment mnamo mwaka 2012 akiwa na Ommy Dimpoz na Stereo.
Harmonize na Feza walifanya video ya ucheshi ambayo inaonyesha wapenzi waliopendana na wenye furaha ndani ya nyumba yao. Asubuhi wanapiga mswaki pamoja, kisha wanaenda kuvaa pamoja huku wakiruhusu utani wa hapa na pale.
Baadaye wanaenda sebleni kutazama movie huko wakipata vinywaji vikali pamoja na popcorn, kisha wanacheza game la soka na kumpumzika kwa muda kabla ya kwenda ufukweni kupata upepo.
Wanaporudi nyumbani, maisha yao ni yake yale yenye utani mwingi ambapo Harmonize anaonekana akiwa amevaa wigi la Feza huko akijitazama kwenye kioo.
Hata hivyo, Feza anachukua wigi lake na kuondoka nalo, kisha anamuita Harmonize ampake rangi kwenye kucha...!
3. Abigail Chams
Mwaka uliopita Harmonize alifanya vizuri zaidi kupitia wimbo wake, Furaha (2025) uliotayarishwa na Kimambo, huku video yake ambayo tayari imetazamwa YouTube mara milioni 37, ikiongozwa na Verse Network.
Katika video hiyo ameonekana Abigail Chams, mwimbaji wa Bongofleva aliyesainiwa Sony Music Africa, ambaye pia anashikilia rekodi kama msanii wa kwanza wa kike Afrika Mashariki kuwania tuzo za BET.
Video inapoanza, wawili hao wanaonekana wakiwa bafuni, Harmonize anajitazama katika kioo, kisha Abigail Chams anazama katika jakuzi lenye povu jingi. Baada ya wote kuvaa, Abigail anampa Harmonize zawadi ya ua zuri kisha wanatoka kwenda matembezi. Wanaenda katika moja ya hotel maarufu Dar es Salaam ambapo wanapata mapokezi maalumu, na Harmonize anatumia nafasi hiyo kumueleza Abigail ni kwa kiasi gani anampenda...!
Ikumbukwe huu ulikuwa ni mradi wa tano kwa Abigail Chams na Harmonize kufanya pamoja baada ya kushirikiana katika nyimbo nne - Closer (2022), Leave Me Alone (2022), Me Too (2025) na Lala (2025).