HEKAYA ZA MLEVI: Maisha ni uhalisia, si tamthilia
Katika maneno yenye tafsiri nyingi hakuna linalozidi “maisha”. Wapo wanaosema maisha ni vita, wengine wanadai maisha ni mchezo. Tena kuna wanaoamini kuwa maisha ni tunu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ukishamsikia mtu akimhusisha Mungu kwenye majibu yake basi ujue hataki maswali ya ziada. Hapo mtaishia kwenye imani maana kuamini ni kusadiki mambo hata kama huna uthibitisho nayo.
Maana ya maisha imewagawanya hata wasomi wakashindwa kuja na jibu la pamoja. Kuna wanaojibu “Maisha ni namna ya kuishi”. Hawa bado hawajasema kwani wanafanana na mwanafilosofia aliyeulizwa “Nini maana ya Filosofia”, akajibu “Ni kuishi kifilosofia”. Hapo bado hakuna jibu kwa kuwa pamoja na mtu kuitwa hivyo, bado hajajua maana yake. Alitakiwa kuelezea maana ya neno na kudadavua kwanini neno likawa.
Kuna huyu nimwite wa ajabu sana. Anasema “Naenda kutafuta maisha” wakati tayari ana maisha! Laiti angelikuwa zombi ningemwelewa kuwa anayatafuta maisha ya kibinadamu aache kuwafyonza damu wenzie. Anayatafutaje maisha wakati anayaishi? Au basi angesema anakwenda kutafuta maisha bora kuliko anayoishi. Hata hivyo ningemwuliza maisha bora ni yapi; mboga saba, magari ya kifahari au ni yapi?
Hebu tuwekane sawa. Kuna tofauti kubwa kati ya maisha mazuri na ukwasi. Wapo wanaodhani maisha mazuri yanapatikana kwenye utajiri, na mabaya yapo kwenye ukata. Lakini mimi huwa naishi kwa uhalisia; nawafahamu matajiri waliojilipua vichwa vyao kuyakatiza maisha hayohayo waliyoyahangaikia. Lakini pia wapo masikini wanaoyafurahia maisha mwanzo mwisho. Hivyo mali si jibu la maisha mazuri.
Wakati mwingine unaweza kumwonea huruma tajiri aliyetafuta fedha kwa nguvu zake zote toka ujana wake. Akajifungia kuanzia kule mwanzo kwa ukuta mrefu mithili ya mvinje, ukuta wenye kamera za ulinzi na nyaya za umeme. Geti kubwa na zito la chuma, mageti mengine kwenye milango ya kuingilia ndani pamoja na ya vyumbani, na milango ya mninga yenye makomeo na vitasa vinaofunga zaidi ya mara tatu tatu.
Mtu huyu analindwa zaidi ya gaidi aliyeko gerezani. Kampuni ya ulinzi wa nyumbani na ofisini, pamoja na msafara wa barabarani unaojumuisha majitu ya miraba sita yanayomlinda mwili pale anapotembea mtaani. Chakula chake kinaandaliwa na kampuni maalum kuepuka hujuma za sumu. Pia ana wataalamu wa afya wanaomkagua kila anapoamka, anapokula na anapolala.
Lakini Waswahili walisema “kuchamba kwingi kutoka na kinyesi”. Wanafilosofia waligundua ni kichaa au mtu asiye na akili timamu tu ndiye anayeweza kutunza kumbukumbu ya dakika na sekunde jambo linapotokea. Ndiyo maana mtu anapaswa kusahau baadhi ya mambo (hasa yaliyopita na yasiyo muhimu) ili aache nafasi ya ubongo kuingiza vitu vingine. Vinginevyo kila siku mtu angelazimika “kuflashi” ubongo aitafute nafasi kinguvu.
Nakumbuka siku moja nilimtungua kinda wa kunguru. Kumbe wenyewe waliniona nikifanya ukatili huo, hivyo wakanimaindi kupita maelezo. Kila nilipopita nao walinisindikiza wakinizomea “huyoo... huyooo!!!” Nikadhani wamenukuu makofia ninayoyavaa, lakini hata nilipotoka kichwa wazi hawakunisahau. Nikasema kweli hawa wadudu noma! Mkaanga samaki alilalamika wamemchukulia fungu la pelege na kichupa cha chachandu!
Uangalizi wa afya uliopitiliza unamfanya mtu aogope vyakula vya asili na matunda pori, na bila shaka atatumia zaidi vyakula vya kusindikwa. Kumbe hicho ni kinyume chake; haya makwasukwasu ya mtaani ndio yenye afya kuliko supu ya Hotelini. Mwanzoni tuliambiwa tusinywe sharubati za viwandani kwa sababu zina kemikali. Wataalamu wa kileo wakasema eti tusitumie sharubati za kukamua zina vijidudu. Sasa kemikali na minyoo kipi ni hatari zaidi?
Wakati mwingine watu wanashirikisha hisia zao katika kula. Sijui kama ungelamba asali iwapo ungeviona virutubisho anavyotumia nyuki kuisindika. Yule mshua wetu alipogundulika na mnyoo mmoja tu, alinyweshwa madawa pasi na wataalamu wake kujua kwamba mnyoo huo ulihitajika kumeng’enya chakula tumboni mwake. Akaishi tofauti na mwili wake, na hatimaye akaangukia kwenye maradhi yasiyoambukizwa.
Akili nyingi zina muda wa kutumika, lakini pia zina muda wa kupumua.
Kwa sababu ya kutumia akili, wasomi hawawezi kufanya biashara kibongobongo. Hata wale waliosomea biashara walijifunza milolongo mingi ya kodi, bima, akiba, dharura na kadhalika. Kila wakipiga hesabu hawaoni kama kuna biashara hapo. Ndio maana wakaamua kukwepa kodi na kufanya biashara za haramu. Wengine mpaka sasa wanabeti.
Lakini wakati huo huo, waliokimbia madarasa ndio wakawa wafanyabiashara wakubwa. Fikiria mtu anakusanya mtaji wake wote na mkopo juu, anafungasha lori la nyanya kutoka Iringa kuja Dar es Salaam. Hafikirii kwamba inaweza kutokea ajali nyanya zikatawanyika porini, au injini ikanoki nyanya zikaoza baada ya siku mbili. Wala hawazi kwamba majambazi wanaweza kuwatageti njiani. Na ndio maana wanafanikiwa.
Mwaka huu usiwaze sana; fanya lile unaloweza kulifanya ili umtukuze Mungu. Heri ya Mwaka Mpya 2025.