Huu muungano wa Rosa Ree, Fid Q basi burudani tele

Muktasari:
- Ametoa albamu, ameshinda tuzo za muziki Tanzania (TMA), ameshirikiana na wasanii wengi wakubwa wa ndani, huku kazi zake mahiri zikimpatia ushawishi kwa kundi kubwa la vijana Afrika Mashariki. Huyu ndiye Rosa Ree
Kwa miaka minane ndani ya tasnia, Rosa Ree amefanikiwa kutengeneza himaya yake na ushawishi hasa upande wa Hip Hop, hakuna ubishi kuwa jina lake tayari lipo juu katika orodha ya wachanaji wakali na bora Bongo kwa muda wote.
Ametoa albamu, ameshinda tuzo za muziki Tanzania (TMA), ameshirikiana na wasanii wengi wakubwa wa ndani, huku kazi zake mahiri zikimpatia ushawishi kwa kundi kubwa la vijana Afrika Mashariki. Huyu ndiye Rosa Ree;.
1. Kupatikana kwa jina lake la kisanaa, Rosa Ree, kunatokana na kutohoa jina lake la kuzaliwa ‘Rosary Robert’ akiwa ni mtoto wa mwisho katika familia yao ya watoto sita ambayo wote majina yao yanaanza na herufi ‘R’ kama lilivyo la baba yao mzazi.
2. Rosa Ree ni msanii wa kwanza na mwisho wa Hip Hop kusainiwa na rekodi lebo ya Navy Kenzo, The Industry ambapo mwaka 2016 alisaini pamoja na wenzake wawili, Seline na Wildad wanaofanya aina nyingine za muziki.
Navy Kenzo, kundi linaloundwa na Nahreel na Aika, tangu kuondoka kwa kina Rosa Ree katika lebo yao mwaka 2017, wamesaini msanii mmoja tu, The Great Eddy aliyetoka na EP yake, Small Bad Wolf (2021).
3. Alianza kuvuma kimuziki baada ya kuachia nyimbo zake mbili, One Time (2016) na Up In The Air (2017) uliofanya vizuri Bongo na kimataifa hadi kuingia tano bora chati za Soundcity, African Rox Countdown nchini Nigeria.
4. Nyimbo zote ambazo Rosa Ree kashirikishwa na Harmonize na Rayvanny ni remix. Vanny Boy alimpa shavu katika ngoma yake, Pochi Nene Remix (2018), huko Konde Boy akimvuta katika wimbo wake, Bedroom Remix (2020).
5. Wimbo wa Rosa Ree wenye mafanikio zaidi kwake ni Blueprint (2022) ulioshinda tuzo ya TMA 2022 kama Wimbo Bora wa Hip Hop ikiwa ni mara yake ya kwanza kushinda kipengele hicho tangu amevuma kimuziki.
Jina la wimbo huo kwa kiasi linashabiana na lile la albamu ya sita ya Rapa wa Marekani, Jay Z, The Blueprint (2001) iliyotoka chini ya Roc-A-Fella Records na Def Jam Recordings, huku ikiuza nakala 427,000 wiki yake ya kwanza sokoni.
6. Huyu ndiye msanii wa kwanza wa kike kushirikishwa na kundi la OMG (Young Lunya, Conboi na Salmin Swaggz) ambapo alisikika katika wimbo wao, Wanangu na Wanao (2018) uliotengenezwa na S2kizzy kipindi akiwa Switch Records.
7. Rosa Ree anaimilikia albamu yake ya kwanza, Goddess (2022) kwa asilimia 100 kutokana gharama zote za uandaaji zimetoka kwake na sio katika rekodi lebo au kampuni yoyote ya usambazaji muziki.
Albamu hiyo yenye nyimbo 17, Rosa Ree alifanya hivyo ili kuwa na hakimiliki ya kazi zake tofauti na wasanii wengi ambao albamu zao humilikiwa na wale wanaokuwa wanawasimamia kipindi zinapotoka.
8. Tayari Rosa Ree ameshinda tuzo tatu tofauti zinazomtaja kama Msanii Bora wa Hip Hop, ameshinda East Africa Arts & Entertainment Awards (EAEA) 2022, The Orange Awards 2022 na Tanzania Music Awards (TMA) 2022.
9. Rosa Ree ndiye msanii wa kwanza wa kike Tanzania kutajwa katika orodha ya wasanii wanaokubalika na Rick Ross, nguli wa Hip Hop Marekani na Mkurugenzi Mtendaji wa Maybach Music Group aliyetoka kupitia albamu yake, Port of Miami (2006).
10. Hadi sasa Fid Q ndiye msanii wa Hip Hop Bongo ambaye Rosa Ree kashirikiana naye katika nyimbo nyingi zaidi, wawili hao tayari wametoa nyimbo nne ambazo ni Ole Chizza (2018), Korasi (2019), Trust (2022) na Bigman (2023).
Ni Fid Q aliyetoa albamu tatu, Vina Mwanzo Kati na Mwisho (2005), Propaganda (2009) na KitaaOLOJIA (2019), huku akishinda tuzo nne za TMA ambapo mwaka 2006 ndipo aliposhinda ya kwanza kupitia wimbo wake ‘Mwanza’ uliotengenezwa na P-Funk Majani.