Jay Z kuadhimisha miaka 30 ya utawala wake kwenye hip hop
Muktasari:
- Jay Z, mkali wa kibao cha Young Forever (2009) kilichotayarishwa na Kanye West (Ye) huku akimshirikisha Mr. Hudson, anatarajia kufanya tamasha maalum huko Paris, Ufaransa na Los Angeles, Marekani.
Marekani. Mwanamuziki maarufu wa Hip Hop duniani kutokea Marekani, Jay Z, 56, yupo katika ratiba ya kufanya show kadhaa kwa ajili ya kusherehekea kutimiza miaka 30 tangu alipovuma kimuziki kwa mara ya kwanza mwaka 1996.
Jay Z, mkali wa kibao cha Young Forever (2009) kilichotayarishwa na Kanye West (Ye) huku akimshirikisha Mr. Hudson, anatarajia kufanya tamasha maalum huko Paris, Ufaransa na Los Angeles, Marekani.
Kwa mujibu wa Roc Nation, Jay Z atatumbuiza katika Uwanja wa Stade de France jijini Paris, Septemba 10 na baadaye atafanya tamasha lingine katika Uwanja wa SoFi uliopo Los Angeles, Oktoba 23.
Tiketi za matamasha hayo zitaanza kuuzwa kwa mauzo maalum ya Citi na Mastercard kuanzia Juni 11, huku mauzo ya kawaida kwa ajili ya mashabiki wote yakianza Juni 12 katika Live Nation.
Matamasha hayo yanakuja baada ya Jay Z kutumbuiza kwenye tamasha la Roots Picnic lililofanyika Philadelphia wiki chache zilizopita.
Katika tamasha hilo alishirikiana na kundi la The Roots na kuwakutanisha jukwaani baadhi ya wasanii waliowahi kuwa sehemu ya Roc-A-Fella Records, akiwemo Beanie Sigel, Freeway na Young Chris.
Moja ya sehemu zilizowakosha mashabiki wengi ilikuwa freestyle ya Jay Z kwa mtindo wa acappella na alisikika akijibu vijembe kutoka kwa baadhi ya watu waliowahi kuwa karibu naye, akiwemo Damon Dash, Drake, Kanye West na Nicki Minaj.
Mbali na matamasha ya Paris na Los Angeles, Jay Z pia anatarajiwa kufanya matamasha matatu katika uwanja wa Yankee kuazia Julai 10 hadi 12 mwaka huu.
Awali Roc Nation ambayo ni kampuni yake, ilikuwa imetangaza shoo mbili pekee, lakini baadaye ikaongezwa moja kutokana na mahitaji makubwa ya mashabiki baada ya tiketi za awali kuuzwa zote.
Matamasha hayo yanayoenda kwa mwendo wa bandika bandua, yanakuja wakati Jay Z akiendelea kuadhimisha mafanikio makubwa ya kazi yake ya muziki, huku albamu yake ya kwanza, Reasonable Doubt (1996), ikielekea kutimiza miaka 30 hapo Juni 25.
Jay Z, mzaliwa wa Brooklyn, wakati anaanza muziki hakuwa na fedha za kurekodi albamu hiyo, hali iliyomlazimu kwenda kufanya kazi katika mgahawa ili aweze kurekodi. Badala kukimbilia kusaini mkataba na lebo, Jay Z aliamua kuazisha yake, Roc-A-Fella Records.
Mwaka 1995, Jay Z kwa kushirikiana na wenzake, Damon Dash na Kareem 'Biggs' Burke, ndipo walianzisha kampuni hiyo ya rekodi lebo na usimamizi wa muziki na baadaye waliwasaini wasanii kama Kanye West, Cam'ron na Jadakiss.
Hivyo albamu hiyo ya kwanza ya Jay Z (Reasonable Doubt) ambayo ilikaa katika chati ya Billboard 200 kwa wiki 18, ilitolewa chini ya Roc-A-Fella, mradi ambao ni moja ya sababu za bifu lake la Nas.
Hata hivyo, mwaka 2005 waliuza asilimia 50 ya Roc-A-Fella kwa dau la Dola30 milioni kwenda Universal Music Group (UMG) ambayo ni kampuni mama ya Def Jam Recordings, huku Jay Z akiwa Rais Def Jam kwa mshahara wa Dola 10 milioni kwa mwaka.
Kwa jumla hadi sasa Jay Z ametoa albamu 13, pamoja na albamu nne za ushirikiano, huku akiwa ameuza nakala za muziki wake zaidi ya milioni 125.
Tayari ameshinda tuzo 25 za Grammy, idadi inayomfanya kuwa msanii namba nne duniani mwenye tuzo nyingi zaidi za Grammy na msanii wa pili wa hip hop mwenye tuzo nyingi zaidi za Grammy.
Mwaka 2008, ndipo Jay Z alianzisha kampuni ya Roc Nation ikiwa imejikita kutoa huduma katika tasnia burudani kama wakala wa usimamizi wa wasanii na wanamichezo chini ya Roc Nation Sports.
Ikiwa na makazi yake New York na Los Angeles, Marekani pamoja na London, Uingereza, vilevile Roc Nation inajishughulisha na utayarishaji filamu, vipindi vya televisheni n.k.
Hadi sasa Roc Nation imeweza kufanya kazi na wasanii kama J. Cole, Rihanna, DJ Khaled, Kelly Rowland, Alicia Keys n.k.
Mwaka 2019, Jarida la Forbes lilimtambua Jay Z kama msanii wa kwanza wa Hip Hop duniani kufikia hadhi ya ubilionea akiwa na utajiri wa Dola 1 bilioni na sasa umeongezeka na kufikia Dola 2.8 bilioni, wastani wa Sh7.3 trilioni.
Aprili 4, 2008, Jay Z alifunga ndoa na mpenzi wake wa muda mrefu, Beyonce Knowles, 44, ambaye tayari wamejaliwa watoto watatu pamoja, Blue Ivy (2012), na pacha Rumi na Sir (2017).
Tarehe yao ya kufunga ndoa, yaani Aprili 4 ilikuwa na maana kubwa kwao na muhimu kwa sababu wana uhusiano wa karibu na namba 4, uhusiano huo unakuja kwa maana Beyonce alizaliwa Septemba 4 huku Jay Z ikiwa ni Desemba 4.
Kutokana na hilo, badala ya kuvishana pete, wote wawili walichora tattoo yenye alama ya namba nne ya kirumi 'IV' katika vidole vyao vya pete lengo likiwa ni kuonyesha kuheshimu namba hiyo ambayo wanaitaja kama ya bahati katika maisha yao!.