Marioo namba moja kwa Mimi Mars
Muktasari:
- Mimi Mars aliyevuma zaidi na ngoma, Ex (2019), akimshirikisha Mwana FA (Hamis Mwinjuma) ambaye sasa ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, yeye na Marioo wana simulizi ndefu
Dar es Salaam. Tangu ametoka kimuziki rasmi miaka zaidi ya minane iliyopita, Mimi Mars (33), ameshirikiana na waimbaji wenzake wengi ila Marioo (30), anabaki kuwa namba moja na wa kipekee kwake kwa sababu kadhaa.
Mimi Mars aliyevuma zaidi na ngoma, Ex (2019), akimshirikisha Mwana FA (Hamis Mwinjuma) ambaye sasa ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, yeye na Marioo wana simulizi ndefu.
Staa huyu aliibuka katika Bongofleva na wimbo wake, Sugar (2017) uliyotayarishwa High Table Sound, ikiwa ni baada ya kusainiwa na Mdee Music, rekodi lebo ya dada yake, Vanessa Mdee.
Wimbo huo ulipokelewa vizuri hadi kupelekea Coke Studio Africa kumpa Mimi Mars nafasi ya kutumbuiza kama Msanii Chupukizi (Big Break Artist) 2018, huku akitabiriwa kuja kufanya makubwa.
Akiwa anaijenga chapa yake katika Bongofleva, Mimi Mars alitokea kukielewa sana kipaji cha Marioo kama mtunzi na mwimbaji mkali mwenye melodi tamu hasa katika nyimbo zake za mapenzi na kubembeleza.
Kwa asilimia kubwa hilo ndilo lilimsukuma Mimi Mars kumshirikisha Marioo katika nyimbo zake mbili, Una (2019) na La La (2022) ambazo zilipokelewa vizuri na kutengeneza upekee niliyoutaja hapo awali.
Mosi; Marioo, mwanzilishi wa Bad Nation Label, ndiye mwimbaji pekee Bongo aliyeshirikishwa na Mimi Mars katika nyimbo mbili na zote video zake zikafanikiwa kutazamwa zaidi ya mara milioni 1 YouTube.
Kuna wasanii wengine ambao Mimi Mars amerekodi nao mara mbili, mathalani Young Lunya, ila kolabo hizo zimeshindwa kuwa kubwa kama hizo alizopiga na Marioo, staa aliyeibuka na kibao chake, Dar Kugumu (2018).
Pili; Kolabo yao, Una (2019), ndio wimbo namba moja kwa Mimi Mars kufanya vizuri zaidi YouTube ukiwa umetazamwa zaidi ya mara milioni 2.6, ikiwa ni miaka mitano tangu video yake imeachiwa.
Una (2019) ni wimbo wa mapenzi ambapo Mimi Mars anaeleza mchanganyiko wa hisia alizonazo kwa mpenzi wake kutokana na mambo mazuri anayomfanyia kila mara kiasi cha kumpagawisha!.
Na kazi hizo mbili ndizo hasa zilipelekea kukawa na madai kuwa wawili hao wana uhusiano wa kimapenzi ingawa kila mmoja kwa wakati wake alikanusha jambo hilo, hivyo ukabaki kama uvumi wa mitandaoni.
Mei 2022, wawili hao walionekana pamoja akifanya mazoezi ufukweni asubuhi lakini ikaja kubainika huo ulikuwa ni mpango wa kuutangaza wimbo wao ‘Una’ uliotayarishwa na Gachi B.
Hata hivyo, akiongea na Podcast, Swahili Radio by Audiomack, Marioo alisema ukaribu wake na Mimi Mars ulikuwa ni kwa ajili ya kumfundisha Kiingereza maana mwenzake ana msingi mzuri wa lugha hiyo.
Mbali na Marioo, Mimi Mars aliwahi kuhusishwa na Young Lunya, Diamond Platnumz na Joh Makini, ila alikanusha akieleza wengine ni kaka zake, wengine wadogo zake, na pia ni ukaribu wa kikazi tu.
Wakati Mimi Mars akifanya kolabo mbili na Marioo, ila cha kushangaza hadi dada yake, Vanessa Mdee anatangaza kuachana na muziki alikuwa hajarekodi naye wimbo wowote wa Bongofleva.
Kolabo pekee waliyonayo ni ile waliyoshirikishwa na dada yao mkubwa, Nancy Hebron katika wimbo wake wa Injili, Beautiful Jesus (2017).
Wakati anatambulishwa Mdee Music, Mimi Mars alisema hana haraka kufanya kazi na Vanessa kwani anataka mashabiki waone uwezo wake kwanza akilenga kuepuka kuonekana anabebwa na dada yake.
Hadi sasa Mimi Mars ametoa Extended Playlist (EP) mbili, The Road EP (2018), Christmas with Mimi Mars (2021), huku akishinda tuzo ya East Africa Entertainment Awards (EAEA) 2025 kama Female Vocalist of the Year.
Ikumbukwe kabla ya muziki, Mimi Mars alianza kutangaza akiwa na kipindi chake cha umbea katika TV, Weekend Gossip, na baada ya kutoka kimuziki akaonekana tena kwenye kipindi cha The Trendy Show.
Na hiyo ni sawa na dada yake, Vanessa ambaye kati ya mwaka 2007 na 2011, alikuwa mtangazaji na kuweza kufanya mahojiano na wasanii wakubwa duniani kama Rick Ross, Ludacris na Kelly Rowland, mwanachama wa Destiny’s Child.