Miss Universe yakanusha uwepo wa Miss Saudi
Muktasari:
- Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa katika tovuti ya shindano hilo, mchakato wa uteuzi wa washiriki haukufanyika nchini Saudi Arabia, hivyo waandaaji wamewataka wadau mbalimbali kupuuza madai hayo kwa kuwa ni ya uongo na ya kupotosha.
Wakati Miss Saudi Arabia mwaka 2021, Rumy Alqahtani akitangaza kushiriki katika mashindano ya urembo ya dunia ya Miss Universe, waandaaji hao wamekanusha kuwepo kwa mwanamitindo huyo kwenye mashindano hayo yanayotarajiwa kuanza Septemba 28, nchini Mexico.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa katika tovuti ya shindano hilo, mchakato wa uteuzi wa washiriki haukufanyika nchini Saudi Arabia, hivyo waandaaji wamewataka wadau mbalimbali kupuuza madai hayo kwa kuwa ni ya uongo na ya kupotosha.
Aidha, taarifa hiyo imeongeza kuwa Saudi Arabia haitakuwa na fursa ya kujiunga na shindano la Miss Universe hadi pale mchakato wa kumchagua atakayewakilisha nchi hiyo utakapokamilika na kuthibitishwa na kamati ya kuidhinisha.
Licha ya taarifa hiyo kutolewa, mpaka sasa Serikali ya Saudi Arabia haijaweka wazi kuhusu taarifa hiyo.
Zaidi ya washiriki 100 kutoka mataifa mbalimbali wanatarajia kushiriki katika shindano la Miss Universe mwaka huu, huku mshindi wa mwaka jana Sheynnis Palacios kutoka nchini Nicaragua, akijiandaa kumvisha taji mshindi wa mwaka huu.