Muziki enzi za mzee Ruksa

Muktasari:

  • Uchaguzi wa wakati huo ulikuwa ni wa chama kimoja, hivyo katika nafasi ya Urais kulikuwa na mgombea mmoja tu, Mzee Ally Hassan Mwinyi, na katika karatasi ya kura ya nafasi ya Urais kulikuwa na picha ya mgombea na nafasi za kutia alama  ya Ndiyo au Hapana. Ndiyo maana ya maneno ya wimbo ule, kuwa Ally Hassan Mwinyi apewe kura za ndiyo.

Kura za ndiyooooo’, hayo yalikuwa maneno katika wimbo wa kampeni ya uchaguzi mwaka 1985. Ulikuwa ni uchaguzi mkuu ambao  kwa mara ya kwanza Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa hagombei nafasi  ya Urais. Zamu ilikuwa na Ally Hassan Mwinyi. Wimbo huu ulikuwa ni utunzi wa Vijana Jazz Band, bendi iliyokuwa inamilikiwa na Umoja wa Vijana wa CCM na wakati huo ikiongozwa na Hemedi Maneti.

Uchaguzi wa wakati huo ulikuwa ni wa chama kimoja, hivyo katika nafasi ya Urais kulikuwa na mgombea mmoja tu, Mzee Ally Hassan Mwinyi, na katika karatasi ya kura ya nafasi ya Urais kulikuwa na picha ya mgombea na nafasi za kutia alama  ya Ndiyo au Hapana. Ndiyo maana ya maneno ya wimbo ule, kuwa Ally Hassan Mwinyi apewe kura za ndiyo.

Mzee Ally Hassan Mwinyi alishinda kwa kura nyingi za ndiyo na akawa Rais wa Tanzania wa Awamu ya Pili. Hali ya uchumi wa nchi haikuwa nzuri, hivyo alianza kazi katika kipindi kigumu sana.

Ili kuweza kuiongoza nchi kuvuka hali hiyo, mambo kadhaa ya awamu ya kwanza ya uongozi wa nchi hii yakalazimika kubadilika. Kati ya makubwa yaliyobadilika ni kuruhusu biashara ya soko huria na kuiondoa serikali katika kufanya biashara iliyokuwa ikifanywa na mashirika mengi ya umma, na kuondoa dhana ya kuwa kutajirika si jambo jema.

Ikawa rukhsa kufanya yale ambayo awali yalionekana ni dhambi kubwa. Na ndipo Mzee Ally Hassan Mwinyi akapewa jina la utani la Mzee Rukhsa. Wakati huohuo, kukawa na kampeni za kulazimisha viongozi wa nafasi za umma kuwajibika, na Rais akatamka, ‘Wasiowajibika watafagiliwa na fagio la chuma’, na kama ilivyokuwa kawaida nyakati zile matamko ya Rais au serikali haraka yalitungiwa nyimbo. Kwaya, bendi , vikundi vya taarabu vilitunga nyimbo nyingi kuhusu kuwajibika.

Bendi iliyokusanya mabingwa mbalimbali katika muziki wa dansi, iliyoitwa Tanzania All Stars iliyowakusanya kina Marijan Rajab, Mzee Gurumo, Zahir Zollo, Aziz Varda na Yunus Varda na wanamuziki mabingwa wengine wengi wa zama hizo, ilitunga wimbo mzuri sana ulioitwa Kuwajibika. Na kibwagizo chake kilikuwa, ‘Usipowajibika ole wako, utakumbwa na fagio la chuma’.

Kama zilivyofanya bendi nyingine, Tancut Almasi Orchestra, bendi iliyokuwa na masikani yake Iringa, mimi nikiwa mmoja  wa wanamuziki wake tulikuwa na wimbo ulioitwa kuwajibika uliotungwa na marehemu Mzee Zacharia Daniel ‘Tendawema’.

Tendawema lilikuwa jina lake la utani kutokana na kutunga wimbo ulioitwa ‘Tenda wema nenda zako’ aliouimba alipokuwa Shinyanga Jazz Band.

Waimbaji wa wimbo huu wa Kuwajibika walikuwa Zacharia Daniel, Kasaloo Kyanga, Kyanga Songa, Mohamed Shaweji na Hashim Kasanga, ambao wote kwa sasa ni marehemu.

Baadhi ya maneno katika wimbo huo yalikuwa,
Mtanzania mwenye moyo wa kizalendo, ni lazima awajibike.Awajibike awajibike kwenye maswala ya kazi,
Kuwajibika maana yake ni kujituma wewe mwenyewe usingoje kusimamiwa,
Tufanye kazi bila kusukumwa ndugu wazalendo

Ni wazi ujumbe bado ni sahihi hata leo na hata milele. Mwishoni mwa mwaka 1989 nilihamia Vijana Jazz Band, na katikati ya mwaka 1990 tarehe ya uchaguzi mkuu ikatangazwa, Vijana Jazz Band kama ilivyokuwa kawaida tukaanza kutayarisha nyimbo za kampeni.

Mzee Ally Hassan Mwinyi alikuwa ametangazwa tena kuwa mgombea wa nafasi ya Urais kwa kipindi kingine cha miaka mitano. Uchaguzi ulikuwa bado ni ule wa kura za Ndiyo au Hapana.  

Kwa kuwa wimbo wa kampeni ya Urais mwaka 1985, ulikuwa maarufu sana tukaona tusiubadili sana na hivyo kwa mara nyingine kibwagizo cha Ally Hassan Mwinyi apewe kura za ndiyo kikarudi tena, bahati mbaya wakati huu Hemedi Maneti alikuwa amekwisha fariki na bendi ilikuwa inaongozwa na Shaban ‘ Wanted’ Yohana Mwanasande.

Kama ilivyokuwa mwaka 1985, wimbo huo mpya ulipendwa sana kwenye kampeni za uchaguzi za mwaka 1990,  ulikuwa rahisi kiasi cha kuweza kuimbwa hata na watoto wadogo, hivyo ukafanikisha nia yake ya kuwa wimbo wa kampeni.

Katika kipindi cha Mzee Ally Hassan Mwinyi, muziki wa  bendi na Taarab uliendelea kuwa muziki pendwa kwa Watanzania. Nyimbo nyingi ambazo hupigwa na bendi mbalimbali  mpaka leo zilitungwa na kurekodiwa wakati wa uongozi wa Mzee Mwinyi.

Karibu kila mji ulikuwa na kumbi iliyojengwa aidha na serikali au Chama Cha Mapinduzi. Muziki ulipigwa katika mabwalo ya majeshi mbalimbali, wanamuziki waliweza kuishi kwa kutegemea muziki tu.  Hakika kipindi cha Mzee Ruksa kilikuwa kizuri kwa muziki wa dansi na Taarab.