Muziki na maajabu yake kwenye maisha ya binadamu
Muktasari:
- Muziki unaweza kukusaidia kuzingatia na kuongeza juhudi katika ufanyaji wa kazi, kupitia muziki unaweza kukusaidia kufanya kazi kwa juhudi zaidi tena wakati mwingine bila hata kugundua.
Dar es Salaam, Umewahi kujiuliza kwa nini unasikiliza muziki? Au muziki una faida gani kwenye maisha yako? Kama hukuwahi, fahamu kuwa muziki una vingi vya kuvutia na umuhimu kwenye maisha yako.
Vitu vya kuvutia kuhusu Muziki
Kuzingatia kazi
Muziki unaweza kukusaidia kuzingatia na kuongeza juhudi katika ufanyaji wa kazi, kupitia muziki unaweza kukusaidia kufanya kazi kwa juhudi zaidi tena wakati mwingine bila hata kugundua.
Hili linajidhihirisha kwa baadhi ya watu wanaopenda kufanya mazoezi ya mwili hupata aina ya muziki ambayo huwapa motisha zaidi na kuwafanya wasihisi uchovu na maumivu ya mazoezi.
Husaidia afya ya moyo
Akizungumzia umuhimu wa muziki kwa afya ya moyo, Mkuu wa Kitengo cha Utafiti na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo (JKCI), Dk Pedro Pallangyo alisema muziki ni tiba kwa wagonjwa hao na tayari njia hiyo inatumika kwa baadhi ya mataifa.
“Kwenye upande wa tiba huku kwetu bado hatujafanyia utafiti lakini kwa wenzetu ni kitu ambacho kimethibitishwa kwa utafiti kwamba kwenye upande wa moyo na maumivu hasa kwa wale wagonjwa kama wa saratani na kwa ambao moyo umefeli muziki umeonekana kuwasaidia kuondoa maumivu kwa kiasi kikubwa.
“Pia wagonjwa hao wa moyo inawasaidia kuacha kuzingatia dalili ambazo zinawatesa na matokeo yake muziki huwapa amani na kuwapunguzia mateso,” alisema.
Alisema muziki ambao mgonjwa anaupendelea huwa na msaada lakini kuna aina ya muziki ambao umethibitishwa kwa ajili ya wagonjwa wenye kufariji moyo.
Muziki hubadilisha mitazamo
Hii ni moja ya ukweli wa kuvutia wa kisaikolojia kuhusu muziki, kuhusiana na jinsi unavyoona ulimwengu unaokuzunguka. Nyimbo zenye maneno ya faraja humfanya mtu awe na furaha na wakati mwingine hubadili mtazamo wa ugumu wa maisha kuwa faraja.
Kuimba hupunguza mawazo
Kuimba muziki kunaweza kupunguza msongo wa mawazo pindi unapoimba au kusikiliza muziki uupendao.
Muziki ni lugha ya kimataifa
Muziki hutumika kama lugha ya kimataifa kwani wapo baadhi ya watu hupenda kusikiliza nyimbo ambazo hata hawaelewi lugha iliyotumika kwenye mashairi yake. Na hapo ndipo muziki huunganisha watu duniani.