Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nyimbo tano zilizotikisa historia ya Kombe la Dunia 

Muktasari:

  • Kupitia Kombe hilo baadhi ya nyimbo, zimejibebea utambulisho kimataifa. Miongoni mwa nyimbo zilizowahi kutolewa kwa ajili ya Kombe la Dunia.

Dar es Salaam. Katika Kombe la Dunia la FIFA mbali na burudani inayopatikana uwanjani kwa dakika 90. Mashindano hayo yamekuwa yakiacha alama kubwa katika ulimwengu wa muziki kupitia nyimbo rasmi zinazobeba ujumbe kwa mashabiki wa mchezo wa mpira wa miguu.

Kupitia Kombe hilo baadhi ya nyimbo, zimejibebea utambulisho kimataifa. Miongoni mwa nyimbo zilizowahi kutolewa kwa ajili ya Kombe la Dunia. Hadi sasa hakuna iliyofanya vizuri ikaizidi "Waka Waka (This Time for Africa)" ya Shakira aliyoshirikiana na kundi la Freshlyground kutoka Afrika Kusini. 

Wimbo huo ulitolewa Aprili 28, 2010 kuelekea Kombe la Dunia lililochezwa Afrika Kusini. Ambalo lilikuwa la kwanza kufanyika barani Afrika.

Picha ya mwanamuziki Shakira ambaye wimbo wake 'Waka Waka' unaongoza kufanya vizuri katika nyimbo za Kombe la Dunia 

Miaka 16 sasa, Waka Waka bado inaendelea kuweka rekodi. Video yake imetazamwa zaidi ya mara bilioni 4.4 katika mtandao wa YouTube. Huku ikiwa imefikisha zaidi ya streams bilioni 1.07 katika jukwaa la Spotify.

Takwimu hizo zimeifanya kuwa wimbo wa Kombe la Dunia uliosikilizwa zaidi katika historia ya jukwaa hilo la muziki. Mbali na hilo, wimbo huo uliuza zaidi ya nakala milioni 15 duniani kote na kuongoza chati za muziki katika zaidi ya nchi 15.

Kabla ya enzi ya Shakira, wimbo uliokuwa ukitajwa zaidi katika historia ya Kombe la Dunia ulikuwa 'La Copa de la Vida (The Cup of Life)' wa Ricky Martin. Wimbo huo ulitolewa Machi 9, 1998 kuelekea Kombe la Dunia lililochezwa Ufaransa.

Kwa mara ya kwanza mashabiki walishuhudia wimbo wa Kombe la Dunia ukiwa hit kubwa duniani na kumgeuza Ricky Martin kuwa nyota wa kimataifa.

'La Copa de la Vida' uliuza zaidi ya nakala milioni tano na kufanikiwa kushika nafasi ya kwanza katika chati za muziki za zaidi ya mataifa 30. Hadi leo, wengi wanautaja kuwa moja ya nyimbo zilizobadilisha historia ya muziki katika michezo duniani.

Hata hivyo Kombe la Dunia la mwaka 2010 pia lilizalisha wimbo mwingine uliotikisa dunia, 'Wavin' Flag' wa msanii wa Somalia aliyezaliwa Canada, K'naan. Ingawa haukuwa wimbo rasmi wa FIFA, ulitumika katika kampeni ya Coca-Cola na kufanikiwa kuuteka ulimwengu kwa ujumbe wake wa matumaini na ushindi.

Wimbo huo uliongoza chati katika nchi mbalimbali za Ulaya na Afrika na hadi sasa unaendelea kutumika katika matukio makubwa ya michezo. Mwaka 2014, Brazil ilipopokea Kombe la Dunia, FIFA ilizindua wimbo 'We Are One (Ole Ola)' uliowakutanisha Pitbull, Jennifer Lopez na Claudia Leitte.

Picha ya mwanamuziki Jennifer Lopez

Wimbo huo ulitolewa Aprili 8, 2014 na mara moja ukawa gumzo katika majukwaa mbalimbali ya muziki duniani. Video yake ilikusanya mamia ya mamilioni ya mitazamo kwenye YouTube. Huku ukitawala redio nyingi wakati wa mashindano hayo.

Katika mwaka huo huo, Shakira alirejea tena na wimbo 'La La La (Brazil 2014)' aliomshirikisha Carlinhos Brown. 

Wimbo huo ulitolewa Mei 22, 2014 na kufanikiwa kuvutia mashabiki wengi hasa kutokana na kuwashirikisha baadhi ya mastaa wakubwa wa soka katika video yake. Mpaka sasa video hiyo umetazamwa zaidi ya mara bilioni 1.3 kwenye YouTube, jambo linalothibitisha ukubwa wa Shakira katika nyimbo za Kombe la Dunia.

Kwa ujumla, takwimu zinaonyesha kuwa 'Waka Waka' ndiyo wimbo uliofanikiwa zaidi katika Kombe la Dunia. Mafanikio yake katika mauzo, idadi ya wasikilizaji yameifanya kuwa alama ya kudumu katika historia ya FIFA. 

Hata hivyo, nyimbo kama 'La Copa de la Vida', 'Wavin' Flag', 'We Are One na 'La La La' nazo zimeandika historia yake na kubaki sehemu ya kumbukumbu tamu za mashindano makubwa zaidi ya soka duniani.

Picha ya Ricky Martin aliyetamba na wimbo wa Kombe la Dunia 'La Copa de la Vida'

Kadiri Kombe la Dunia linavyoendelea kufanyika, nyimbo zake nazo zinaendelea kuwa sehemu muhimu ya utamaduni wa mashindano hayo. Zikibeba hisia za mamilioni ya mashabiki kutoka kila kona ya dunia.