Nyuma ya pazia Maria Carey kuachana na mpenzi wake
Muktasari:
- Tanaka anataka kuanzisha familia, yaani kuwa na watoto na hivyo hakuona hilo likifanikiwa akiwa na Mariah, kwa hiyo ameamua kutazama upande mwingine.
Mwimbaji maarufu duniani, Mariah Carey ameachana rasmi na mpenzi wake wa muda mrefu, Bryan Tanaka ambaye aliwahi kuwa dansa wake ikiwa ni miaka saba ya kuwa pamoja.
Tanaka alifanya kazi kama dansa na Mariah Carey kuanzia mwaka 2006 na baada ya miaka 10 ya kazi, mwaka 2016 wawili hao walianzisha uhusiano ambao sasa umefikia ukingoni.
Sababu ya kuachana kwa Mariah, 54, na Tanaka, 40, inatajwa kuwa tofauti ya umri, miaka 14 sasa, hilo limesababisha kila mmoja kuwa na kipaumbele ambacho ni tofauti na mwenzake, jambo lililowafanya kushindwa kusonga mbele.
Tetesi za wawili hao kuachana zilianza mapema 2023, pale Mariah alipofanya mahojiano na People na kusema mwaka huu ulikuwa mgumu kwake.
Mtandao wa Pagesix umenukuu chanzo kimoja kilichodai kuwa Tanaka anataka kuanzisha familia, yaani kuwa na watoto na hivyo hakuona hilo likifanikiwa akiwa na Mariah, kwa hiyo ameamua kutazama upande mwingine.
Utakumbuka tayari Mariah ana watoto wawili ambao ni pacha, Morocco na Monroe, 12, aliojaliwa na aliyekuwa mume wake, Nick Cannon ambaye walifunga ndoa mwaka 2008 na kudumu hadi mwaka 2016 walipoachana kwa talaka.
Mshindi huyo wa Grammy na Tanaka kwa mara ya mwisho walionekana pamoja katika siku yake ya kuzaliwa Mariah mnamo Machi, mwaka huu.
Hata hivyo, hii sio mara ya kwanza wawili hao kuripotiwa kuachana, waliwahi kuachana mwaka 2017 lakini wakarudiana ndani ya muda mfupi.
Ikumbukwe Mariah alipata umaarufu na albamu yake ya kwanza, Mariah (1990) iliyosimamiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Columbia Records, Tommy Mottola ambaye baadaye alimuoa. Na huyu ndiye msanii pekee mwenye nyimbo tano zilizoshika namba moja chati za Billboard Hot 100.
Albamu zake mbili, ‘Music Box’ (1993) na ‘Daydream’ (1995) zilifanya vizuri zikitoa nyimbo maarufu kama 'Dreamlover', 'Hero', 'Without You', 'Fantasy', 'Always Be My Baby', 'One Sweet Day' n.k.
Hadi sasa Mariah ameuza rekodi zaidi ya milioni 220 duniani kote na ni miongoni mwa wanamuziki waliouza sana.