Oprah Winfrey, alivyoficha siri ya Whitney Houston kuanguka jukwaani
Muktasari:
- Akizungumza katika mkutano wa Cannes Lions, Oprah alisema tukio hilo lilitokea wakati Whitney aliporejea tena kwenye kipindi hicho kwa ajili ya kuimba mbele ya watazamaji, na wakati huo tayari alikuwa amerejea katika matumizi ya dawa za kulevya baada ya hapo awali kuacha
Marekani. Mtangazaji maarufu wa televisheni Marekani, Oprah Winfrey, 72, kwa mara ya kwanza amefunguka alivyosaidia kuficha tukio la marehemu Whitney Houston kuanguka jukwaani wakati akitumbuiza kwenye kipindi cha The Oprah Winfrey Show.
Akizungumza katika mkutano wa Cannes Lions, Oprah alisema tukio hilo lilitokea wakati Whitney aliporejea tena kwenye kipindi hicho kwa ajili ya kuimba mbele ya watazamaji, na wakati huo tayari alikuwa amerejea katika matumizi ya dawa za kulevya baada ya hapo awali kuacha.
Oprah alieleza kuwa aliwahi kufanya mahojiano ya kina na Whitney wakati ambapo alikuwa ameacha kutumia dawa za kulevya, lakini hali ilikuwa tofauti kabisa alipomwalika tena katika kipindi chake kwa ajili ya kutumbuiza.
“Nafikiri hiyo ndio ilikuwa mara yake ya mwisho kuja kwetu. Na alikuwa ameanza tena kutumia dawa za kulevya. Mahojiano ya kwanza niliyofanya naye alikuwa sawa lakini siku alipokuja kwenye kipindi kuimba hakuwa katika hali ile ya mwanzo, na ndipo alianguka jukwaani.
“Nilijua kama habari hiyo ingetoka hadharani, basi Whitney angeharibikiwa sana na jambo hilo, ingawa watazamaji waliokuwapo walikuwa na kamera zao, niliwasihi wasisambaze picha hizo kwa sababu zingeharibu maisha yake,” alisema Oprah.
Hata hivyo, muda mfupi baada ya kauli hiyo ya Oprah, familia ya Whitney kupitia TMZ ilitoa ufafanuzi kuhusu ukweli wa jambo hilo.
“Whitney alianguka jukwaani lakini ilikuwa wakati wa majaribio ya sauti (sound check), na ilisababishwa na eneo hilo kuwa na giza pamoja na kutolijua vizuri jukwaa hilo. Hakuna ukweli kwamba alikuwa amelewa dawa za kulevya,” familia ilieleza.
Familia hiyo ilikiri kuwa Whitney alipitia changamoto za uraibu wa dawa za kulevya lakini si sahihi kuhusisha kila tukio au kila kipindi cha maisha yake na uraibu wake.
Whitney, mkali wa kibao cha Greatest Love of All (1986), alifariki mwaka 2012 akiwa na umri wa miaka 48 baada ya kuzama kwa bahati mbaya kwenye beseni la kuogea (jacuzzi) ndani ya hoteli. Hata hivyo, ugonjwa wa moyo na matumizi ya cocaine vilitajwa pia kama sababu zilizochangia kifo chake.
Kwa miaka mingi, watu waliamini kuwa Whitney alianza kutumia dawa za kulevya wakati wa uhusiano wake na Bobby Brown ambaye walifunga ndoa mwaka 1992. Lakini kwa mujibu wa filamu iitwayo Whitney (2018), msanii huyo alianza matumizi ya dawa hizo kabla hata ya kukutana na Bobby Brown.
Katika filamu hiyo ilifichuliwa kuwa kaka zake Whitney, Gary na Michael ambao walikuwa wakisafiri naye wakiwa kama walinzi wake ndio hasa waliomuingiza mwimbaji huyo katika matumizi ya dawa za kulevya.
Keith Kelly ambaye ni rafiki wa kaka zake Whitney, alikiri kuwa ndiye aliyempa Whitney bangi na cocaine kwa mara ya kwanza katika birthday party yake ya kutimiza miaka 16.