Sauti za Busara 2026 yagusa unyanyasaji wa kijinsia
Muktasari:
- Akizungumza leo Januari 20,2026, jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari Journey amesema Sauti ya busara ni zaidi ya muziki
Dar es Salaam. Zikiwa zimesalia wiki mbili kabla ya ufunguzi wa msimu wa 23 wa Tamasha la Sauti za Busara 2026, linalotarajiwa kufanyika Februari,5 hadi 8, Stone Town -Zanzibar. Mkurugenzi wa Tamasha hilo, Journey Ramadhan amesema wanatarajia kukutanisha zaidi ya wasanii 400.
Akizungumza leo Januari 20,2026, jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari Journey amesema Sauti ya busara ni zaidi ya muziki.
"Tunatoa elimu, uwezeshaji wengi wanajua ni muziki lakini kuna vitu vingi ambavyo tunavitengeneza kwa mustakabali wa muziki ambavyo watu waliohudhuria na wasiohudhuria wote wanapata. Kitu kipya kilichokuja ni eneo tunalotegemea kulitumia ni la wazi lakini tutaweka fensi. Ni Mnazi Mmoja. Tunategemea uwepo wa mashabiki na wengine mbalimbali.
"Program yetu ya muziki itakuwa na wasanii mbalimbali nitoe wito kwa wasanii wa ndani ni muda wa kujifunza kutoka kwa wasanii wengine hata sisi tunajifunza kupitia matamasha madogo kutakuwa na Salif Keita, Ben Pol, Man Fongo, Man Kifimbo, Alamokha na wengine. Kila siku nawaambia wasanii msijichukulie poa mnajiumiza wenyewe,"amesema Journey
Hata hivyo kwa upande wake Mkurugenzi wa Busara Promotions, Lorenz Herrmann amesema mwaka huu kumekuwa na miradi mbalimbali ikiwemo wa kuelimisha dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia.
"Taasisi ya Busara promotions lengo lake kuu ni kutengeneza majukwaa kwa wasanii wanaotengeneza muziki wa kizazi kipya ukiwa unaoneshwa live. Pia kutoa mafunzo kwa ajili ya taaluma ndani ya muziki na kuwatengenezea nafasi za ajira, pia kuandaa matamasha makubwa ya kimataifa Tanzania. Mwisho ni kubadilisha tabia kwa wanajamii kupitia burudani ya kitamaduni ikiunganishwa na ujumbe wa kuweza kubadilisha tabia.
"Miradi ya mwaka huu ambayo tunaendelea nayo na inatusaidia kama taasisi ya Busara cha kwanza ni mradi ambao tumeungana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na UN Women tunaenda kwenye jamii za Zanzibar kuelimisha kuhusu unyanyasaji wa kijinsia na njia gani za utatuzi zinapatikana kwa Zanzibar. Kupitia hilo tunafikia wananchi wa ndani (Uswazi)tunafikisha ujumbe,"amesema Lorenz
Ameongezea wameungana na UNESCO kuweza kutengeneza ujuzi kwa meneja na wasanii wa Tanzania kwa lengo la kuwawezesha kufanya kazi kwa usahihi.
"Ni mradi wa miaka miwili tutafanya mafunzo na tutakutanisha mameneja na wasanii Ulaya kwenye soko la Live music. Pia kuna sekta ya women empowerment ambao wasichana zaidi ya 179 kutoka nchi 11 wameomba kuwepo kwenye hayo mafunzo huu ni mradi mwingine ambao tunaendelea nao,"amesema
Naye mwanamuziki Ben Pol ambaye ni mmoja kati ya wasanii wanaotarajia kutumbuiza kwenye tamasha hilo amesema
"Kwa hadhi ya Tamasha la Sauti za Busara, kuwa sehemu ya main stage ya performance nawashukuru sana. Ni watu ambao nawaheshimu sana. Kwa hiyo mimi najua umuhimu wa kufanya promotion na wadau wote ambao wanafanikisha kuwa vinara wa ku-accomodate wasanii ambao wanapenda live. Tunaandaa burudani ambayo
inakuwa chachu na mabadiliko chanya katika jamii,"amesema Ben
Ikumbukwe Sauti za Busara ni tamasha la burudani linalofanyika kila mwaka. Kwa 2026 litafanyikia katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, Unguja, badala ya Ngome Kongwe kama ilivyozoeleka.