Serikali yapunguza ada kwa watengeneza maudhui mtandaoni
Muktasari:
- Akiwasilisha bajeti ya serikali itakayotumika katika mwaka 2026/2027 leo Alhamisi Juni 11, 2026 bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omari amependekeza ada ya maombi ya leseni ya huduma za maudhui mtandaoni kupunguzwa kutoka Sh50,000 hadi Sh10,000.
Dar es Salaam. Serikali imependekeza kufanya marekebisho kwenye kanuni za mawasiliano ya kielektroniki na Posta (Maudhui Mtandaoni) kwa lengo la kupunguza ada za huduma za maudhui mtandaoni zinazotumiwa zaidi na vijana.
Akiwasilisha bajeti ya serikali itakayotumika katika mwaka 2026/2027 leo Alhamisi Juni 11, 2026 bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omari amependekeza ada ya maombi ya leseni ya huduma za maudhui mtandaoni kupunguzwa kutoka Sh50,000 hadi Sh10,000.
Vilevile, ada za mwanzo (initial), za mwaka na za kuhuisha leseni ya huduma za maudhui mtandaoni kupunguzwa kutoka Sh500,000 hadi Sh50,000.
Katika hatua nyingine, serikali imependekeza kupunguza ada ya maombi ya leseni ya mtengeneza maudhui mtandaoni (Online Content Aggregator) kutoka Sh100,000 hadi Sh20,000.
Pia, ada za mwanzo (initial), za mwaka na za kuhuisha leseni ya mtengeneza maudhui mtandaoni (Online Content Aggregator) zitapunguzwa kutoka Sh1,000,000 hadi Sh100,000.
Amesema hatua hiyo inalenga kupunguza gharama za huduma za maudhui mtandaoni zinazotumiwa zaidi na vijana na kuongeza ushiriki wao katika sekta ya kidijitali.