Simulizi ya Frida kutoka kwenye Hip-Hop hadi Balozi wa Mazingira Duniani
Muktasari:
- Baada ya kutumbuiza kwenye jukwaa la kimataifa Desemba 10 na 11, nimeshuhudia matamasha yote yaliyohudhuriwa na zaidi ya watu 6,000 kutoka mataifa zaidi ya 170 duniani.
Kenya. Wiki kadhaa baada ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP) kumteuwa mkali wa Hip-Hop nchini na mwanaharakati wa mazingira, Frida Amani kuwa Balozi wa Mazingira Duniani, Mwananchi imefanya nae mahojiano.Baada ya kutumbuiza kwenye jukwaa la kimataifa Desemba 10 na 11.
Nimeshuhudia matamasha yote yaliyohudhuriwa na zaidi ya watu 6,000 kutoka mataifa zaidi ya 170 duniani.
Ni kwenye Kikao cha saba cha Baraza la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEA-7) linaloendelea katika jiji la Nairobi nchini Kenya. Hili linanipa hamasa ya kufanya mahojino na msanii huyu mara baada tu ya kushuka jukwani. Lengo ni kufahamu safari yake ya muziki kutoka Tanzania hadi kwenye jukwaa la ulimwengu.
Haya ni Mahojiano maalum kati ya Mwananachi na Frida Amani.
Mwananchi : Unafikiri umefanya yapi mpaka ukachaguliwa na UNEP kuwa balozi wa mazingira duniani?
Frida: Kwa muda mrefu nimekuwa mwana Mazingira, nimefanya project mbalimbali za Mazingira, kama “Kisiki hai” ambayo ni wimbo na pia mradi wa upandaji miti ambayo inafanyika kwa kushirikiana na LEAD Foundation, ambapo ilihusisha kupanda miti zaidi ya 24 milioni katika maeneo mbalimbali ya nchini.
Maeneo haya ni kama Monduli mkoani Arusha, Dadoma, na sehemu nyingine ambazo zilisumbuliwa na ukame kwa muda mrefu baada ya ukataji miti.
Tumeweza kutumia njia ya kuuhisha visiki, kwani unaweza kukutana na kisiki ukakichukulia kawaida kumbe kinaweza kuwa tena mti wa kawaida.
Mwananchi : Kwa nafasi yako, tunawezaje kuunganisha ubunifu na uwezo watu kuhamasisha uhifadhi, urejeshaji wa mazingira?”
Frida: Ninachokitumia mimi kikubwa ni muziki wangu. Mimi ni msanii, natengeneza muziki ili ufikie watu. Nimeandika nyimbo nyingi sana kuhusu mazingira. Mbali na “Kisikihai” ipo “nakijanisha” niliyofanya na Ben Pol, Christina Shusho na Joh Makini.
Lakini pia nimekuwa balozi wa mabinti na watu wengine kwa muda mrefu pia, hasa vijana kina mama.
Na project nyingine pia inatwa Mtoe Mama Gizani. Ambayo imefanyika sehemu mbalimbali kama Tanga. Hii imefanyika Dodoma pia.
Mradi unalenga kuweka umeme unaotokana na nishati ya jua kwenye maeneo yasiyo na umeme au umeme umefika lakini bado unasumbua. Mradi unalenga nyumba za kinamama na huduma za kujamii. Hili ni muhimu kwa sababu umeme jua ni nishati jadidifu na safi kwa mazingira.
Kwa kutumia muziki ninafanya tamasha maalumu (show) ambayo nilianza mwaka jana nchini na nje ya nchi na inakwenda na jina la “Performance for Nature” au utendaji kwa ajili ya mazingira ya asili.
Hapa nashirikiana na wasanii wengine, wadau wa mazingira na watu wengine. Kwa mwaka huu tulipanga kufanya baada ya uchaguzi mkuu kwa Tanzania lakini kama unavyofahamu yaliyotokea Septemba 29,2025 tuliahirisha. Lakini hapa nimefanya “show”.
Ndoto yangu ni kuendelea kuona wasanii wengi wakishiriki.
Mwananchi : Ilikuaje ukaanza kutambuliwa kimataifa. Hasa kwenye masuala ya mazingira, na upi wito kwa vijana wenzako?
Frida: Kutokana na haya nilianza kupata utambuzi kutoka kwa mataifa mengine duniani. Mfano mwaka 2023 nilifanikiwa kushinda Tuzo ya Wimbo Bora wa Kutunza Mazingira na kuhamisha maendeleo endelevu baada ya mradi wangu wa “Kisiki hai”. Tuzo iliitwa, “Music Cities Awards“ iloyotolewa nchini Marekani.
Hapo ilianza kunikutanishwa na watu wa Umoja wa Mataifa. Na mpaka sasa nazidi kukutana na wadau wengi na tunaendelea kushirikiana. Nilialikwa pia kufanya tamasha kwenye UNEA-6 mwaka jana.
Mwananchi: Unajiona wapi miaka mitano au kumi ijao? Changamoto na fursa.
Frida: Jambo langu kubwa ambalo natamani kulifanya sana ni kurudisha ukaribu mkubwa kati ya binadamu na nature (mazingira asili). Natamani sana pia kuungana na vijana wenzangu, watoto na makundi ya jamii yaliyo kwenye hatari zaidi ya kuathirika na athari za mazingira.
Muhimu ni kufanya uchechemuzi, kuhamasisha vijana kujihusisha na mambo ya mazingira kwamba mazingira si vitu vya watu fulani, wasomi fulani, wanasayansi fulani, bali ni jukumu kwa wote. Kwani matatizo ya mazingira yanagusa kila mtu.
Lakini pia kama unavyoniona, ninapata bahati na nafasi. Kwa mfano tuko kwenye UNEA-7, tunajua hapa dunia imekutana, wanazungumza kutafuta njia gani ambazo zitaweza kusaidia kurejesha mazingira. Nazidi kupata mawazo ya kuendelea kujumuisha na wengine.
Kwa sababu napata hizi nafasi na ninawakilisha vijana wenzangu wengi. Kufikisha vitu ambavyo wanavitamani, tunatamani kusikia vinafika mbali zaidi. Mazungumzo ambayo labda kijana akiongea mtaani yanakuwa magumu kufika kwa watu, lakini mimi naweza kufika.
Kwa sasa ninafahamiana na watu wengi sana kwenye taasisi mbalimbali ambao wanahitaji msaada wa elimu, wanahitaji msaada wa kujulikana, wanahitaji msaada pia wa ufadhuli. Na mimi niko kwenye nafasi ambayo naweza kuzungumza kwa niaba yao na tukaendelea kufanikisha malengo mengi.
Najiona mbali sana, na najiona kama mmoja wa vijana wa kutazamwa kwa kuwa nimefanya mabadiliko makubwa kwenye maeneo mbalimbali. Nitaendelea kuwa balozi wa mabinti, wa vijana na makundi maalumu. Kwa miaka ijayo, najiona nikiendelea kufanya kwa ubora mkubwa zaidi.
Lakini sijioni mimi peke yangu, nawaona pia vijana ambao wananitazama kama picha wakifanikiwa na kufika kwenye malengo haya na zaidi na ninajiona kama daraja la wao kufanikisha hili.
Mwananchi: Je, unashirikiana vipi na serikali ya Tanzania na unaona fursa gani zaidi kuboresha ushirikiano huo?
Frida: Tumekuwa tukifanya kazi na serikali. Tunashirikiana kwa pamoja vizuri sana. Mfano, tamasha langu la “Performance for Nature” mwaka huu ilikuwa tunafanya kwa pamoja na Ofisi ya Makamu wa Rais -Mazingira. Tumeshirikiana kwa ajili ya kufanikisha hilo. Japo haikufanyika ila bado tunaendelea kujadili.
Na hata nilipopata nafasi hii ya kuwa balozi, kwa kuwa tunafanya kazi kwa karibu na ofisi ya makamo wa Rais na viongozi wengine tuliwapa taarifa na wametupongeza. Pia tulipanga kukutana baada ya hili.
Tanzania ni moja ya sehemu ambazo tuko urejeshaji wa ikolojia inahitajika kwa nguvu na kwa haraka sana. Kwa hiyo tukikutana kwa pamoja kuna mawazo ambayo naamini tutashirikiana kutokana na ndoto na malengo tuliyo nayo.
Kwa mfano Mpango wa miaka kumi wa Umoja wa Mataifa wa Urejeshaji wa Mazingira (2021–2030) “The UN Decade on Ecosystem Restoration” unaolenga kuhamasisha dunia kurejesha misitu, ardhi iliyoharibika, mito, maziwa na bahari.
Kwenye hili kuna nafasi kubwa ya kushirikiana na serikali kwa malengo ya nchi ni kurejesha angalau hekta milioni tano hadi 2030 na hadi sasa tumefika hekta 2.5 milioni.
Nategemea kushirikiana nao kwa ukubwa, japokuwa bado siishii mipaka ya Tanzania, kwa sababu nimetambulishwa duniani. Kwa hiyo itanibidi nifanye kazi na mataifa yote kwa ujumla.