Prime
Simulizi za muziki: Wanamuziki wamenza zamani kudai sheria ya hakimiliki
Katika aya ya mwisho ya makala ya wiki iliyopita niliandika kuwa kuanza kutumika kwa kanuni ya stika za TRA za mwaka 2013, ikawa ndio kengele ya kufunga maduka halali ya kanda za muziki, CD na DVD. Lakini kabla ya kueleza sababu ambazo zilifikisha hali hiyo, turudi kwenye historia fupi ya kanuni hiyo.
Makala ya leo itaendeleza mfululizo wa makala ambazo nimekuwa naziandika kuhusu swala la Hakimiliki nchini mwetu, ntangulize shukrani kwa walionipigia simu kupata ufafanuzi wa mambo niliyoandika na hata kuendelea kunipa taarifa za ziada ambazo zitakuwemo katika muendelezo wa makala hizi.
Katika aya ya mwisho ya makala ya wiki iliyopita niliandika kuwa kuanza kutumika kwa kanuni ya stika za TRA za mwaka 2013, ikawa ndio kengele ya kufunga maduka halali ya kanda za muziki, CD na DVD. Lakini kabla ya kueleza sababu ambazo zilifikisha hali hiyo, turudi kwenye historia fupi ya kanuni hiyo.
Nilianza kuisikia kuhusu matayarisho ya kanuni hiyo baada ya kutaarifiwa na afisa mmoja wa mamlaka ya kodi ambaye alijitambulisha kuwa amepewa kazi ya kutengeneza kanuni hiyo. Baada ya muda mfupi tulipata taarifa kuwa Ikulu imetoa fedha kwa ajili ya mtaalamu kufanyia utafiti wa kusaidia sheria hiyo ifanye kazi.
Taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari tarehe 4 Februari 2013, iliongeza uzito wa habari hiyo kwani taarifa hiyo ilieleza jinsi Diamond Platnumz alivyotoa shukrani zake kwa Rais Kikwete walipokutana Kigoma ambapo rais alikuwa mgeni rasmi wa sherehe za za miaka 36 ya kuzaliwa kwa CCM.
Sehemu ya taarifa hiyo ilisema, ‘Shukrani kubwa za Diamond zilihusu hatua ya Rais Kikwete kumlipa mtaalamu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliyefanya utafiti wa namna ya kuwasaidia wasanii, hatua iliyopelekea Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA) kuanzisha mfumo wa kusaidia kuthibiti kazi za wasanii mwaka huu.
Mtaalamu huyo alilipwa Sh 20 Milioni kwa kazi hiyo’ Pamoja na kuweko nia nzuri sana ya jambo hilo kwa ambao tulikuwa tumehudhuria mikutano mbalimbali toka miaka ya 90, ilikuwa inaeleweka wazi kuwa stika za kodi si njia sahihi ya kusaidia kupatikana haki kwa wanamuziki na hata kupatikana kodi kwa serikali.
Kwanza Mamlaka ya Kodi si chombo cha kujua Hakimiliki ya muziki ni ya nani, na pili kwa kuwa kazi yake ya kwanza ni kukusanya mapato, hiyo ndio itakuwa kipaumbele wakati wa kuuza stika za kodi. Hatukusita kutoa taarifa hiyo kwa wahusika na hata baadhi ya wabunge tuliwapa taarifa hiyo mapema na kuwaeleza kuwa kwanza tayari kulikuwa na kanuni ya Cosota kuhusu hilo ila tu imekosa fedha za kuanza kufanya kazi hiyo. Bahati mbaya shughuli ilienda kama ilivyopangwa na hatimaye sheria ikapitishwa.
Jitihada za kupata nakala ya ‘Utafiti toka Chuo Kikuu’ mpaka leo hazijafanikiwa wala hata jina la mtafiti halijulikani.
Kanuni za sheria hiyo mpya zilitaka mfanyabiashara wa kazi za muziki kuwa na stika kwa kila album iliyopo dukani. Kwa sheria kila album ilitakiwa kuwa na mkataba wake na stika zilizotakiwa kununuliwa kwa kila album zilitakiwa kuwa 5000. Maduka ya wasambazaji walikuwa na maelfu ya album tofauti tofauti, hivyo basi wangetakiwa kununua mamilioni ya stika ili maduka yao yawe yanauza kazi halali kisheria. Na kulikuwa na kazi nyingine kubwa ilifuatia, sheria ilikuwa ikieleza lazima ripoti itolewe kila mwezi kuhusu stika hizo. Haichukui akili kubwa kuona kwanini biashara hiyo ililazimika kufa.
Mwaka 2007 wakati Cosota ikijitayarisha kutumia stika za Hakigramu, tayari ilikuwa ilikuwa imependekeza kuwa shughuli ifanyike kwa ubia na TRA, katika mfumo uliopendekezwa TRA ingepata taarifa ya biashara kutokana na mauzo ya stika na hiyo kuweza kukadiria na kukusanya mapato stahiki, huku wanamuziki wakipata mgao wao stahiki kutoka Cosota, kama inavyofanyika mahala pengine ulimwenguni.
Wakati huohuo wanamuziki wakaanza kufuatilia kanuni inayovitaka vyombo vya utangazaji kulipia mirabaha kwa kazi zinazotumiwa na vyombo hivyo.
Kihistoria awali kulikuwa na chombo kimoja tu cha utangazaji ambacho kilikuwa mali ya serikali na ni katika zama za chombo hiki ambapo ulipwaji wa mirabaha ulisitishwa kama nilivyoeleza katika makala ya awali. Usitishwaji huu wa kulipa mirabaha haukutokea nchini mwetu tu bali nchi nyingi za Afrika mara tu baada ya kupata Uhuru na kutaifisha vituo vya redio, na ulipaji mirabaha ukasimama.
Nchi nyingi zilibadili sheria ya Hakimiliki kama ilivyokuwa kwetu mwaka 1966, na sheria mpya ilisitisha ulipaji wa mirabaha. Baadhi ya watafiti wa sheria za hakimiliki Afrika, husema kuwa nia ya sheria mpya ya Hakimiliki haikuwa imelenga muziki, bali ililenga biashara ya vitabu. Kama ilivyo kwenye muziki vitabu vinapotumika kwa shughuli zaidi ya kuuza hulazimika kulipiwa mirabaha. Kwa mfano kitabu kikipitishwa kutumika katika shule basi hapo mtunzi huweza kufaidi kiasi kikubwa cha fedha kutokana na mirabaha. Sasa kwa kuwa nchi za Kiafrika zilikuwa ndio zimepata Uhuru na zilikuwa na nia ya kuelimisha watu watu wake, hivyo kupunguza deni la elimu ikalazimu kutunga sheria zilizoruhusu kutokulipa mirabaha.
Sheria ya Hakimiliki ya no 61 ya mwaka 1966, ilidumu mpaka mwaka 1999. Hiyo ni miaka 33 ya utamaduni wa vyombo vya utangazaji kutokulipa mirabaha, na hakika vyombo binafsi viliporuhusiwa nchini, viliendeleza utamaduni huo, japokuwa sheria ilivitaka kulipia mirabaha, na hasa baada ya kuona hata kituo kikuu cha utangazaji cha serikali kinakiuka sheria ya kulipa mirabaha.
Wanamuziki hawakukaa kimya ila mengi yalijitokeza tutakutana wiki ijayo, ujue yaliyojiri.