Tabata ilivyogeuka chimbo la kuponda raha
Muktasari:
- Wimbo huo ulitoka miaka mitatu iliyopita. Hama kwa hakika alichokiimba makabila kwa asilimia kubwa kinapatikana Tabata. Moja ya eneo la jiji la Dar es Salaam lenye vibe muda wote.
Dar es Salaam. “Tabata, Tabata hamning’oi,
Tabata, bila Tabata sitoboi,” x2
“Dulla naweza nikaishi Mbezi au nikaishi Magomeni
Naweza nikapanga ghorofa Sinza au kwa Wema Sepetu Mbweni, ila wanangu Tabata, Tabata hamning’oi,”
“Kwingine nitaendelea kutembea ila kwa kuishi sitoboi
Kwanza ukija Tabata muda wote tuko bize vibe kila sehemu
“Na huku kwetu hakuna wivu demu wako ndiyo anakutafutia demu, Makabila nikihama Tabata nahamia Tabata
Yaani nikihama Bima njoo Kinyerezi utanikuta,”ameimba Dulla Makabila
Hiyo ni baadhi ya mistari inayopatikana kwenye wimbo uitwao Tabata wa mwanamuziki wa singeli Dulla Makabila .
Wimbo huo ulitoka miaka mitatu iliyopita. Hama kwa hakika alichokiimba makabila kwa asilimia kubwa kinapatikana Tabata. Moja ya eneo la jiji la Dar es Salaam lenye vibe muda wote.
Tabata haichagui, haina mwanzo wa wiki wala mwisho wa wiki. Huko siyo ajabu kukuta Jumatatu watu wakijirusha ‘Boss Monday’ kwa Jesca Kikumbi yaani Kitambaa Cheupe.
Kama mgeni unaweza kujiuliza ni muda gani watu hao wanafanya kazi. Kwani ni bata juu ya bata ni vaibu tu mtu wangu.
Wenyewe wanasema ni starehe na bata la kufa Mbwa. Kila chochoro kumbi za starehe zilizopambwa wa mikito ya muziki wa kila aina humo ndani sasa watu wako nyomi. Wenye juice kama wagonjwa, mitungu, maji yaani ni miksa bata la Tataba halichagui mtu.
Licha ya kuwa maeneo kama Sinza na Kinondoni ndiyo yalitamba, kuwa na sehemu nyingi za watu kuponda raha. Lakini sasa kijiti hichi kimeshikwa na Tabata.
Watu kutoka kona mbalimbali za jiji la Chalamila hukutana Tabata kumwagilia moyo. Tabata unapata kitu roho inapenda.
Kuna viwanja maarufu kama Mikasa, Small planet, Kitambaa Cheupe, New Highbury, London Lounge, Caliphonia, Last Call Lounge pale Kimanga, Kwetu Pazuri Segerea, The Great Park na Ale Bush Pub. Haya ni baadhi tu ya maeneo ambayo watu kutoka maeneo mbalimbali hufika.
Mapochopocho kama nyama choma, ndizi choma, michemsho, makange, nyama pori na marostirosti pamoja na vinywaji vya kila aina ikiambatana na bendi za muziki wa dansi, klabu za disko zote zipo Tabata. Hayo yote ni kutokana na ukweli kwamba, vijana wengi na wapenzi wa burudani wamehamia huko.
Hata hivyo hilo haliishii kwenye bata tu. Hata bendi mbalimbali hudondoshwa Tabata kwa ajili ya kutoa burudani. Wasanii nao baadhi wametoka kuishi Sinza wamehamia Tataba.
Kwa kifupi biashara zinazohusisha burudani ni rahisi kutoboa Tabata kama ilivyokuwa Sinza hapo awali.
Licha ya eneo hilo kwa sasa kuwa la kuponda raha. Zipo simulizi mbalimbali zinazoeleza kuwa, awali eneo hilo lilikuwa la mashamba. Kwa sababu hiyo inadaiwa ndio jina Tabata likazaliwa
Chimbuko la jina la Tabata
Kwa mujibu wa wenyeji wakongwe wa Tabata, wanadai jina hilo limetokana na neno la Kinyamwezi ‘matabata’, likimaanisha mashamba au maeneo yaliyokuwa yakilimwa.
Inaelezwa kuwa kabla ya kupanuka kwa Jiji la Dar es Salaam, Tabata ilikuwa eneo la vijiji na mashamba makubwa yaliyotumiwa kwa shughuli za kilimo.
Kadiri makazi yalivyoongezeka na mji ukapanuka, jina hilo lilibaki kutambulisha eneo hilo hadi likawa jina rasmi la kata na vitongoji vinavyounda Tabata ya leo.
Pia zipo simulizi nyingine zinazodai kuwa jina Tabata lilitokana na jina la familia iliyokuwa miongoni mwa wakazi wa kwanza wa eneo hilo. Hata hivyo, simulizi hizo hazijapata uthibitisho wa kutosha katika nyaraka za kihistoria.
Mmoja kati ya wenyeji katika eneo la Tabata Mawenzi Mzee Mussa Sumai anasema ni zaidi ya miaka 30 sasa tangu aishi eneo hilo. Anasema alipata kiwanja katika eneo la hilo kukiwa na mapori tofauti na ilivyo sasa.
“Nilipata kiwanja zamani sana enzi hizo kulikuwa na mashamba kila kona. Hakukuwa kama hivi unavyoona sasa. Nakumbuka usiku kulikuwa kunasikika sauti za fisi tu.
“Palikuwa panatisha sana yaani kiza kila sehemu. Sio sasahivi umeme upo, watu wanaweza kutembea usiku. Kipindi hicho ni mashamba na mapori tu sikuwahi kufikiria kama kuna siku panaweza kuwa pamechangamka kiasi hiki,” anasema.
Anaendelea kwa kusema licha ya kuwa awali kulikuwa na mashamba. Lakini kwa sasa ndilo eneo linalompatia fedha za kuendesha maisha ya familia yake, kwani sehemu zile zilizokuwa pori zamani ndizo amejenga fremu ambazo watu wamepangisha. Huku sehemu moja ikiwepo bar kubwa na maarufu Tabata ambayo mtu kapanga na kuwekeza.
Zamani machimbo yalikuwa haya
Hapo awali zilikuwepo kumbi nyingine kama Lang’ata (FM Club) na baadaye kuitwa Club Aset huko bendi mbalimbali zilikiwasha na vijana wote wa zamani walikuwa wanakutana hapo kufanya yao.
Pia, kulikuwa na kumbi kama Vijana Social hall, Ukumbi wa Safari Resort wa Kimara, Muleba Bar Mabibo, ukumbi wa Hotel 92 na hata Motel Jasmina wa Kijitonyama.
Bila kusahau Mango Garden, Msasani Club, Gogo Hotel, Msasani Bay Villa, Tiger Motel, Bahari Beach Hotel, DDC Magomeni Kondoa, DDC Mlimani Social, Lango la Jiji, Friends Corner Hotel na Texas zote zimepoteza mvuto kabisa.
Ilala kulikuwa na kumbi maarufu kama Amana Club, Max Bar, Y2k, Afri Center, Mbowe, Ushirika, na DDC Kariakoo wakati Temeke kulikuwa na Imasco, Harbours Club, Highway Park za Kurasini, Omax Keko, Wapiwapi Chang’ombe, Temeke Stereo, Sugar Ray, Kisuma baa na DDC Keko ambazo zilikuwa zinatamba kwelikweli.