Tyla avunja ukimya kuhusu tetesi za kujiunga Roc Nation
Muktasari:
- Tetesi hizo zilianza kushika kasi baada ya tangazo lililowekwa katika eneo la Times Square, New York, likimkaribisha Tyla kujiunga na Roc Nation. Hatua hiyo iliwafanya mashabiki wengi kuamini kuwa msanii huyo alikuwa tayari amesaini rasmi na kampuni hiyo.
Mwanamuziki anayefanya vizuri katika soko la kimataifa, Tyla, amekanusha uvumi uliokuwa ukisambaa kwa siku kadhaa ukidai kuwa amesaini mkataba wa mamilioni ya dola na kampuni ya Roc Nation inayomilikiwa na rapa maarufu Jay-Z.
Tetesi hizo zilianza kushika kasi baada ya tangazo lililowekwa katika eneo la Times Square, New York, likimkaribisha Tyla kujiunga na Roc Nation. Hatua hiyo iliwafanya mashabiki wengi kuamini kuwa msanii huyo alikuwa tayari amesaini rasmi na kampuni hiyo.
Hata hivyo, Tyla aliweka wazi ukweli huo kupitia ukurasa wake wa Instagram, ambapo aliandika: "Sijasaini Roc Nation." Wakati huohuo, aliwahamasisha mashabiki wake kusubiri albamu yake ya pili iitwayo APOP, inayotarajiwa kuachiwa Julai 24 mwaka huu.
Kwa sasa, Tyla bado yuko chini ya lebo ya FAX Records, huku kazi zake zikisambazwa kupitia makubaliano ya kipekee ya leseni na Epic Records, ambayo ni tawi la Sony Music Entertainment.
Epic Records ni miongoni mwa lebo kubwa za muziki duniani, ikiwa inasimamia wasanii wenye majina makubwa kama Travis Scott, Future, 21 Savage, Camila Cabello, Mariah the Scientist, DDG na GIVEON. Hali hiyo inamfanya Tyla kuwa mmoja wa wasanii wa Afrika wenye nafasi kubwa ndani ya lebo hiyo.
Mbali na mkataba wake wa muziki, Tyla pia anasimamiwa na Africa Creative Agency na ni sehemu ya ushirikiano wa usimamizi wa kimataifa unaohusisha HYBE, kampuni kubwa ya burudani kutoka Korea Kusini inayosimamia kundi maarufu la K-pop, BTS.
Roc Nation, iliyoanzishwa mwaka 2008 na Jay-Z, imekuwa moja ya kampuni zenye ushawishi mkubwa katika sekta ya burudani duniani. Mbali na usimamizi wa wasanii, kampuni hiyo hutoa huduma za uchapishaji wa muziki, maandalizi ya ziara za muziki, usimamizi wa wanamichezo na ushirikiano wa kibiashara na chapa mbalimbali.
Katika miaka yake ya uendeshaji, Roc Nation imefanya kazi na mastaa kama Rihanna, Megan Thee Stallion, Alicia Keys, A$AP Rocky, J. Cole, DJ Khaled na Christina Aguilera, pamoja na kushirikiana na baadhi ya wasanii wa Afrika kupitia mikataba ya usimamizi.
Licha ya tetesi hizo kuzua mjadala mkubwa mitandaoni, Tyla amesisitiza kuwa kwa sasa hana mpango wa kuhamia Roc Nation. Badala yake, anaendelea kujikita katika maandalizi ya uzinduzi wa albamu yake mpya, APOP, huku akiendeleza mafanikio yake katika soko la muziki la kimataifa akiwa na timu yake ya sasa.