Upekee wa Zari kwa Diamond Platinumz
Muktasari:
- Kwa miaka kadhaa sasa mashabiki wengi wamekuwa wakisifu jinsi walivyoweza kuweka kando tofauti zao binafsi kwa ajili ya malezi bora ya watoto, kitu ambacho mastaa wengi kimewashinda.
Dar es Salaam. Licha ya kutengana, Zari The Bosslady na Diamond Platnumz wameendelea kudumisha uhusiano mzuri kwa ajili ya watoto wao na mara kadhaa wameonekana wakishirikiana katika shughuli za kifamilia, jambo linaloonyesha ukomavu na heshima.
Kwa miaka kadhaa sasa mashabiki wengi wamekuwa wakisifu jinsi walivyoweza kuweka kando tofauti zao binafsi kwa ajili ya malezi bora ya watoto, kitu ambacho mastaa wengi kimewashinda.
Kabla ya Zari, tayari Diamond alishawahi kuwa na uhusiano na wanawake wengi tena maarufu kutoka katika tasnia ya burudani lakini Zari ndiye wa kwanza kumzalia mtoto.
Hili limemfanya Zari kuwa na upekee zaidi hasa pale anapotazamwa na Bi. Sandra maarufu kama Mama Dangote. Ni Zari aliyemletea mjukuu wake wa kwanza kutoka kwa Diamond.
Kingine ni Diamond ana mtoto mmoja pekee wa kike, Tiffah ambaye mama yake ni Zari. Watoto aliozaa na Hamisa Mobetto na Tanasha Donna kutokea Kenya, wote ni wa kiume.
Hili limemjengea upekee Zari kwenye famili hiyo, pia limemfanya Tiffah kuwa mtoto maarufu zaidi wa Diamond akifuatiliwa na watu zaidi ya milioni 4.6 kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram.
Kwa Diamond, Zari ndiye baby mama mwenye uwezo mkubwa zaidi wa kiuchumi - akimiliki miradi mikubwa ya biashara, vyuo, magari na nyumba za kifahari Afrika Kusini.
Ingawa anajimudu, bado ana busara zake kichwani ndiyo sababu tunasema Zari ni mmoja tu kwa Diamond, mwanamuziki wa Bongo Fleva na mwanzilishi wa WCB Wasafi.
Pindi walipoachana baada ya mfululizo wa visa vilivyotajwa na visivyotajwa, waliishia kutupiana vijembe wao kwa wao mtandaoni bila kuhusisha familia kwa jumla, hili limemtofautisha Zari na wengine.
Apili 2020, Tanasha akiongea na Jarida la True Love huko Kenya, alimshambulia vikali Mama Dangote kwa madai kuwa alikuwa anaingilia uhusiano wao, huku Diamond akishindwa kumwambia kuwa amevuka mipaka.
"Kumheshimu mama mkwe au mama wa mpenzi wako ni jambo linalostahili kabisa lakini wakati mwingine huyo mama anaweza kuvuka mipaka na kuanza kuendesha uhusiano wenu," amesema Tanasha na kuongeza jambo hilo lilimshinda kwa sababu yeye sio mtu kuendeshwa.
Ila Zari hakuwahi kufanya hivyo na ndiyo sababu imekuwa rahisi kurejea Bongo mara kwa mara na kupata mapokezi makubwa kwenye familia ya mwimbaji huyo ambayo mara nyingi huwa na drama za hapa na pale.
Uhusiano wa Zari na Diamond utakumbukwa kwa mengi, mathalani Mei 31, 2018, Diamond aliachia wimbo wake 'Iyena', katika video ya wimbo huo aliomshirikisha Rayvanny, alitokea Zari.
Zari na Diamond alicheza kama wapendanao waliofunga ndoa. Walionekana kama maharusi wa kweli kabisa. Kama ni mara yako ya kwanza kuwaona na hujui chochote kuhusu wao, unaweza kudhani ni kweli.
Hata hivyo, wakati video hiyo inatoka haikuwa na msisimko mkubwa kwani tayari walikuwa wameshaachana, huku Zari akisusia kabisa upande wa promosheni wa video hiyo mtandaoni kama siyo yeye aliyetokekea kwenye kichupa hicho.
Ikumbukwe uhusiano wao ulidumu kwa takribani miaka minne na kujaliwa kupata watoto wawili, Tiffah (2015) na Nillan (2016) ambao wanaishi Afrika Kusini na Mama yao pamoja na kaka zao watatu.
Sio katika familia ya Diamond tu Zari anakubalika, bali hata katika baadhi ya makampuni Bongo kwani yameendelea kumpa dili za ubalozi kutokana na nguvu yake ya ushawishi hasa mtandaoni.
Ni mara nyingi tu tumeshuhudia Zari akitoka Afrika Kusini na kuja Bongo kusaini dili. Hilo lilifanya baadhi ya mashabiki kuwataka wanaotoa dili hizo kuwa wazalendo kwa kuwatazama na mastaa wa ndani pia.
Hata hivyo, staa wa filamu Bongo, Shamsa Ford alikuwa na mtazamo tofauti akieleza hakuna mfanyabiashara atayekubali kumchukua staa wa Bongo kisa uzalendo tu halafu apate hasara baadaye.
Aliongeza kuwa baadhi ya mastaa wengi wa Bongo wanajulikana kwa mambo ambayo si mazuri kitu ambacho si kizuri kwa chapa za kibiashara ambazo zinapambana kulinda soko lao na kusaka wateja wapya.
"Maana kama jamii inakudharau hata hiyo bidhaa unayoibeba itadharaulika. Kikubwa tujifunze, suala sio kujulikana ila suala ni kuwa unajulikana vipi?, watu wanakutambua kwa lipi," amesema na kuongeza.
"Ni vizuri tumeumia sasa tujipange na kufukia mashimo yaliyotoboka ili na sisi tueshimike na kuthaminika,” amesema Shamsa Ford.
Ikumbukwe Zari kutokea Uganda ndiye mwanamke mwenye wafuasi wengi zaidi Instagram ukanda wa Afrika Mashariki akiwa nao milioni 12.6, huku akifuatiwa na Hamisa na Wema, Miss Tanzania 2006.