Madiwani wahoji ujenzi hospitali ya wilaya kukwama
Muktasari:
Madiwani wa halmashauri Mtama mkoani Lindi wamekerwa na kitendo cha Sh500 milioni kutotosha katika ujenzi wa wodi tatu za hospitali ya wilaya
Lindi. Madiwani wa halmashauri Mtama mkoani Lindi wamekerwa na kitendo cha Sh500 milioni kutotosha katika ujenzi wa wodi tatu za hospitali ya wilaya.
Kutotosha kwa fedha hizo kumeelezwa na mhandisi idara ya ujenzi, Abruhan Juma kutoa taarifa ya kuchelewa kukamilika kwa ujenzi wa wodi ya uzazi, wanaume na wanawake kwamba umekwama kwa sababu kiasi hicho cha fedha kuisha na kuhitajika nyingine Sh198 milioni.
"Mradi umesimama baada ya ongezeko la mahitaji ya vifaa ikiwemo mbao na silingi bodi," amesema Juma.
Akizungumza kwa niaba ya madiwani, diwani wa Nahukahuka, Hamza Nguachi amesema wanatambua Serikali imepeleka Sh500 milioni lakini cha kushangaza hazikutosha," fedha hizi zimepelekwa kila wilaya kwa maelekezo lakini kwingine zmemaliza ujenzi ila Mtama zimeshindwa kukamilisha ujenzi na kunahitajika nyingine kama Sh200 milioni," amesema Nguachi
Diwani mwingine, Hawa Nameta amesema uadilifu kwa watendaji umekuwa mdogo kwani wamekuwa wakijali maslahi yao binafsi kuliko halmashaur hali ambayo isipo zibitiwa itaendelea kudidimiza maendeleo ya halmashauri.
"Siku mmoja nilitamani kulia nliipoambiwa kuna vifaa vya ujenzi vinatakiwa kununuliwa nje ya halmashauri ya Mtama wakati vinapatikana kila mahali hapa tena kwa bei ya kupatana," amesema Nameta
Rashidi Mega, mwenyekiti wa kijiji cha Kiwalala amesema kitendo cha madiwani kuhoji na kutokubaliana kuongeza fedha za kumalizia mradi wa ujenzi wa wodi tatu ni sahihi kwani miradi ya Serikali inaletwa kwa bajeti na maelekezo.
"Kwanza niwapongeze madiwani wangu kwa kuwa na msimamo wa namna hiyo wakiendelea na tabia hiyo watarudisha uaminifu, uwajibikaji na uadilifu kwa watendaji," amesema Mega.
Mkurungezi mtendaji wa halmashauri hiyo, George Mbilinyi amesema wana changamoto nyingi ikiwemo matumizi ya fedha bila kufuata utaratibu, miradi kutokamilika kwa wakati.
"Ndugu zangu hii halmashauri inakosa usimamizi kila mtumishi alikuwa anafanya kazi kivyake na kimazoea kulikuwa hakuna wa kusimamia hayo, nimewaomba madiwani kunipa muda kurudisha nidhamu kazi, uadilifu na mahusiano," amesema Mbilinyi.