Benki ya I&M yatangaza kupata faida miezi sita 2021

Benki ya I&M yatangaza kupata faida miezi sita 2021

Nairobi, Kenya. Benki ya I&M Group imetangaza ongezeko la faida kwa asilimia 33 baada ya kodi katika hesabu zake za nusu mwaka za 2021 kutoka Ksh3.2 bilioni (Sh6.4 bilioni) hadi Ksh4.2 bilioni (Sh8.4 bilioni).

Mali za benki hiyo ziliongezeka kwa asilimia 12 na kufika Ksh382.6 bilioni kutoka Ksh340.6 bilioni katika kipindi hicho ikichangiwa na upanuzi wa biashara zake nchini Uganda na kuongezeka kwa mikopo iliyotolewa.

Mapato halisi ya riba yalikua kwa asilimia 28 hadi Ksh8.9 bilioni kutoka Ksh6.9 bilioni za Juni 2020 ikichangiwa na ongezeko la mapato ya dhamana za Serikali.

Amana za wateja zilikua kwa asilimia 10 kutoka Ksh252.5 bilioni Juni 2020 hadi Ksh 276.8 bilioni mwaka huu.

Akizungumzia taarifa hizo za fedha, Mwenyekiti wa I&M Group, Daniel Ndonye alisema utoaji mikopo ni muhimu kwa ukuaji wa benki hasa kipindi hiki ambacho dunia inapambana na janga la Uviko-19.

Utoshelevu wa mtaji ulikuwa asilimia 21 kiwango sawa na mwaka uliopita wakati uwiano wa ukwasi ulikuwa asilimia 48 juu ya mapendekezo ya kisheria cha asilimia 20.

Katika kipindi hicho, I&M ilikamilisha ununuzi wa asilimia 90 ya hisa za Benki ya OBL ya nchini Uganda ikiwa ni sehemu ya mkakati wa upanuzi wake kikanda ili kukidhi mahitaji ya wateja wake.

“Tutaendelea kuwajali wateja wetu kwa kuwapa bidhaa zenye ubunifu zinazokidhi mahitaji na matarajio yao,” amesema.

Katika kipindi hicho, benki hiyo ilizindua kampuni tanzu inayojihusisha na usimamizi wa mali ijulikanayo kama I&M Capital Limited ambayo inatarajiwa kuongeza mapato kupitia huduma zake za kuwezesha uwekezaji, usimamizi wa mali, mapato ya kustaafu na mipango ya fedha.

Kampuni tanzu za Rwanda na Tanzania zilizindua Whatsapp Banking, huduma inayowawezesha wateja wake kuwasiliana na wahudumu kupitia mtandao huo wa kijamii muda wowote hivyo kuwaongezea uhuru wa kupata wanachokitaka.