Dk Mohammed Shein asihi CRDB kuwekeza zaidi Zanzibar

Friday February 14 2020
shein pic

Zanzibar. Rais  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza haja kwa Benki ya CRDB kuendelea kutoa huduma zake kwa pande zote mbili za  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili wananchi  wafaidike na matunda ya benki hiyo.
Dk. Shein aliyasema hayo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na mkurugenzi mtendaji mpya wa benki ya CRDB Abdulmajid Mussa Nsekela aliyefika Ikulu kwa ajili ya kujitambulisha akiwa na uongozi wa benki hiyo ulioongozwa na mwenyekitiwa bodi ya wakurugenzi Ally Hussein Laay.
Katika maelezo yake Rais Dk. Shein aliipongeza Benki hiyo kwa kuendelea kutoa huduma zake hapa Zanzibar sambamba na mikakati na malengo yake iliyoyaweka katika kutoa huduma kwa wananchi pamoja na kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Dk. Shein alisisitiza haja kwa Benki hiyo kuongeza matawi yake Zanzibar pamoja na kuipongeza azma yake ya kushirikiana na Serikali katika kuendeleza na kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo.
Pia, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuupongeza uongozi wa Benki hiyo kwa mipango waliyoipanga ya kuhakikisha Benki hiyo inaleta tija kwa nchi na wananchi wake huku akieleza matarajio yake makubwa katika uongozi wa Mkurugenzi huyo mpya wa Benki hiyo ya CRDB.
Alisisitiza kuwa iwapo Benki hiyo itaendelea  kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi Benki nyengine hapa nchini zitaweza kupanua wigo kutoka Benki hiyo hatua ambayo itapelekea kufuatwa ile dhana ya uzalendo kwani wananchi, makampuni na hata Serikali wataitumia benki hiyo ikiwemo kukopa fedha badala ya kwenda kukopa kwenye benki za nje ya nchi.
Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa Benki ni taasisi ya kiuchumi, hivyo, kuongezeka kwa benki hapa Zanzibar ambapo hivi sasa zipo Benki 13 kutaendelea kuongeza ushindani wa kibiashara sambamba na kukuza uchumi wa Zanzibar ambao umekuwa ukiimarika kila uchao.
Katika maelezo yake Rais Dk. Shein alieleza uzoefu alionao wa Benki hiyo kutokana na shughuli zake inazozifanya kwa muda mrefu hapa nchini ikiwa ni pamoja na kuunga mkono sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo kilimo, afya, viwanda, biashara, miundombinu ya barabara, wajasiriamali na mambo mengineyo.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein aliuhakikishia uongozi wa Benki hiyo ya CRDB kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Benki hiyo.
Nae Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Benki ya CRDB Abdulmajid Mussa Nsekela alimueleza Rais Dk. Shein kuwa atahakikisha anatekeleza vyema majukumu yake ili benki hiyo iendelee kupata mafanikio zaidi.
Alieleza jinsi Benki hiyo inavyofanya kazi zake hapa Zanzibar pamoja na Tanzania Bara na kueleza azma ya Benki ya CRDB ya kuunga mkono miradi mbali mbali ya maendeleo Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Aliongeza kuwa Benki hiyo inayomilikiwa na Serikali imekuwa ikipata mafanikio makubwa katika utoaji wake wa huduma hali ambayo ilitokana na hatua iliyochukuliwa ya kwenda kwa wananchi.
Alieleza kuwa kwa upande wa Zanzibar Benki hiyo ina matawi mawili ambapo tawi moja liko Unguja na jengine liko Pemba na ina wafanyakazi 42 Zanzibar na wateja wapatao 30,062 ikiwa na Mawakala kwa ujumla 145 (128 kwa Unguja na 17 Pemba) sambamba na kutoa huduma za kifedha katika uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume.
Pamoja na hayo, Mkurugenzi huyo alieleza azma ya Benki hiyo ya kufungua tawi lake jipya Zanzibar huku akionesha maeneo ambayo Benki yake imedhamiria kushirikiana na Zanzibar yakiwemo miundombinu, kilimo, utalii na ukusanyaji mapato. 
Mkurugenzi huyo pia, alitumia fursa hiyo kumueleza Rais Dk. Shein jinsi Benki ya CRDB ilivyodhamiria kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika miradi ya kimkakati kwa lengo la kuendelea kuimarisha uchumi wa Zanzibar.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Ally Hussein Laay kwa upande wake alisema kuwa Benki hiyo inayofuata misingi ya Utawala Bora imekuwa na mikakati na Sera madhubuti katika kuhakikisha inabadilishana madaraka huku akieleza namna Benki hiyo inavyochangia uchumi wa Tanzania.

Advertisement