EACLC, Yiwu kurahisisha biashara na China
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Aristides Mbwasi akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa ushirikiano mpya kati ya EACLC na Yiwu.
Muktasari:
- Hatua hiyo ni baada ya makubaliano ya EACLC na Yiwu, Yiwu ni miongoni mwa masoko makubwa zaidi ya bidhaa za jumla duniani, likiwa na zaidi ya maduka 75,000 yanayouza bidhaa za aina mbalimbali, zikiwemo vifaa vya nyumbani, nguo na viatu, vifaa vya umeme, vito na mapambo, pamoja na bidhaa nyingine ambapo sasa watakuwa wanaagiza na kuletewa.
Dar es Salaam. Wafanyabiashara wa Tanzania na mataifa mengine ya Afrika wanatarajiwa kunufaika na urahisi wa kuagiza bidhaa kutoka China baada ya Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki (EACLC) kuingia makubaliano ya ushirikiano na Soko la Yiwu (Yiwu International Trade City), moja ya masoko makubwa zaidi ya bidhaa za jumla duniani.
Kupitia ushirikiano huo, wafanyabiashara hawatalazimika tena kusafiri mara kwa mara kwenda China kutafuta bidhaa. Badala yake, watawasilisha mahitaji yao kupitia EACLC, huku Soko la Yiwu likiratibu ununuzi na usafirishaji wa bidhaa hadi Afrika Mashariki.
Yiwu lina zaidi ya maduka 75,000 yanayouza bidhaa za aina mbalimbali, zikiwemo vifaa vya nyumbani, nguo na viatu, vifaa vya umeme, vito na mapambo pamoja na bidhaa nyingine zinazohitajika katika soko la Afrika.
Makubaliano hayo yanatarajiwa kupunguza gharama za uagizaji wa bidhaa, kuokoa muda wa wafanyabiashara na kuongeza ufanisi katika upatikanaji wa bidhaa kutoka China, sambamba na kufungua fursa zaidi za biashara kwa wafanyabiashara wa Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya uzinduzi wa makubaliano hayo uliofanyika jana, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Aristides Mbwasi, alisema ushirikiano huo una manufaa makubwa kwa wafanyabiashara kutokana na hadhi ya Soko la Yiwu, ambalo linahudumia wanunuzi kutoka sehemu mbalimbali duniani.
"Ushirikiano huu utawasaidia wafanyabiashara wetu kupunguza gharama za biashara. Badala ya kusafiri kwenda China kufuata bidhaa katika soko la Yiwu, sasa bidhaa hizo zitapatikana hapa hapa Tanzania," amesema.
Mbwasi amesema bidhaa zitakazoletwa kupitia mfumo huo zitakuwa halisi na zenye ubora, huku zikiwa zimethibitishwa na mamlaka husika. Ameongeza kuwa ushirikiano huo pia utatoa fursa ya kutangaza na kukuza bidhaa zinazozalishwa Tanzania katika masoko ya kimataifa.
Akiwa anamwakilisha Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Denis Londo, Mbwasi amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha mazingira ya biashara, ikiwemo kuhakikisha EACLC inakuwa kitovu kikuu cha biashara kwa ukanda wa Afrika Mashariki.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa EACLC, Dk Lisa Wang, amesema makubaliano hayo ni sehemu ya mkakati wa kituo hicho wa kurahisisha upatikanaji wa bidhaa kutoka China kwa wafanyabiashara wa Tanzania na nchi jirani.
"Tunatarajia makubaliano haya yatazaa matokeo chanya na Watanzania watanufaika zaidi. Badala ya kusafiri kwenda China, sasa wataweza kufika katika kituo hiki na kuagiza bidhaa wanazohitaji kwa urahisi," amesema.
Amesema mfumo huo utawasaidia wafanyabiashara kuokoa muda na gharama walizokuwa wakitumia kusafiri nje ya nchi, huku ukiwaongezea uhakika wa kupata bidhaa kutoka kwa wauzaji wanaoaminika.
Naye Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao katika kituo hicho, Ayoub Katuga, amesema makubaliano hayo yataongeza ushindani wa biashara kwa kuwa yataondoa utegemezi mkubwa wa mawakala wa kati ambao wamekuwa wakiongeza gharama za uagizaji wa bidhaa.
"Wafanyabiashara wanaoagiza bidhaa kutoka China sasa wana fursa ya kuja hapa Ubungo na kufanya manunuzi ya bidhaa mbalimbali kutoka China bila kulazimika kutumia watu wa kati ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakiongeza gharama za uagizaji," amesema.
Amesema hatua hiyo itarahisisha upatikanaji wa bidhaa kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati, huku ikichochea ukuaji wa biashara kati ya Tanzania, China na nchi nyingine za Afrika Mashariki.