Mpigadebe aliyegeukia utengenezaji mashine

Msimamizi wa kiwanda, Rashidi Juma (kushoto) akioneysha mashine ya kufyatulia matofali aliyoiyunda katika ofisi yake iliyopo Mwenge jijini Dar es Salaam. Picha na Sunday George

Ukisikia mtu anafanya kazi ya kupigadebe kuna picha fulani inakujia kichwani kutokana na unaowaona. Picha ya jumla si ile inayoonyesha matumaini kuwa kundi hilo linaweza kupiga hatua kubwa maishani.

Gazeti hili limefanya mahojiano na Rashid Kundai (46), mpigabede mstaafu wa daladala jijini Dar es Salaam ambaye hivi sasa anamiliki karakana ya kuunda mashine ndogondogo.

Baada ya kupigadebe kwa miaka miwili kuanzia mwaka 1999, baadaye alikuwa kondakta wa gari alilokuwa akiendesha kaka yake kabla hajaachana na kazi hiyo na kuanza kufanya kazi ya uchomeleaji, huku matarajio yake ya kiuchumi hayakufikiwa hivyo akarudi kupigadebe.

“Kule kwenye kuchomelea nilikuwa chini ya mtu, hivyo fedha kidogo ilikuwa haionekani wakati huku kwenye kupiga debe nilikuwa nimeshazoea kushika hela mwenyewe na mzunguko nauona kila siku naangalia nimeingiza kiasi gani,” anasema.

“Ukiwa chini ya mtu ni changamoto, unaweza kufanya kazi siku nzima usipate hata Sh100, baada ya hapo unarudi nyumbani umechoka na macho yanauma na huna kitu mfukoni, nikaseme bora nirudi kupiga debe,” anasema Kundai.

Aliporudi kuendelea kupiga debe, anasema hakukaa sana akaelekea kwenye ufundi wa pikipiki na akabobea na kuwa fundi mzuri, kazi ambayo aliifanya kwa muda mrefu na kumpa fursa ya kufanya kazi kwenye taasisi za Serikali kwa mikataba ya muda mfupi, hivyo kupata mtaji wa shughuli anayoifanya sasa.

“Kazi yangu ya kutengeneza pikipiki ndiyo iliyonipa fursa ya kufanya kazi katika taasisi hizo, kwani nilikuwa nikikutana na kufanya kazi na watu tofauti, baadaye walivutiwa na huduma yangu nikapata mkataba wa kwanza wa kufanya kazi,” alisema Kundai.

Anasema safari yake ilikuwa ngumu kwa kuwa kila alichofanya kilikuwa chini ya usimamizi wa watu wengine na siku zote alikuwa anapambana ili mwisho aweze kusimama mwenyewe na alikuwa bado ana ndoto ya kuwa mjasiriamali wa kuchonga chuma.

Anaongeza kuwa alianza kwa kutengeneza mashine tatu za kufyatua matofali za mkono, baada ya kuziuza akatengeneza nyingine saba na biashara ikaendelea na akahamia katika utengenezaji wa mshine za umeme, bidhaa ambayo ndiyo kuu katika uzalishaji wake.

Anasema ujuzi wa kutengeneza mashine hizo pamoja na kuwa alishawahi kufanya kazi ya kuchomelea miaka ya nyuma, ujuzi wake unatokana na kukaa karibu na watu wanaofanya shughuli hizo na kiu yake ya mafanikio kutokana na maisha magumu.

“Ukipiga hesabu umkabe mtu ili upate fedha unaona mambo yanakuwa magumu, ndiyo maana nikajikuta nimedondokea hapa, nilikutana na wadau wakanipa wazo nami nikawatafuta mafundi wanaonizidi uwezo ndo nikawa nao jirani,” anasema huku akisisitiza kuwa kitu muhimu maishani ni nia.

Anasema mtaji wake wa kuanzia hakukopa, ila alitunza fedha kutokana na kazi alizokuwa akifanya na alipofikisha Sh1 milioni akaanza kutengeneza mashine hizo tatu ambazo zilimpa faida ya Sh150,000.

“Baada ya hapo nilihamasika na kuona naweza kupata chochote kwani kadri ninavyouza napata kiasi kikubwa cha fedha na wakati huo biashara ilikuwa na mzunguko mzuri nikaweza kutunza akiba kutoka kwenye biashara hiyo,” alisema.

Kundai anasema biashara ya kuchonga vyuma aliianza mwaka 2017 na anashirikiana na wasaidizi wake kuchonga mashine hizo, akisema kwake kazi hiyo inamaanisha maisha, hivyo anaisimamia kwa karibu.

Kwa sasa anasema biashara imekua, kwani anapokea oda ya mashine za matofali za umeme hadi sita kwa mwezi ambazo kila moja inagharimu Sh5.5 milioni, uwezo wa karakana yake ni kutengeneza mashine tano kwa mwezi.


Mashine anazotengeneza

Sehemu kubwa ya biashara yake anasema ni kutengeneza mashine ya kuchanganya mchanga na kufyatua matofali, ingawa anaunda mashine za kukamua juisi ya miwa, mafuta ya alizeti, majiko ya kuni na mkaa, masufuria na matolori.

Mbali na mashine hizo, Kundai anaweza kutengeneza vitu vinavyohusiana na uchongaji wa chuma kutokana na mahitaji ya mteja, ila biashara yake kubwa ni mashine za kuchanganya mchanga na kufyatua matofali.

“Masufuria na majiko ninayotengeneza ni yale ambayo yanaweza kutumiwa na taasisi ambazo zinahitaji kupika chakula kingi kama shule au magereza,” anasema.

Biashara ya mbunifu huyu imejikita zaidi kwenye mashine za matofauli, kwani anapokea oda chache za mashine za kukamulia miwa pamoja na mafuta ya alizeti. Hata hivyo anasema soko la mashine za kukamua alizeti ni miongoni mwa analolitamani zaidi, lakini halijawa rahisi kwake kuwapata wanunuzi kwa ukubwa anaoutaka.

“Mashine ya alizeti gharama yake inaweza kuwa hadi Sh7 milioni inayoweza kukamua kuanzia tani moja,” anasema Kundai.


Changamoto

Kundai ameisajili biashara yake, lakini bado hajafanikiwa kuwa na chapa ya utambuzi ili kuzitambulisha mashine zake.

“Kuwa na chapa ya kutambulisha bidhaa zangu ni matamanio yangu, naendelea kukua taratibu. Biashara yangu kwa kiasi imesogea, lakini nilikuwa natamani isogee zaidi ya hapo,” anasema Kundai.

Katika harakati za kujaribu kukuza biashara yake anasema ameshawahi kuomba mkopo kwenye taasisi za fedha, lakini hajafanikiwa hivyo kuikumbusha Serikali kuangalia namna ya kuwashika mkono wenye viwanda vidogo.

“Kukaa na kusubiri akiba yako itoshe ni changamoto, nahitaji mkopo, lakini nakutana na changamoto kila taasisi ninayoifuata wanasema hawawezi kunishika mkono kwa kuwa bado niko chini ya mtu (sina jengo la karakana),” anasema.

Ili kufungua karakana ya viwango inavyotaka benki kumfanya akopesheke, ikiwamo kumiliki jengo, anasema inahitaji mtaji mkubwa ambao yeye hana, ndiyo maana katika kuomba mkopo huwaeleza mpango wote wa biashara ili kuwashawishi lakini anakwama.

Anasema anahitaji mkopo kwa ajili ya kuboresha biashara yake kwa kuweka mashine za kumsaidia kazi ili kuongeza uwezo wa uzalishaji kutoka wastani wa mashine moja kwa siku tano iwe ni kazi ya saa kadhaa tu.

“Huwa naangalia mashine nyingi zinazonifaa kwa kazi zangu zinauzwa Sh20 milioni, nyingine Sh30 milioni, lakini nahitaji kama milioni Sh100, japo nikipata hata Sh30 milioni ili ninunue mashine ambayo najua itanisaidia kukua kutoka hapa nilipo hata kama ni kwa muda mrefu,” anasema.