Ujenzi mtambo kuzalisha sukari kumaliza uhaba

Dar es Salaam. Wakati ujenzi wa mtambo mdogo wa kuzalisha sukari ukitarajiwa kukamilika Juni mwaka huu, hatua hiyo inatajwa kuwa sehemu ya juhudi za kumaliza changamoto ya uhaba wa bidhaa hiyo kufikia mwaka 2025.

Shirika la Uhandisi na Usanifu Mitambo Tanzania (Temdo), ndilo linalotekeleza mradi huo, Dumila mkoani Morogoro, uliopaswa kukamilika mwaka jana na kuanza kazi mwezi unaofuata.

Ucheleweshaji wa utoaji fedha za utekelezaji wa mradi huo ndiyo uliosababisha kuchelewa kukamilika kwa kazi hiyo, kulingana na Temdo.

Akizungumza na Mwananchi jana, Mkurugenzi wa Temdo, Profesa Frederick Kahimba alisema: “Tumepokea fedha zote kutoka kwa Serikali na Bodi ya Sukari Tanzania (SBT) kwa ajili ya kukamilisha mradi ulioanza kusanifiwa Machi 2021”.

Katika utekelezaji wa mradi huo, Serikali imetoa Sh350 milioni na SBT Sh166 milioni, huku Temdo ikichangia Sh44 milioni kusaidia ujenzi wake unaogharimu jumla ya Sh560 milioni.

Kwa mujibu wa Profesa Kahimba, kiwanda hicho kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kuchakata tani 200 za miwa na kuzalisha tani 20 za sukari kwa siku.

Hata hivyo, alisema shirika hilo lina uwezo wa kutengeneza kiwanda kidogo hata cha Sh250 milioni kulingana na mahitaji ya wateja.

“Sio ghali kama inavyoonekana gharama yake ni nafuu mara mbili zaidi ya ile ambayo mitambo inayoagizwa kutoka nje.

Kwa sasa Tanzania ina viwanda vinne vya bidhaa hiyo ambavyo ni Kagera Sugar Ltd, Kilombero Sugar, Mtibwa Sugar Estates Ltd na TPC Ltd, jumla vinazalisha takriban tani 370,000 za sukari chini ya mahitaji ambayo ni tani 670,000 kwa mwaka.

Kulingana na Ilani ya CCM, Tanzania imepanga kujitosheleza kwa uzalishaji wa sukari kufikia mwaka 2025, ikitarajia kuzalisha tani 700,000 kwa mwaka.

Kutokana na hilo, Serikali imepanga kutengeneza ajira milioni saba kutoka sekta rasmi na zisizo rasmi.

Ikumbukwe kuwa Babati na Manyara kuna viwanda vidogo vya uzalishaji sukari ambavyo mitambo imeingizwa kutoka nje na kinachofanywa na Temdo sasa ni kubuni mbinu zitakazochakata sukari nchini.

Uwezekano wa hili, utatokana na uboreshwaji wa teknolojia zitakazotumika katika viwanda hivyo, ili zifanane na zile zinazoagizwa kutoka nje na kuondoa haja ya wazalishaji kuingia gharama ya kuagiza.

Hata hivyo, takriban tani 200,000 za miwa zinaachwa bila kuuzwa kila mwaka na kwamba hatua hiyo mpya itatengeneza soko jipya kutokana na mahitaji ya malighafi. Katika juhudi za kujitosheleza kwa bidhaa hiyo, China na India zinatumia mbinu hiyo hiyo ya kuanzisha viwanda vidogo vya kuchakata miwa ili kusaidia viwanda vikubwa.

Nchi za Asia ndio vinara wa uzalishaji sukari kwa sasa, zimekuwa zikipitia mabadiliko ya hatua kwa hatua hadi kuwa wazalishaji wakubwa duniani.