Watanzania waelezwa sababu za kujiwekea akiba benki

Friday February 21 2020
akiba pic

Dar es Salaam. Watu wengi wanaamini mazoea hujenga tabia, yaani ukiwa na mazoea ya kufanya jambo fulani ukaendelea kulifanya kwa muda mrefu, hiyo itakuwa tabia.

Hivyo ndivyo ilivyo katika kuweka akiba, mtu akijijengea mazoea ya kuanza kuweka akiba kidogokidogo kupitia namna mbalimbali za utunzaji fedha, mazoea hayo yakadumu kwa muda mrefu hiyo itakuwa tabia.

Hivyo kujiwekea akiba si jambo la kushangaza katika karne hii, zipo sababu nyingi sana kwa nini ni muhimu mtu kujiwekea akiba.

Ili kulifafanua hilo, Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), imetoa rai kwa Watanzania kujenga utamaduni wa kujiwekea akiba hata kama ni fedha kidogo.

Meneja Masoko wa NBC, Alina Maria Kimaryo jana alipokuwa akikabidhi zawadi kwa washindi wa droo ya mwezi ya kampeni ya “Ibuka Kidedea na NBC Malengo',” jijini Dar es Salaam, alisema kuweka akiba kunamsaidia mtu kupata matumizi ya kawaida lakini pia inasaidia kwa ajili ya tahadhari,na sababu ya tatu ni kwa ajili ya kuwekeza zaidi.

Ili kufanikisha hilo, Benki hiyo ilizindua rasmi kampeni hiyo Oktoba mwaka jana na imeendelea kushuhudia wateja wa zamani wakiweka amana katika akaunti zao za Malengo huku wateja wapya wakijiunga na NBC Malengo kwa lengo la kujishindia zawadi na mbalimbali.

Advertisement

Maria amesema kama Watanzania wote watakuwa na utamaduni wa kujiwekea akiba, itawasaidia kuepukana na adha mbalimbali za ukosefu wa fedha.

“Kama kila Mtanzania atajiwekea lengo la kufanya hivyo hata kama ni kidogo kidogo ni faida kwake, Waswahili husema 'bandu bandu humaliza gogo,” amesema Maria.

“Tunaposema ‘Ibuka Kidedea' ni kweli tunamaanisha, Kwa sababu hadi sasa jumla ya wateja 10 wamejishindia zawadi za boda boda huku washindi wanane wameshinda safari za kwenda Sychelles na Serengeti kwa mapumziko,” amesema.

Amesema NBC Ibuka Kidedea imekuja kusaidia Watanzania kutimiza malengo yao. Meneja huyo amesema Watanzania kila mmoja anayo malengo yake.

Ametoa wito kwa wateja ambao bado  hawajajiunga na NBC Malengo wafanye hivyo ili watimize ndoto hiyo.

Maria amesema NBC inajali maisha ya wateja wake na Watanzania kwa ujumla na hiyo imekuwa moja ya sababu  inayowasukuma kuingiza bidhaa na huduma mbalimbali zinazoendana na kukidhi mahitaji.

“NBC ni benki ya kizalendo, tunajua fika mahitaji halisi ya watanzania, tunajua mahitaji ya wateja wetu, akaunti ya Malengo ya NBC ni moja ya fursa iliyoletwa na NBC ili kumuwezesha mteja wetu kujiwekea akiba kidogo  ili kutimiza malengo yake.

Pamoja na hayo meneja huyo  anasema wale wote wanaojiunga na NBC Malengo sio tu kupata nafasi ya kuibuka kidedea lakini pia wanashuhudia akaunti zao zikipata faida nono  kila mwezi hivyo kuwasaidia kutimiza malengo yao.

Katika droo ya leo (jana), washindi watano wameibuka kidedea na kujishindia pikipiki mpya aina ya Yamaha  kila mmoja huku zawadi kubwa ikipangwa kuwa pikipiki ya miguu mitatu aina ya Toyo itakayotolewa katika droo kubwa inayotarajiwa kufanyika mwezi ujao,” amesema Maria.

Mbali na droo hiyo, mshindi wa droo ya Desemba, mwaka jana, Rosemary Kibodya wa Dar es Salaam alikabidhiwa pikipiki yake, tukio lililoshuhudiwa pia na wakaguzi kutoka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania.

 


Advertisement