Yafahamu mambo muhimu kadhaa yanayoathiri thamani ya shilingi

Thursday October 22 2020
shilingi pic

Kati ya masuala muhimu kiuchumi ni thamani ya sarafu ya nchi moja ikilinganishwa na nyingine kwa sababu ina maana kubwa katika kufanikisha biashara ya kimataifa.

Thamani hii, pamoja na mambo mengine, hutegemea mwenendo wa biashara, deni la Taifa, kipato cha wananchi na uwekezaji. Ni muhimu kufahamu thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya nyingine kama vile kwacha ya Zambia, randi ya Afrika Kusini, naira ya Nigeria na dola ya Marekani.

Thamani ya shilingi ya Tanzania inapimwa kwa kuilinganisha na nyingine duniani. Kiwango cha kubadilisha shilingi kwa sarafu nyingine ndicho kipimo kikuu cha thamani ya shilingi.

Ni mazoea kuilinganisha shilingi na dola ya Marekani kwa sababu ndiyo inayotumika sana katika miamala ya kimataifa.

Kama ilivyo bei ya bidhaa za kawaida, thamani ya shilingi au sarafu nyingine yoyote hupanda na kushuka.

Thamani hushuka pale zinapohitajika shilingi nyingi kupata dola moja, na zinapohitajika shilingi chache kupata dola moja basi shilingi huwa imeimarika.

Advertisement

Katika soko huru ambako bei za bidhaa na huduma hutegemea mwingiliano wa nguvu za soko, thamani ya shilingi hutegemea uhitaji wake sokoni pia.

Tangu katikati ya miaka ya 1980 Tanzania ipo katika soko huu, bei huamuliwa na wateja na wanunuzi, hakuna mamlaka inayoingilia hilo. Katika soko ambalo Serikali huingilia nguvu za soko kwa mkono usioonekana, thamani hii haitegemei nguvu za soko bali uamuzi wa kisiasa.

Kwa kiasi kikubwa, Tanzania ilikuwa katika hali hii kati ya mwaka 1967 hadi katikati ya miaka ya 1985.

Mauzo, ununuzi wa nje

Kiuchumi, biashara ya kimataifa huathiri thamani ya sarafu. Mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi ni muhimu sana katika kuimarisha thamani ya sarafu yake kwa sababu mauzo haya huingiza fedha za kigeni kama vile dola ndani ya mipaka.

Kunapokuwa fedha nyingi za kigeni katika uchumi, gharama za kuzibadilisha hushuka. Gharama inaposhuka, thamani ya sarafu ya ndani, shilingi, hupanda.

Kwa hiyo uimara wa shilingi unategemea kiasi cha bidhaa na huduma zinazouzwa nje ya nchi. Pale thamani ya mauzo ya nje inapokuwa kubwa kuliko ununuzi toka nje, thamani ya shilingi huimarika hivyo ni muhimu kuuza zaidi nje ya nchi ingawa kiuhalisia mauzo ya Tanzania huingiza nchini fedha kidogo kuliko zinazotoka kulipia ununuzi nje ya nchi.

Kama zilivyo nchi nyingine, Tanzania inategemea bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi. Katika nadharia na uhalisia wa uchumi wa kimataifa, hamna nchi iliyojaliwa rasilimali zote zinazoitajika kuzalisha bidha na huduma zinazohitajika.

Ili kukidhi tusivyozalisha nchini au ambavyo ni ghali zaidi kuzalisha, inabidi kununua kutoka nje hivyo kulipa kwa fedha za kigeni kama vile dola, Euro, pauni au yuan.

Takriban asilimia 60 ya ununuzi wote kutoka nje hulipwa kwa dola. Ununuzi huu husababisha fedha za kigeni kuondoka nje ya Tanzania.

Fedha za kigeni zikiwa chache sokoni, bei yake hupanda, thamani ya shilingi hushuka hivyo shilingi nyingi zaidi huhitajika kuipata dola ya kuagizia huduma au bidhaa kutoka nje.

Fedha kutoka ughaibuni

Pamoja na thamani ya shilingi kuathiriwa na mauzo na ununuzi wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi, fedha zinazotumwa nchini na Watanzania waishio ughaibuni muhimu katika kuilinda thamani ya shilingi.

Wakituma fedha za kigeni nyumbani, fedha hizi huingia katika mfumo wa benki na waliotumiwa hupokea shilingi. Kwa njia hii, fedha za kigeni huongezeka hivyo kuimarisha shilingi.

Kwa baadhi ya nchi kama Afrika Magharibi, India na Pakistani, mapato makubwa ya fedha za kigeni hutokana na watu wao wanaofanya kazi nje ya nchi na kutuma fedha nyumbani kwa ndugu, jamaa na marafiki.

Misaada na uwekezaji

Tanzania hupokea misaada kutoka nchi mbalimbali wahisani. Misaada hii huja katika fedha za kigeni hivyo kuchangia kuimarisha shilingi japokuwa nchi haipaswi kuitegemea misaada.

Hii hutokea pia kwa uwekezaji unaoingia nchini kutokana na wawekezaji wa kigeni wanaokuja na sarafu zao.

Jambo la msingi ni kwamba misaada na uwekezaji huu vinaongeza fedha za kigeni hasa dola ya Marekani sokoni hivyo kushusha bei yake na kuiimarisha shilingi.

Advertisement