Zanzibar, Yas kutumia Sh300 bilioni kusambaza intaneti
Muktasari:
- Kupitia makubaliano hayo kati ya Yas Fibre na Wakala wa Miundombinu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Zanzibar (ZICTIA), zaidi ya kaya 100,000 zinatarajiwa kuunganishwa na huduma ya intaneti ya kasi ndani ya miaka mitatu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huo.
Dar es Salaam. Zanzibar imesaini mkataba wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi wenye thamani ya takribani Sh300 bilioni na kampuni ya Yas Fibre kwa ajili ya kupanua miundombinu ya intaneti ya nyaya za mawasiliano kwa kipindi cha zaidi ya miaka 20.
Hatua hii inalenga kuharakisha mageuzi ya kidijitali na kuongeza upatikanaji wa huduma za intaneti visiwani humo.
Kupitia makubaliano hayo kati ya Yas Fibre na Wakala wa Miundombinu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Zanzibar (ZICTIA), zaidi ya kaya 100,000 zinatarajiwa kuunganishwa na huduma ya intaneti ya kasi ndani ya miaka mitatu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huo.
Viongozi mbalimbali wamesema mradi huo ni miongoni mwa uwekezaji mkubwa wa muda mrefu katika sekta ya miundombinu ya kidijitali kuwahi kufanyika Zanzibar.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Yas Fibre, Maxime Woimant amesema hatua hiyo ni mwanzo wa zama mpya za maendeleo ya kidijitali Zanzibar.
"Leo hatusaini tu makubaliano, bali tunaweka msingi wa sura mpya ya ukuaji wa kidijitali, ubunifu na fursa kwa Zanzibar," amesema.
Amesema uwekezaji huo utaongeza upatikanaji wa huduma ya intaneti ya uhakika na nafuu kwa kaya, biashara na taasisi mbalimbali katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Woimant amesema miundombinu ya kidijitali imekuwa nguzo muhimu ya ukuaji wa uchumi, ujumuishaji wa kijamii na ushindani wa kiuchumi, akieleza kuwa huduma bora za intaneti zitafungua fursa zaidi katika elimu, afya, ujasiriamali na utoaji wa huduma za umma.
Kwa mujibu wake, wanafunzi watanufaika kwa kupata rasilimali za kujifunzia kidijitali kwa urahisi zaidi, huku vituo vya afya vikitarajiwa kuboresha huduma kupitia mifumo ya afya ya kidijitali inayotegemea mtandao wa uhakika.
“Pia wafanyabiashara na wajasiriamali watapata mazingira bora ya kuvumbua na kushindana katika masoko ya ndani na nje ya nchi,” amesema.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu Zanzibar, Naibu Katibu Mkuu, Hawaa Mbaye amesema mahitaji ya huduma za intaneti yameongezeka kwa kasi kutokana na matumizi makubwa ya mifumo ya kidijitali katika biashara, elimu, afya, utalii na utawala wa umma.
Amesema ushirikiano huo unaonyesha imani inayoongezeka ya sekta binafsi katika sekta ya Tehama Zanzibar pamoja na dhamira ya Serikali kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya kisasa.
"Mafanikio ya ushirikiano huu yatapimwa kwa matokeo halisi kwa wananchi, ikiwemo kuongezeka kwa maeneo yenye huduma za fibre optic, kuboreshwa kwa ubora wa intaneti, kupungua kwa changamoto za mawasiliano na kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia katika maisha ya kila siku," amesema.
Kwa mujibu wa wizara hiyo, mradi huo unaendana na Mpango wa Maendeleo wa Zanzibar (ZADEP) 2021/22–2025/26 pamoja na Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050, ambayo yote yanaipa sekta ya TEHAMA nafasi muhimu katika kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kijamii.
Mkurugenzi Mtendaji wa ZICTIA, Shukuru Awadhi Suleiman amesema mradi huo utaunganisha miundombinu ya mkongo wa taifa iliyowekezwa na Serikali na uwekezaji wa sekta binafsi katika kupeleka huduma hadi kwa watumiaji wa mwisho, hatua itakayosaidia kupunguza gharama za intaneti.
Amesema wananchi wengi bado wanategemea huduma za intaneti za simu ambazo mara nyingi ni ghali na hazina uthabiti wa kutosha.
"Tunataka wananchi wapate huduma bora zaidi za intaneti kwa gharama nafuu. Serikali tayari imewekeza katika miundombinu ya msingi ya mawasiliano, huku mshirika wetu akielekeza uwekezaji wake katika kuunganisha nyumba na biashara," amesema.
Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu Zanzibar, Mudrick Soraga, alisema huduma bora za mawasiliano zitasaidia kupunguza pengo la kidijitali na kuongeza upatikanaji wa huduma mbalimbali za mtandaoni.
Amesema baadhi ya hoteli na vituo vya utalii bado vinakabiliwa na changamoto za mawasiliano ya intaneti ambazo huathiri huduma kwa wageni na uendeshaji wa shughuli zao.
"Mageuzi ya kidijitali hayawezi kufikiwa bila kuwa na miundombinu imara ya mawasiliano. Kupitia ushirikiano na sekta binafsi tunaweza kwenda kwa kasi zaidi na kuwafikia wananchi wengi zaidi," amesema.
Ujenzi wa miundombinu hiyo umeanza kabla ya kusainiwa rasmi kwa makubaliano hayo, huku utekelezaji ukianzia Mji Mkongwe kabla ya kusambazwa katika maeneo mengine ya Zanzibar.