Siri ya Yas kuongoza katika ubora, viwango vya mtandao iko hapa
Ofisa Mkuu wa Teknolojia na Ufundi wa Yas Tanzania, Emmanuel Mallya kushoto) akifanya katika mahojiano maalumu na Mwandishi wa habari wa Mwananchi, Ephrahim Bahem katika ofisi za makao makuu ya Yas zilizopo jijini Dar es Salaam.
Katika zama ambazo matumizi ya intaneti yamekuwa sehemu muhimu ya maisha ya kila siku, ushindani wa kampuni za mawasiliano hauko tena katika idadi ya wateja pekee, bali katika ubora wa huduma wanazopata.
Ni katika mazingira hayo ambapo kampuni ya Yas Tanzania imezindua kampeni yake mpya ya “Mtandao wa Viwango”, ikisema hatua hiyo ni matokeo ya mageuzi makubwa ya kiteknolojia na uwekezaji yaliyofanyika ndani ya miaka ya karibuni.
Katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Ofisa Mkuu wa Teknolojia na Ufundi wa Yas Tanzania, Emmanuel Mallya, anasema kauli mbiu ya Mtandao wa Viwango si matangazo ya kawaida ya biashara, bali ni utambulisho mpya wa mtandao huo baada ya kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika kuboresha huduma zake.
Anasema mageuzi hayo yamelenga kuhakikisha mtandao wa Yas unapatikana kwa ubora uleule katika maeneo mbalimbali ya nchi, mijini na vijijini.
“Tumefanya mapinduzi makubwa ya mtandao wetu. Lengo letu ni kuhakikisha tunatoa huduma yenye ubora wa juu na inayopatikana karibu kila sehemu ya Tanzania,” anasema Mallya.
Kwa mujibu wa Mallya, mtandao wa Yas sasa unawafikia zaidi ya asilimia 96 ya Watanzania, jambo linalouweka miongoni mwa mitandao yenye ueneaji mkubwa nchini.
Hata hivyo, anasema jambo la msingi si kufika kwa mtandao pekee, bali ubora wa huduma zinazopatikana katika maeneo hayo.
Anasema moja ya viashiria vya ubora wa mtandao ni kasi ya kupakua na kupakia taarifa, ikiwemo video, picha na nyaraka mbalimbali.
“Mtandao wa viwango ni ule ambao haukwami, hauna kwikwi na unafanya kazi kwa kasi ileile bila kujali kama mteja yupo mjini au kijijini,” anasema.
Kwa mujibu wa Mallya, Yas imejenga mtandao wake kwa msingi wa teknolojia ya 4G katika maeneo mengi ya nchi, huku ikiendelea kusambaza huduma za 5G katika miji mikubwa na maeneo ya kimkakati.
Anasema tofauti na kipindi cha nyuma ambapo huduma nyingi zilitegemea zaidi teknolojia za 2G na 3G, sasa mahitaji ya watumiaji yanahitaji uwezo mkubwa zaidi wa kubeba data.
“Leo hii watu wanatuma video, wanafanya mikutano ya mtandaoni, wanaendesha biashara kupitia intaneti na hata wakulima wanatumia teknolojia kupata taarifa za masoko. Haya yote yanahitaji mtandao wenye uwezo mkubwa,” anasema.
Ofisa Mkuu wa Teknolojia na Ufundi wa Yas Tanzania, Emmanuel Mallya akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi.
Mbali na huduma za data, Mallya anasema kampuni hiyo imewekeza pia katika kuboresha ubora wa sauti wakati wa mawasiliano ya simu.
Anasema kwa sasa mtandao wa Yas unatoa huduma za sauti kwa viwango vya HD na HD Plus, jambo linalosaidia kuongeza usikivu na kupunguza changamoto ya simu kukatika katikati ya mazungumzo.
“Tunataka mteja wetu asisikie tu sauti, bali aisikie kwa ubora wa hali ya juu bila kukatika,” anasema.
Msingi wa mafanikio hayo, kwa mujibu wa Mallya, unatokana na uwekezaji mkubwa ambao kampuni imeufanya katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Anasema Yas imewekeza zaidi ya Sh1 trilioni katika kuboresha miundombinu ya mawasiliano nchini, Jambo linalowafanya kuwa mtandao wenye minara mingi zaidi kuliko mtandao mwingine wowote. “Minara yetu ni 1,000 zaidi ya anayetufuatia, jumla ya minara yetu ni 4800”
“Uwekezaji huu umeelekezwa katika upanuzi wa mtandao, uwekaji wa miundombinu ya faiba na kuhakikisha minara yetu mingi inatumia teknolojia ya 4G huku miji muhimu ikihudumiwa na 5G,” anasema.
Mbali na mtandao wa simu, Yas pia imeingia kwa nguvu katika huduma za intaneti ya nyumbani kupitia teknolojia ya faiba.
Kwa sasa huduma hizo zinapatikana katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam yakiwemo Mbweni, Sinza, Goba na Kigamboni, huku mipango ya kuzipeleka Dodoma, Arusha na Mwanza ikiwa inaendelea.
Mallya anasema kuna dhana kwamba kuenea kwa huduma za faiba kunaweza kupunguza matumizi ya intaneti ya simu, lakini kwa mtazamo wake teknolojia hizo mbili zinakamilishana badala ya kushindana.
“Faiba inaweza kutumika nyumbani kwa ajili ya huduma nyingi zinazohitaji intaneti ya kasi kubwa, lakini wakati huohuo mtu huyo huyo ataendelea kutumia simu yake akiwa nje ya nyumba. Teknolojia hizi zinasaidiana,” anasema.
Katika kuthibitisha ubora wa mtandao, Mallya anawashauri watumiaji kutumia programu ya kupima kasi ya intaneti ya Speedtest ya kampuni ya kimataifa ya Ookla.
Anasema tofauti na miaka ya nyuma ambapo tathmini za ubora wa mtandao zilitegemea hisia au maoni ya watumiaji, sasa kuna mifumo ya kisasa inayotoa matokeo yanayoweza kuthibitishwa.
“Leo kuna vipimo na ripoti zinazopatikana wazi. Sisi hatusemi peke yetu kwamba tuna ubora. Kuna taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi ambazo zimekuwa zikithibitisha viwango vyetu,” anasema.
Anasema ripoti mbalimbali za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zimekuwa zikionesha Yas kuwa miongoni mwa mitandao inayoongoza katika ubora wa huduma kwa miaka kadhaa mfululizo.
Kutambuliwa huko, anasema, ni motisha inayowasukuma kuendelea kuwekeza zaidi katika kuwahudumia wateja.
“Tunapotambuliwa ndani na nje ya nchi tunapata sababu zaidi ya kufanya kazi kwa bidii na kuwapa wateja huduma bora zaidi,” anasema.
Katika kuendelea kujenga mtandao wa kizazi kijacho, Mallya anasema Yas inaendelea kupanua huduma za 5G katika maeneo mbalimbali nchini.
Anasema upanuzi huo unazingatia pia kiwango cha matumizi ya vifaa vinavyoweza kutumia teknolojia hiyo.
“Tunatazama maeneo ambayo yana watumiaji wengi wa vifaa vya 5G na kuhakikisha huduma hiyo inapatikana. Ndio maana tumeanza na miji muhimu na maeneo ya kimkakati,” anasema.
Hata hivyo, ili kuwasaidia Watanzania wengi zaidi kufaidika na teknolojia hizo, Yas imeanzisha programu za kuwawezesha wateja kupata simu janja za 4G na 5G kwa gharama nafuu.
Anasema kupitia mpango huo, wateja wanaweza kupata simu kwa mfumo wa malipo ya takribani Sh1,000 kwa siku pamoja na gharama ndogo ya awali.
“Tunataka hata watu wa kipato cha kawaida waweze kumiliki simu janja na kufaidika na huduma za kisasa za kidijitali,” anasema.
Kuhusu uimara wa mtandao wakati wa majanga au hitilafu zinazoweza kutokea katika miundombinu ya mawasiliano, Mallya anasema Yas imejenga mfumo wa njia mbadala ili kuhakikisha huduma haziathiriki kwa kiwango kikubwa.
Anasema hata pale nyaya za kimataifa za mawasiliano ya chini ya bahari zinapokatika, kampuni hiyo huwa na njia nyingine za kuendelea kutoa huduma.
“Hata sasa kuna maeneo ambayo yameathiriwa na kukatika kwa nyaya za faiba, lakini kutokana na uwekezaji wetu katika njia mbadala, wateja wengi hawaoni athari kubwa katika matumizi yao ya kila siku,” anasema.
Kwa sasa, anasema, Yas hutumia njia kuu za kimataifa za mawasiliano kupitia mifumo ya EASSy, 2Africa na SEACOM, jambo linaloongeza uthabiti wa huduma zake.
Mbali na mtandao wa simu na intaneti, Mallya anasema kampuni hiyo imeendelea kuboresha huduma nyingine zinazowagusa moja kwa moja wateja, ikiwemo huduma za kifedha, programu ya Yas App pamoja na maduka ya huduma kwa wateja yaliyoenea nchini kote.
“Tunachokisema ni rahisi sana. Tuna kasi, tuna ubora na tuna upatikanaji. Huo ndio msingi wa Mtandao wa Viwango,” anasema.