Absa, WWF wapanda miti 1,300 Pugu Kazimzumbwi
Meneja Huduma za Jamii na Matukio wa Benki ya Absa Tanzania, Abigail Lukuvi (kulia), Mhifadhi Misitu wa Wilaya ya Kisarawe, Bw. Baraka Mtewa na Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Utawala wa Shirika la Uhifadhi wa Mazingira (WWF), Manyerere Wajama, wakishirikiana kupanda miti kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira duniani.
Muktasari:
- Absa inaendelea kutekeleza dhamira yake ya kuchangia maendeleo endelevu kwa jamii kupitia kaulimbiu yake ya “Kuiwezesha Afrika ya Kesho, Pamoja, Hatua Moja Baada ya Nyingine,” ikibainisha kuwa Msitu wa Pugu Kazimzumbwi una mchango mkubwa kwa Jiji la Dar es Salaam kwa kusaidia kusafisha hewa.
Kisarawe. Wafanyakazi wa Benki ya Absa Tanzania, kwa kushirikiana na Shirika la Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF), wamepanda miti 1,300 katika Msitu wa Pugu Kazimzumbwi, wilayani Kisarawe Mkoa wa Pwani, katika kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani.
Akizungumza katika kazi ya upandaji miti hiyo jana, Jumamosi, Juni 13, 2026, Mkurugenzi wa Masoko na Mawasiliano wa Absa Tanzania, Aron Luhanga, amesema upandaji miti ni sehemu muhimu ya juhudi za kuhifadhi mazingira kutokana na mchango mkubwa wa misitu katika ustawi wa maisha ya binadamu.
Amesema Absa inaendelea kutekeleza dhamira yake ya kuchangia maendeleo endelevu kwa jamii kupitia kaulimbiu yake ya “Kuiwezesha Afrika ya kesho, pamoja, hatua moja baada ya nyingine,” akibainisha kuwa Msitu wa Pugu Kazimzumbwi una mchango mkubwa kwa Jiji la Dar es Salaam kwa kusaidia kusafisha hewa.
“Msitu huu ni muhimu kwa afya ya wakazi wa Dar es Salaam kwa kuwa unasaidia kufyonza hewa chafu na kuchangia upatikanaji wa hewa safi,” amesema Luhanga.
Ameongeza kuwa, kupitia kaulimbiu yao ya “Stori yako ina thamani,” Benki ya Absa inaamini kila hatua ya Mtanzania ina mchango mkubwa, hivyo kushiriki upandaji miti ni sehemu ya kuandika simulizi chanya ya mazingira ya Jiji la Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Masoko na Mawasiliano wa benki hiyo, Aron Luhanga (kushoto) na Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja na Huduma za Kidigitali wa Benki ya Absa Tanzania, Samuel Mkuyu, wakipanda miti kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira duniani, kwa kushirikiana na Shirika la Uhifadhi wa Mazingira (WWF), katika msitu wa Pugu Kazimzumbwi, Wilayani Kisarawe, mkoani Pwani jana.
Kwa upande wake, mkuu wa kitengo cha fedha na utawala wa WWF, Manyerere Wajama, amesema ushirikiano huo ni uwekezaji muhimu katika kulinda mazingira na afya ya jamii kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Amesema Msitu wa Pugu Kazimzumbwi ni rasilimali muhimu kwa wakazi wa Kisarawe na maeneo jirani kutokana na mchango wake katika kuboresha ikolojia na kufyonza hewa chafu.
“Tunachokifanya leo ni uwekezaji kwa maisha ya baadaye. Tunahitaji ushirikiano wa Serikali, sekta binafsi na wananchi kuhakikisha miti hii inalindwa,” amesema Wajama.
Naye Naibu Ofisa Misitu wa Wilaya ya Kisarawe, Idd Mbaruku, amesema kazi hiyo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uhifadhi wa msitu huo kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na wadau wengine.
Amesema Msitu wa Pugu Kazimzumbwi ni muhimu kwa mazingira ya Dar es Salaam kutokana na mchango wake katika kufyonza hewa chafu inayotokana na shughuli za viwanda na ukuaji wa miji
“Msitu huu ni mapafu ya Dar es Salaam, hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha miti hii inapandwa na kulindwa,” amesema Mbaruku.Bottom of Form