Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hiki ndicho kinakwenda kutokea kesho kesi ya Baba Levo

Muktasari:

  • Jaji Mkuu atoa GN kuiongezea muda wa miezi sita



Kigoma. Sasa ni rasmi shauri la uchaguzi kupinga ushindi wa Mbunge wa Kigoma Mjini, Clayton Chipando au ‘Baba Levo’ kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) kesho linaingia katika hatua muhimu ya usikilizwaji, baada ya kuvuka viunzi vya hatua mbalimbali za kisheria.

Hatua hiyo inakuja sambamba na hatua ya Jaji Mkuu wa Tanzania, George Masaju, naye kutoa notisi ya kuongeza muda wa kusikiliza shauri la uchaguzi ya mwaka 2026, kwa kuliongezea shauri hilo muda wa usikilizwaji wa miezi sita zaidi.

Uamuzi wa Jaji Mkuu umo katika Tangazo la Serikali namba 124 la 2026 ambalo limewekwa katika TanzLII ambayo ni tovuti ya Serikali ya Tanzania inayochapisha maamuzi, sheria na kanuni bure mtandaoni zikiwamo hukumu za Mahakama Kuu.

“Kwa kuzingatia mamlaka aliyopewa Jaji Mkuu kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani, muda wa kusikiliza shauri hilo unaongezwa kwa muda wa miezi sita kuanzia Mei 15 hadi Novemba 14, 2026,” linasema tangazo hilo.

Kifungu cha 144 (1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya 2024 kinasema kila shauri la uchaguzi litawasilishwa ndani ya siku 30  kuanzia tarehe ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi na msimamizi wa uchaguzi.

Lakini, kifungu kidogo cha (2) kinasema Mahakama itasikiliza na kuamua shauri la uchaguzi ndani ya miezi sita kuanzia tarehe ya kuwasilisha shauri na hii ndio imemfanya Jaji Mkuu wa Tanzania, Masaju kuongeza muda wa miezi 6 mingine.

Shauri hilo namba 28949 la 2025 lililofunguliwa na wapigakura wanne ambao ni Johary Kaborour, Loum Mwitu, Pendo Kombolela na Luma Akilimali wanaotetewa na Wakili John Seka, linasikiliwa Mahakama Kuu, Masjala ndogo ya Kigoma.

Shauri hilo linalosikilizwa na Jaji Victoria Nongwa, ni dhidi ya Msimamizi wa Uchaguzi Kigoma mjini kama mlalamikiwa namba moja, Baba Levo mlalamikiwa namba mbili, na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), mlalamikiwa namba tatu.


Nini kinafanyika Jumatatu

Kwa mujibu wa ratiba ya usikilizwaji wa mashauri ya madai na jinai Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Kigoma, shauri hilo limepangwa kwa ajili ya usikilizwaji wa awali Jumatatu ya Juni 15, 2026 ili kukubaliana hoja zinazobishaniwa.

Jana Ijumaa Juni 12, 2026, Jaji Nongwa alilikubali ombi la walalamikiwa katika shauri hilo wa kukagua nyaraka za shauri hilo, kabla ya kwenda kwenye usikilizwaji wa awali, kwa kuwa nyaraka zilizowasilishwa na wadai zinahusu pia matokeo.

Wakili Seka anayewawakilisha wadai katika shauri hilo alilithibitishia gazeti hili kuiona notisi hiyo ya Jaji Mkuu na kwamba usikilizwaji wa awali utafanyika Jumatatu ili kupata hoja zinazobishaniwa ili kesi sasa ianze kusikilizwa rasmi.

“Ni kweli Jaji Mkuu ameongeza muda wa miezi sita na jana (Ijumaa ) wenzetu waliomba wapewe muda wa kukagua nyaraka za usikilizwaji wa awali kwa sababu zina pia matokeo hivyo waliomba wapewe muda zaidi kuzipitia,”alisema.

Wakili Seka alisema Jaji alikubaliana na ombi hilo na kuwapa hadi Jumatatu ya Juni 15, 2026 ili siku hiyo usikilizwaji wa awali ufanyike kupata hoja zinazobishaniwa ili baada ya hapo lipangwe tarehe ya kusikilizwa kwa wao kuanza kuleta mashahidi.


Malalamiko ya wapiga kura

Wapiga kura hao, wamewasilisha sababu 35 kuthibitisha kile wanachodai kuwa ubunge wa Baba Levo ni batili, hivyo ufanyike uchaguzi mdogo katika jimbo hilo.

Katika uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 29, 2025, Baba Levo aliyeapishwa kuwa mbunge, bungeni mjini Dodoma Novemba 11, alipata kura 35,727 akifuatiwa na mshindani wake wa karibu, Zitto Kabwe wa ACT Wazalendo aliyepata kura 16,619.

Wanaomba mahakama itamke kuwa msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo na wasaidizi wake wachukuliwe hatua za kinidhamu na kijinai kwa kuvuruga kwa makusudi mchakato wa uchaguzi kwa kuzingatia matakwa ya sheria.

Halikadhalika wanaomba kufanyika kwa uchunguzi wa kura kuthibitisha kuwa Baba Levo hakuwa mgombea aliyepata kura nyingi katika Jimbo la Kigoma na hivyo hakustahili kutangazwa kuwa mshindi na uteuzi wake haukuwa halali.

Mbali na ombi hilo, lakini wanaiomba mahakama  iamuru kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo hilo, kulipa fidia ya gharama za kufungua na kuendesha kesi hiyo ikiwa ni pamoja na kugharamia mashahidi wa kesi hiyo.

Wanaiomba pia itoe tamko kuwa walalamikaji wameomba na kupatiwa msaada wa kisheria kutoka Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) na wana mamlaka ya kisheria ya kufugua shauri bila kupitia mchakato wa kuweka dhamana ya uchaguzi.


Sababu za kufungua shauri

Kulingana na nyaraka zilizowasilishwa kortini, walalamikaji katika shauri hilo wanadai kuathiriwa kwa matokeo ya uchaguzi, kunatokana na kutozingatiwa kwa masharti ya sheria ya uchaguzi ya mwaka 2024 yaliyofanywa na msimamizi.

Kuhusu kutozingatiwa kwa masharti ya sheria ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani ya mwaka 2024, walalamikaji wameorodhesha vitendo 13 wanavyodai vilifanyika na kuathiri uhalali wa uchaguzi wa mbunge wa Kigoma mjini.

Wanadai mawakala ACT Wazalendo wa vituo karibia vyote,  kuzuiwa bila kuzingatia matakwa ya sheria, kuingia na Daftari la wapiga kura ili kujiridhisha ikiwa inaruhusiwa kisheria na waliondolewa vituoni na wengine kukamatwa na Polisi.

Mbali na malalamiko hayo, lakini wanadai mawakala wa ACT-Wazalendo walizuiwa kushiriki zoezi la kuhesabu kura, walinyimwa nakala ya matokeo mawakala hao kulazimishwa kusaini fomu za matokeo kabla ya zoezi la kuhesabu kura.

Wanalalamikia pia kuruhusiwa kwa upigaji holela wa kura usiozingatia sheria, taratibu na Kanuni ikiwa ni na mtu mmoja kupiga kura zaidi ya moja kwenye sanduku na  karatasi za kura kuchanwa kabla ya mpiga kura kuingia kituoni.

Pia, wanadai kuliruhusiwa upigaji holela wa kura usiozingatia sheria, taratibu na Kanuni ikiwa ni pamoja na kuurhusu mtu mmoja kuingia na vitambulisho zaidi ya kimoja akisema anawapigia kura watu wasio na uwezo wa kupiga kura na

Halikadhalika kuliruhusiwa upigaji holela wa kura usiozingatia sheria, taratibu na Kanuni ikiwa ni pamoja na kuruhusu watu kupiga kura bila kuzingatia taarifa zao katika kituo kama ni wapiga kura halali wa kituo alichoenda kupiga kura.

Wanalalamikia kufanyika kwa majumuisho ya kura ya siri bila kumjulisha mgombea wa ACT-Wazalendo wala Mawakala wake na kutobandika matokeo ya Uchaguzi wa ngazi ya Jimbo katika mbao za matangazo kama sheria inavyotaka.

Pia, wanadai watu waliruhusiwa kuendelea kuingia kupiga kura kutoka nje zaidi ya saa 10:00 jioni bila ya kuwa wamepanga mstari ikiwemo katika Kituo cha Shule ya Msingi Kabingo Kata ya Gungu, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Wanalalamikia pia kuwa mawakala walitishwa kwamba hawapaswi kuhoji chochote wanachoona au kinachoendelea ndani ya vituo na na kulikuwa ujazaji wa fomu ya matokeo wenye kasoro na usiofuata taratibu kwenye kata.

Walalamikaji katika shauri hilo pia wanadai kutumika kwa hoja za udini wakati wa kampeni za uchaguzi kunakodaiwa kufanywa moja kwa moja na Baba Levo.

Wanadai pia wakati wa mchakato wa kugombea na wakati wa kampeni, kulikuwa na vitendo vya rushwa na pia madai ya uwepo wa kura feki.

Walalamikaji wanadai kuingizwa kwenye masunduku ya kupigia kura katika baadhi ya vituo, kura feki, kura zisizo halali na kura zilizopigwa bila kufuata utaratibu kwa lengo la kumnufaisha na zilizomnufaisha mlalamikiwa wa pili, Baba Levo.

Kwamba kwenye baadhi ya vituo, Zitto alishinda lakini matokeo yamebadilishwa na kuwekwa yasiyo na uhalisia.

Walalamikiwa wamekanusha vikali madai yote hayo na kwamba kulikuwa hakuna ukiukwaji wowote wa sheria na taratibu na Baba Levo alishinda kihalali katika uchaguzi huo Jimbo la Kigoma Mjini hivyo kesi hiyo itupiliwe mbali.