Prime
Ahueni bei ya nafaka NFRA ikianza kununua mahindi
Muktasari:
- Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kutangaza mpango wa kununua tani milioni 1.2 za nafaka katika mwaka wa fedha 2026/27
Dar es Salaam. Wakulima wa Tanzania waliokuwa wakikabiliwa na kushuka kwa bei za nafaka licha ya mavuno makubwa wamepata ahueni baada ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kutangaza mpango wa kununua tani milioni 1.2 za nafaka katika mwaka wa fedha 2026/27.
Hatua hiyo inalenga kuimarisha utulivu wa soko la ndani na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha chakula katika ukanda wa Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kupitia mauzo ya ziada ya mazao nje ya nchi.
Tangazo hilo limeleta matumaini kwa wakulima katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji, huku taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikionesha kushuka kwa bei ya mahindi katika baadhi ya maeneo.
Katika wilaya za Kiteto (Manyara) na Songea (Ruvuma), gunia la mahindi limekuwa likiuzwa kwa bei ya chini hadi Sh32,000 kutoka zaidi ya Sh50,000 iliyokuwapo awali.
Katika mikoa mingine ikiwemo Songwe, Katavi, Rukwa, Dodoma na Arusha, bei zimeendelea kubaki chini ya Sh45,000 kwa gunia, hali inayowaweka wakulima katika hatari ya kupata hasara.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti dada la The Citizen Juni 23, 2026, Kaimu Mkurugenzi wa Hifadhi ya Chakula wa NFRA, Imani Nzobonaliba amesema Serikali imejipanga kutoa soko la uhakika kwa wakulima.
“NFRA inawahakikishia wananchi kwamba itanunua nafaka msimu huu kama ilivyofanya katika misimu iliyopita, mpango wetu mwaka huu ni kununua zaidi ya tani milioni moja za nafaka. Kiasi kikubwa kitakuwa mahindi, takribani tani 93,000 za mpunga na tani 7,000 za mtama,” amesema.
Amesema suala hilo linaungwa mkono na mkakati madhubuti wa usafirishaji na ukusanyaji wa mazao, huku wakulima wakubwa na wafanyabiashara wakialikwa kusambaza nafaka kupitia mikataba ya awali.
Amesema mwitikio umekuwa mkubwa, maombi ya kuuza nafaka kwa NFRA yamefikia takribani tani milioni 3.
Ili kuhakikisha wakulima wadogo katika maeneo ya mbali hawabaki nyuma, NFRA itafungua vituo vya ununuzi katika maeneo hayo.
“Tutaenda kwenye maeneo yao kwa sababu lengo letu kuu ni kuwahamasisha wakulima waendelee kuzalisha,” amesema.
Katika mgawanyo wa kanda, Makambako imepangiwa tani 140,000, Sumbawanga tani 100,000, Arusha tani 82,000 na Shinyanga tani 74,000, kanda nyingine zikiwemo Songwe, Mpanda, Kipawa na Dodoma pia zimepewa mgao wa ununuzi.
Mpango huo mkubwa wa ununuzi unakuja wakati taarifa za Mapitio ya Uchumi ya Mwezi ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Mei mwaka huu zikionyesha kuwa NFRA kwa sasa ina tani takribani 500,000 za nafaka katika maghala yake dhidi ya uwezo wa kuhifadhi tani 770,000.
Kupitia mzunguko wa mauzo na uondoaji wa akiba ya zamani, wakala huo unaendelea kutengeneza nafasi ya kupokea mavuno mapya huku ukiendelea kuhifadhi akiba ya kimkakati ya Taifa.
Katika soko la kimataifa, Nzobonaliba amesema Tanzania inaendelea kujijengea nafasi kama ghala la chakula la ukanda kwa kusambaza ziada ya nafaka kwa nchi jirani.
Amebainisha kuwa NFRA tayari imepata mkataba wa kusambaza tani 84,000 za mahindi nchini Rwanda, huku mazungumzo yakiwa katika hatua za mwisho kwa ajili ya tani 500,000 kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Pia, Chama cha Wasagaji Nafaka cha Kenya kimeonesha mahitaji makubwa ya mahindi kutoka Tanzania.
Masoko mengine yanayotarajiwa ni Malawi, Msumbiji na Zimbabwe ambako uzalishaji unatarajiwa kuwa mdogo msimu huu.
“Mnunuzi anapofika anakuta mzigo tayari kwa kusafirishwa,” amesema akieleza kuwa mifumo ya Tanzania ya ukusanyaji na uhifadhi wa nafaka imeimarika.
Ameongeza kuwa ufadhili wa mpango huo utaendelea kupitia mfumo wa kujigharamia wenyewe, ambapo mapato yanayotokana na mauzo ya nafaka yatarejeshwa katika ununuzi mpya, yakisaidiwa na Serikali pamoja na mikopo kutoka benki za biashara.
Msimu rasmi wa ununuzi wa nafaka unatarajiwa kutangazwa kati ya Julai 15 na Julai 22, 2026.
Hata hivyo, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Dk Anna Temu alionya ucheleweshaji wa ununuzi mara nyingi umekuwa ukidhoofisha juhudi za NFRA kusaidia wakulima.
“Serikali inapaswa kununua kwa bei nzuri ili kuwalinda wakulima, lakini changamoto ni kwamba mara nyingi ununuzi huanza kuchelewa. Wakulima wanahitaji fedha mara moja, si baada ya wiki kadhaa,” amesema.
Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Kilimo Tanzania (ACT), Jitu Soni ameshauri NFRA kuanzisha utaratibu maalumu wa kununua nafaka moja kwa moja kutoka kwa wakulima wadogo.
Amesema wafanyabiashara wengi hununua nafaka kwa bei ya chini kutoka kwa wakulima na baadaye kuiuza kwa NFRA kwa faida kubwa.
“NFRA inapaswa kununua moja kwa moja kutoka kwa wakulima ili waweze angalau kurejesha gharama zao za uzalishaji,” amesema.