Asilimia 96 vijana walioomba mafunzo ya kilimo wakosa

Muktasari:

  • Miongoni mwa vijana 20,227 waliojitokeza kuomba nafasi ya mafunzo ya kilimo, ni vijana 812 tu ndio waliopata nafasi sawa na asilimia 4.

Dodoma. Miongoni mwa vijana 20,227 waliojitokeza kuomba nafasi ya mafunzo ya Kujenga Kesho Mpya kupitia kilimo biashara (Building Better Tomorrow-BBT), ni vijana 812 tu ndio waliopata nafasi sawa na asilimia 4.

 Dirisha hilo lilifunguliwa Januari 10, 2023 na Wizara ya kilimo ikiwa ni maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kutaka kuzalisha ajira milioni tatu kwa wanawake na vijana katika sekta ya kilimo nchini.

Akitoa taarifa hiyo leo Alhamisi, Februari 23, 2023 Waziri wa kilimo, Hussein Bashe amesema miongoni mwa vijana waliochaguliwa wanawake ni 282 sawa na asilimia 34.73 na wanaume ni 530 sawa na asilimia 65.27.

Bashe amesema vijana hao watatakiwa kuripoti katika vituo watakavyopangiwa ifikapo Machi 17, 2023 kwaajili ya kuanza mafunzo ya miezi minne ya kilimo katika vituo 15 vilivyotengwa.

Hata hivyo, Bashe amesema Serikali haitasita kumuacha mtu atakayeonesha uzembe na makosa kwa kushindwa kufanya mafunzo au kufeli katika uzalishaji.

“Huu muda wa miezi minne utaendelea kutusaidia kujua ni yupi mwenye nia ya kuendelea na hii fursa, ambaye hana nia ataondoka mwenyewe,” amesisitiza Bashe.