Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ATCL kuanza safari Dar–Moscow

Ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL). Picha na Mtandao

Muktasari:

  • Rais Samia ametangaza ATCL kuanza safari za Dar es Salaam–Zanzibar–Moscow kuanzia Julai 2, akisema hatua hiyo itachochea utalii, biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Russia.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) litaanza rasmi safari za moja kwa moja kati ya Dar es Salaam, Zanzibar na Moscow kuanzia Julai 2 mwaka huu.

Hatua hiyo ametaja kuwa inalenga kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kiuchumi, biashara na utalii kati ya Tanzania na Russia.

Akizungumza Ijumaa, Juni 5, 2026, katika Mkutano wa Kimataifa wa Uchumi wa St. Petersburg (SPIEF 2026), Rais Samia amesema kuanzishwa kwa safari hizo kutarahisisha usafiri wa watu na bidhaa kati ya mataifa hayo mawili na kuongeza fursa za uwekezaji.

“Katika sekta ya usafiri wa anga, Shirika la Air Tanzania litaanza rasmi safari zake za Dar es Salaam, Zanzibar na Moscow ifikapo Julai 2 mwaka huu, ikiwa ndege ya kwanza kufanya safari hizo. Hatua hii itakuwa kichocheo muhimu cha kukuza na kuimarisha utalii baina ya mataifa yetu mawili,” amesema Rais Samia.

Hatua hiyo ya Rais Samia inakuja wakati Tanzania na Russia zikiendelea kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kupitia mikutano ya biashara, uwekezaji na diplomasia ya uchumi.

Viongozi wa Russia pia wameeleza kufurahishwa na ushiriki wa Tanzania katika SPIEF 2026, wakiitaja Tanzania kuwa miongoni mwa washirika muhimu wa Russia barani Afrika na eneo lenye fursa kubwa za uwekezaji.

Wamesema kuanza kwa safari za moja kwa moja za ATCL kwenda Moscow kutaimarisha zaidi mahusiano ya kidiplomasia, biashara na utalii kati ya mataifa hayo mawili.

Akizungumza baada ya hotuba ya Rais Samia, Waziri wa Maendeleo ya Uchumi wa Russia, Maxim Reshetnikov, amesema ushirikiano wa wafanyabiashara wa Tanzania na Russia unaendelea kuongezeka kupitia majukwaa mbalimbali ya biashara ya kimataifa.

“Ushirikiano wa wawekezaji na wajasiriamali wa Tanzania na Russia utaendelea wiki ijayo katika maonesho ya kimataifa hapa Russia na baadaye katika maonesho ya kimataifa ya Sabasaba nchini Tanzania,” amesema.

Ameipongeza pia Tanzania kwa kupeleka wafanyabiashara 150 kushiriki katika jukwaa hilo, akisema hatua hiyo inaonyesha dhamira ya dhati ya kukuza biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.