Baada ya miaka nane, ndege za abiria kurejea Musoma
Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa akisalimiana na baadhi ya viongozi mkoani Mara alipowasili mjini Musoma kwa ajili ya jaribio la kutua na kuruka kwa ndege katika uwanja wa ndege Musoma. Picha na Aurea Simtowe
Muktasari:
- Huduma hizo zinarejea baada ya kusitishwa tangu Machi 2018, wakati uwanja huo ulikuwa ukipokea ndege zenye uwezo wa kubeba abiria 45 pekee. Sasa, baada ya maboresho yaliyofanywa na Serikali, uwanja huo utaweza kuhudumia ndege zenye uwezo wa kubeba hadi abiria 80.
Musoma. Baada ya kipindi cha miaka minane bila huduma za ndege za abiria, wakazi wa Mkoa wa Mara wanatarajia kupata afueni kufuatia kurejea kwa safari za anga katika Uwanja wa Ndege wa Musoma kuanzia Julai mwaka huu.
Hatua hiyo inatokana na kukamilika kwa maboresho makubwa ya uwanja huo yaliyoongeza uwezo wake wa kupokea na kuhudumia ndege za ukubwa wa kati na kubwa, hatua inayotarajiwa kuimarisha usafiri na kurahisisha mawasiliano ya kiuchumi na kijamii katika mkoa huo na maeneo jirani.
Urejeaji wa huduma za ndege unatarajiwa kufungua fursa mpya za biashara, utalii na uwekezaji, sambamba na kupunguza muda wa safari kwa wananchi waliokuwa wakilazimika kutumia njia mbadala za usafiri kwa kipindi chote ambacho huduma hizo zilikuwa zimesitishwa.
Huduma hizo zinarejea baada ya kusitishwa tangu Machi 2018, wakati uwanja huo ulikuwa ukipokea ndege zenye uwezo wa kubeba abiria 45 pekee. Sasa, baada ya maboresho yaliyofanywa na Serikali, uwanja huo utaweza kuhudumia ndege zenye uwezo wa kubeba hadi abiria 80.
Hatua hiyo imejidhihirisha leo Ijumaa Juni 12, 2026 mjini Musoma baada ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kufanya safari ya majaribio katika uwanja huo, safari iliyothibitisha utayari wa miundombinu ya uwanja huo kuanza kutoa huduma za usafiri wa anga kwa viwango vinavyohitajika.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Abdul Mombokaleo amesema Uwanja wa Ndege wa Musoma ni miongoni mwa viwanja 61 vinavyosimamiwa na mamlaka hiyo na sasa umefikia hadhi ya daraja la 2C baada ya kukamilika kwa maboresho yake.
Amesema uwanja huo ulianza kutumika mwaka 1980 kwa ajili ya kuhudumia wananchi wa eneo hilo kabla ya kuchukuliwa rasmi na TAA mwaka 1999 na kwamba una umuhimu mkubwa kutokana na nafasi yake ya kuunganisha Mkoa wa Mara na nchi jirani za Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.
Kutokana na umuhimu huo, Serikali ilianza utekelezaji wa mradi wa ukarabati mwezi Aprili 2021 kwa gharama ya Sh35 bilioni.
Mradi huo ulihusisha kuboresha njia ya kurukia na kutua ndege kutoka ya changarawe yenye urefu wa mita 1,600 hadi kuwa ya lami yenye urefu wa mita 1705 pamoja na miundombinu mingine muhimu ya kiwanja hicho.
"Maboresho hayo yameongeza uwezo wa uwanja huo kupokea ndege za ukubwa wa kati zenye uwezo wa kubeba abiria 80, tofauti na ilivyokuwa awali ambapo uliweza kuhudumia ndege za abiria 45 pekee," amesema.
Amesema changamoto iliyobaki ni kukamilika kwa jengo la abiria la muda ambapo ujenzi wake unaendelea kwa utaratibu wa dharura na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi miwili ijayo.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa ATCL, Peter Ulanga amesema Mkoa wa Mara sasa unakuwa kituo cha 17 cha shirika hilo nchini, hatua itakayorahisisha usafiri kwa wananchi na wafanyabiashara wa eneo hilo.
“Hii ni fursa kubwa kwa wananchi wa Mara kutumia usafiri wa anga kufika maeneo mbalimbali nchini kwa haraka na kwa ufanisi zaidi,” amesema Ulanga.
Ameongeza kuwa shirika hilo linaendelea kupanua mtandao wake wa safari na linatarajia kufungua safari mpya za Russia, Oman na Shinyanga katika kipindi kijacho.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Suleiman Kakoso, amesema kukamilika kwa uwanja huo kutakuwa chachu ya ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Mara, hususan katika sekta za uvuvi, biashara na utalii.
Amesema bidhaa za uvuvi kutoka Musoma sasa zitaweza kusafirishwa kwa haraka zaidi kwenda masoko mbalimbali ya ndani na nje ya nchi, huku akiwataka wananchi wa Mara kutumia fursa hiyo kwa kuwekeza katika shughuli za uzalishaji na biashara.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi amesema kurejea kwa huduma za ndege kutapunguza changamoto za usafiri zinazowakabili wananchi ambao kwa sasa hulazimika kutumia safari ndefu za barabara zinazoweza kufikia saa 15 kufika katika baadhi ya maeneo.
Kanali Mtambi ameiomba Serikali kuanza ujenzi wa jengo la abiria la kudumu il uwekezaji uliofanywa uweze kuwa na tija na kuleta matokeo tarajiwa.
"Uwanja huu una manufaa makubwa kwetu, lakini bado hauna jengo la abiria pamoja na ujenzi wa jengo la dharura niiombe wizara kuhakikisha jengo la abiria la kudumu linajengwa ili uwekezaji huu mkubwa uweze kuleta matokeo chanya kwa mkoa wetu na taifa kwa ujumla," amesema Kanali Mtambi
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema mradi wa Uwanja wa Ndege wa Musoma ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga nchini ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Amesema Serikali pia imelipa Sh13.3 bilioni kama fidia kwa wakazi walioathiriwa na utekelezaji wa mradi huo.
“Mafanikio ya safari hii ya majaribio yanathibitisha kuwa kazi iliyofanyika inakidhi viwango vya kitaifa na kimataifa. Kukamilika kwa mradi huu kutaleta manufaa makubwa kwa Mkoa wa Mara kupitia ukuaji wa sekta za utalii, biashara, mifugo, kilimo na viwanda pamoja na kuongeza ajira na kipato kwa wananchi,” amesema Profesa Mbarawa.
Amesisitiza kuwa maeneo yaliyobaki yakamilishwe kwa wakati huku viwango vya usalama vikiendelea kuzingatiwa ili kuhakikisha uwanja huo unaanza kutoa huduma kwa ufanisi uliokusudiwa.