Bashe atishia kufuta leseni viwanda vya chai vinavyodaiwa na wakulima

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe akizungumza alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa wadau wa tasnia ya chai 2022, unaofanyika mjini Iringa, leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ameagiza viwanda vya chai kulipa madeni ya wakulima vinginevyo atavifutia leseni.

Iringa. Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ameagiza viwanda vya chai kulipa madeni ya wakulima vinginevyo atavifutia leseni.

Amesema haiwezekani wakulima waliopeleka chai kwenye viwanda vyao tangu Agosti, 2022 bado hawajalipwa malipo yao jambo ambalo sio sahihi.

Bashe amesema hayo jana Januari 18 wakati akizungumza katika mkutano wa Wadau wa Kilimo katika ukumbi wa Royal Palm Mjini Iringa

“Sitaki kusikia tena kwamba kuna fedha za wakulima hazijalipwa kwa muda muafaka, hatuwezi kuendelea na huu utaratibu. Ni heri nijue hakuna kiwanda kinafanya kazi lakini pesa za wakulima lipeni.

“Nitawafutia leseni, sitajali gharama za uwekezaji wenu, lipeni hela za wakulima. Mnadhani wanalishaje familia zao?  Mtu amevuna mwezi wa 10, anaishije? Hamuoni aibu?” amehoji Bashe.

Awali, Mwenyekiti wa Muungano wa Vyama vya Ushirika vya Chai Njombe (Munyulu), Wilfred Swalle amesema kijiji cha Kanikelele, Lupembe Mkoani Njombe kinadai zaidi ya Sh10 milioni fedha ambayo hawajapewa.

“Wakulima wanadai fedha nyingi na sisi wenyewe kama Mungulu kuna fedha tunazidai,” amesema Sawalle.

Meneja wa Chama cha Msingi cha Lupali, Victor Chomba amesema kwenye chama chake, chai iliyouzwa mwaka Mei mwaka jana, imelipwa Januari 13, mwaka huu.

“Kuna uzembe kusema kweli, wakulima wanahitaji kusaidiwa sana kwenye zao hili,” amesema.