Benki zinavyovuna kwa wateja mabilioni ya faida
Licha ya biashara mbalimbali kupita katika msukosuko wa kiuchumi, faida baada ya kodi katika benki zinazotoa huduma nchini imeongezeka kwa takribani asilimia 700 kutoka Sh133.89 bilioni mwaka 2018 hadi Sh934.38 bilioni mwaka 2022.
Katika miaka ya karibuni uchumi wa dunia umekumbwa na athari kubwa zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, majanga ya Uviko-19 na vita vya Russia na Ukraine, hali iliyosababisha ukuaji wake kutokuwa wa kasi inayotabirika.
Mwaka 2019 kasi ya ukuaji wa uchumi wa dunia ilikuwa asilimia 2.9 na mwaka 2020 baada ya mlipuko wa Uviko-19, ulisinyaa kwa asilimia 3.1. Mwaka 2021 uchumi uliimarika kwa asilimia 6.3, lakini kasi hiyo ikaporomoka tena na kufikia asilimia 3.4 mwaka 2022.
Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo ziliathiriwa na zinaendelea kuishi na athari za mambo hayo matatu kwa mawanda hayohayo.
Mwaka 2019/2018 ukuaji wa uchumi wa Tanzania ulikuwa na kasi ya asilimia 7.0, mwaka 2019 ukaendelea na kasi hiyo kabla ya kushuka mwaka 2020 kufikia asilimia 4.8, mwaka 2021 asilimia 4.9 na mwaka 2022 asilimia 4.7.
Akiwasilisha bungeni bajeti ya Serikali ya mwaka 2023/2024, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba aliyataja mambo hayo matatu kama sababu za Serikali kutofikia malengo yake ya ukuaji wa uchumi kwa miaka mitatu iliyopita.
Hata hivyo, Licha ya mambo hayo kuibua changamoto za kiuchumi katika nyanja mbalimbali, sekta ya benki imeshuhudia ukuaji mkubwa katika viashiria vyote vya ukuaji, huku faida ikiongezeka maradufu, ikilinganishwa na miaka mitano iliyopita.
Kupitia ripoti tofauti za BoT, Mwananchi limefanya uchambuzi wa vipengele tofauti vya ufanisi wa benki katika kipindi hiki, ikilinganishwa na miaka mitano iliyopita na kuangazia sababu za kuongezeka kwa faida za wakopeshaji hao katika nyakati ngumu za kiuchumi.
Faida iliyopatikana
Ripoti ya usimamizi wa sekta ya fedha ya BoT ya mwaka 2022 inaonyesha kuwa faida baada ya kodi iliyopatikana na katika benki zinazotoa huduma hapa nchini imeongezeka takribani asilimia 700 kutoka Sh133.89 bilioni mwaka 2018 hadi Sh934.38 bilioni mwaka 2022.
Benki mbili za CRDB na NMB kwa ujumla, faida yake mwaka 2022 ilikuwa ni takribani Sh800 bilioni, huku benki nyingine 43 zikigawana sehemu ya faida inayobakia.
Mapato yatokanayo na riba (shughuli za kukopesha) katika benki zote, yaliongezeka kutoka Sh2.12 trilioni mwaka 2021 hadi Sh2.88 trilioni mwaka 2022, huku yasiyo ya riba mapato (tozo za huduma na vyanzo vingine) yakiongezeka kutoka Sh910.63 trilioni hadi Sh1.48 trilioni.
Kodi zilizolipwa serikalini nazo zimeongezeka kutoka Sh191.99 bilioni mwaka 2018 hadi Sh522.22 bilioni mwaka 2022 na kiwango cha mikopo yenye mashaka (chechefu) kimepungua kutoka Sh532.64 bilioni hadi Sh311.71 bilioni, yote hayo yakionyesha ufanisi mzuri wa sekta hiyo katika kipindi husika ambacho wengine wanasema kigumu.
Ingawa, takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaonyesha kupunguza idadi ya taasisi za kibenki nchini kwa kipindi cha miaka mitano, zikitoka 53 hadi 45, bado sekta hiyo imefanya vizuri.
Hii ni baada ya baadhi ya benki, ama kufilisika au nyingine kuunganishwa ili kuleta ufanisi.
Katika benki hizo 45; benki 10 kubwa zinatawala soko kwa asilimia zaidi ya 77, zikiwa na asilimia 78.9 ya mali zote na asilimia 77.9 ya amana zote za wateja.
Katika ripoti hiyo ya hali ya usimamizi wa sekta ya fedha, ujumbe wa Gavana wa Benki Kuu (BoT), Emmanuel Tutuba ni kuwa mwaka 2022 mazingira ya kiuchumi hayakuwa mazuri kutokana na kuvurugika kwa mfumo wa usambazaji uliosababishwa na vita kati ya Russia na Ukraine, kuendelea kufufua shughuli za kiuchumi zilizoathiriwa na Uviko-19 pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Matukio haya ya kiulimwengu yalielemea shughuli za kiuchumi za ndani na kuongeza mfumuko wa bei. Hata hivyo hatua zilizochukuliwa kukabili hali hiyo ziliufanya uchumi kuenenda vizuri kwa kiwango kinachoridhisha cha asilimia 4.7, ambacho kilikuwa chini ya asilimia 4.9 iliyoshuhudiwa mwaka 2021.
(Katika kipindi husika) Sekta ya Benki iliendelea kupata faida, imara na stahimilivu, ikiwa na mtaji na ukwasi juu ya kiwango kilichowekwa na mamlaka ya udhibiti. Matarajio ni sekta kuendelea kuwa imara na kukua zaidi mwaka 2023,” alisema Tutuba.
Si jambo baya
Mhadhiri Mwandamizi wa Shule Kuu ya Biashara, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Thobias Swai alisema benki kupata faida si jambo baya, isipokuwa zinapopata faida kubwa sana ni changamoto.
“Hata kwenye tasnifu yangu niliandika, benki kupata faida sio shida, ila kupata faida kubwa sana ni shida kwa kuwa watu watashindwa kumudu huduma zake,” Dk Swai alisema, huku akihusisha ongezeko la faida na riba kubwa za mikopo na gharama za huduma.
Alisema gharama za mikopo katika benki nchini ni kubwa, ingawa pia hata wakopaji wazuri hawapo, hivyo benki zinalazimika kukopesha kwa gharama kubwa na kutafuta vyanzo vingine vya mapato.
“Benki zimetoka kwenye biashara zake za msingi (mikopo) na sasa zinafanya mambo mengine ili kupata faida, ndiyo maana zile ambazo hazinufaiki na miamala ya Serikali faida zake si kubwa kwa kiwango sawa na zile zinazonufaika,” alisema.
Aidha, Dk Swai alitaja sababu nyingine ya kuongezeka kwa faida za benki nchini kuwa ni kukua kwa huduma za kidijitali, akisema zimepunguza gharama za uendeshaji kwa kiwango kikubwa, huku taasisi zikitoa huduma kwa watu na maeneo mengi zaidi.
“Mikopo ya kidijitali ina gharama kubwa na watu wanaikimbilia kwa kuwa hawana elimu ya fedha, pia huduma za uwakala zimepunguza gharama za uendeshaji wa matawi, huku zikiwafikia watu wengi zaidi,” alisema Dk Swai na kuongeza kuwa usajili wa alama za kibaiolojia kupitia kitambulisho cha Taifa nao umepunguza kiwango cha mikopo chechefu.
Hata hivyo, msomi huyo wa uchumi alisema kuongezeka kwa faida za benki kunapaswa kuakisi kupungua kwa gharama za huduma zinazotolewa, kwa kuwa hayo ndiyo yanayopaswa kuwa matokeo ya ukuaji.
Kwa upande wake, Mtaalamu wa masuala ya fedha na Benki, Azizi Rashid alisema kwa sehemu kubwa faida chekwa ya mabenki imetokana na kuunganishwa kwa mifumo ya malipo, hususan ya Serikali kwa kuwa hivi sasa watu wengi wanalipia huduma mbalimbali za Serikali kupitia akaunti zao za benki kwa njia za kidijitali.
“Faida hii huenda imetokana na mambo mengi, ikiwemo kuunganishwa kwa mifumo ya malipo na huduma mbalimbali, sasa watu wengi wanaweza kulipia bili zao kupitia mifumo ya kifedha, zikiwemo benki,” alisema Rashid.
Rashid, ambaye ni mhadhiri wa masoko ya benki na fedha katika Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU), alisema huduma za benki kidijitali nazo huenda zimechangia kuongezeka kwa faida hiyo na kuna uwezekano pia kuwa kuna mikopo mingi imeiva.
Alisema licha ya kuwa kipindi kilichopita kilikuwa na kuzorota kwa uchumi, ukuaji uliendelea na kilichobadilika ni kasi, hivyo kuna uwezekano kuwa sekta ya benki yenyewe ilikuwa na ukuaji mzuri zaidi.
Hata hivyo, alisema ufanisi huo mzuri wa benki hautoi mwelekeo wa moja kwa moja wa kushuka kwa riba za mikopo wala kupungua kwa gharama za huduma za kibenki, kwani hizo zitatokana na malengo ya kiuchumi ya Serikali.
“Serikali ndiyo inatathmini inataka nini kwa wakati fulani, kwani hatua za kupunguza gharama za mikopo au huduma za kifedha kwa kiwango fulani, zinakuwa na athari za moja kwa moja katika mwenendo wa sekta ya fedha na ukwasi katika uchumi, mikopo ikishuka fedha zikawa nyingi sana baadaye zinaweza kushindwa kurudishika,” alisema.
Novemba 4, 2021 akiwa bungeni, Mbunge wa Vunjo, Dk Charles Kimei alisema sera ya fedha Tanzania bado ina upungufu mkubwa kwa kuwa haiwajali watu wenye kipato cha chini, akipendekeza kupunguzwa kwa riba na makato ya huduma.
Mchumi huyo alisema “Lazima tuangalie suala la riba za benki, kwa sasa ni kubwa mno, lazima turudi kwenye single digital (tarakimu moja) ndipo tutafaulu.”
Dk Kimei ambaye aliiongoza Benki ya CRDB kwa miaka 21, alisema uwepo wa riba kubwa imekuwa ni faida ya benki na wanahisa wake wanaotengeneza faida kubwa, lakini kwa wananchi ni maumivu.
Mbunge huyo alisema riba ikishuka itasaidia wananchi wengi kukopa kwa wingi na kufanya taasisi za fedha kuwa rafiki na wafanyabiashara.
Sera ni nzuri
Mwenyekiti wa Chama cha Mabenki Tanzania (TBA), Theobald Sabi anasema miaka iliyopita wakati na baada ya Uviko-19, BoT iliweka sera nzuri, zikiwemo za kuongeza ukwasi ambazo zilisaidia kuwa na usimamizi mzuri na ukuaji wa sekta ya fedha, ikiwemo kuongeza kiwango cha mikopo inayotolewa kwa sekta binafsi
Kuhusu ukubwa wa faida, bosi huyo wa benki ya NBC anasema imetokana na wao kujikita katika kuongeza wateja na kuwapa huduma zinazokidhi mahitaji ya soko, hivyo matarajio ni kuona ukuaji huo wa faida unazidi kuongezeka kwa kuwa kupungua kwa mikopo chechefu nako kunaongeza ufanisi.
“Kukua kwa daftari la mikopo, ambako ni matokeo ya kupanuka kwa huduma za kibenki na kufufuka kwa uchumi baada ya Uviko-19, yote hayo yaliongeza ufanisi wa sekta. Benki zote zimeongeza uwekezaji wake katika utoaji wa huduma za kidijitali ambazo zimewafikia watu wengi na kupunguza gharama za uendeshaji,” anasema Sabi.
Vilevile Sabi anasema kwa miaka ya karibuni ufanisi wa sekta ya benki nchini unahusiana na hatua za Serikali za hivi karibuni za kuvutia uwekezaji kutoka nje ya nchi (FDI) pamoja na nia ya kuendelea kuboresha mazingira ya biashara.
“Kuboreshwa kwa mazingira ya biashara na juhudi za kuvutia uwekezaji zinazofanywa na Serikali, huduma nzuri zinazotolewa na benki, mwenendo mzuri wa uchumi wa Tanzania vimeifanya sekta kuwa na faida nzuri katika sekta,” alisema Sabi.