Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bombadier Q400 kuanza kutua kiwanja cha ndege Shinyanga

Muktasari:

  • Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji Mitaji ya Umma (PIC) imezitaka Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kuwasiliana ili kuwezesha huduma kuanza kutolewa.

Shinyanga. Kukamilika kwa ujenzi wa kiwanja cha ndege Shinyanga Juni 10, 2025, kutawezesha ndege aina ya Bombadier Q400 kuanza kutua kwenye kiwanja hicho.

Akizungumza leo Alhamisi Machi 20, 2025, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Dk Charles Msonde amesema ujenzi wa kiwanja hicho umefikia asilimia 75.

"Njia za kuruka na kutua ndege, maegesho na barabara ya kuingia na kutoka kiwanjani zimekamilika, jengo la abiria ujenzi wake unaendelea na umefikia hatua nzuri," amesema.

Hata hivyo, Februari 16, 2025, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alikagua maendeleo ya ujenzi wa uwanja huo na kuelekeza jengo la zamani la abiria litumike kwa sasa wakati jengo jipya linaendelea kukamilika, ili kuruhusu huduma kuendelea.

Dk Msonde amesema mchakato ili uwanja huo uanze kutumika umeanza wakishirikiana na mamlaka nyingine.

Akizungumzia ubora wa kiwanja hicho baada ya upanuzi, Dk Msonde amesema kukamilika kwake kutawezesha ndege aina ya Bombadier Q400 kukitumia.

Dk Msonde amebainisha hayo baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji Mitaji ya Umma (PIC), kukagua maendeleo ya ujenzi wa kiwanja hicho ulichogharimu Sh48.5 bilioni.

Amesema kiwanja hicho chenye urefu wa mita 2200 na upana wa mita 30 kitakamilika Juni 10, mwaka huu.

"Kukamilika kwake kutachochea ukuaji wa shughuli za kilimo, madini na biashara mkoani Shinyanga," amesema Dk Msonde huku akibainisha kwamba ujenzi wake umetoa ajira 240 kwa wananchi.

Mbali na kukagua njia za kuruka na kutua ndege, maegesho na barabara ya kuingia na kutoka, kamati hiyo pia ilikagua jengo la abiria ambalo ujenzi wake upo katika hatua za mwisho kukamilika.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Augustine Holle ameiagiza wizara ya ujenzi kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati.

Amesema hatua ambayo umefikia ni nzuri, kama si jengo la abiria, ungekuwa umefika asilimia 90 kukamilika huku akiipongeza Wizara ya Ujenzi na Tanroads, kwa kazi nzuri na kuwahimiza kumsimamia mkandarasi akamilishe ujenzi kwa wakati na huduma za usafiri wa ndege zianze mara moja.

Aidha, Holle amezitaka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) na Tanroads kuwasiliana ili huduma za usafiri zianze kwenye kiwanja hicho.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Julius Mtatiro amesema kukamilika kwa ujenzi wa kiwanja hicho kutaondoa adha kwa watumiaji wa huduma za ndege, na kuchochea ukuaji wa uchumi mkoani humo.

"Awali tulilazimika kukitumia kiwanja cha Mwanza au cha Kahama ambacho usafiri wa ndege pale ni mara tatu kwa wiki, kukamilika kwa kiwanja cha Shinyanga kutarahisisha huduma za usafiri huo, pia kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi mkoani hapa," amesema Mtatiro ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mjini.