Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

BoT yazindua jukwaa la kulinganisha gharama za huduma za kifedha

Mchambuzi wa Fedha wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutoka Kurugenzi ya Kukuza na Kujumuisha Huduma za Kifedha, Fanuel Kijoji akifafanua kuhusu jukwaa la Kilinganisha Bei katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba

Muktasari:

  • Jukwaa hilo litaongeza uwazi, ushindani na upatikanaji wa huduma nafuu. BoT imesisitiza wakopaji kuangalia gharama zote za mikopo, huku wananchi wakisema mfumo huo utawasaidia kuepuka gharama zisizotarajiwa na kuchagua huduma bora zinazolingana na uwezo wao.

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imezindua jukwaa la kidijitali la kulinganisha bei litakalowawezesha wananchi kulinganisha ada, tozo na viwango vya riba vinavyotolewa na taasisi mbalimbali za kifedha kabla ya kuchagua huduma au bidhaa za kifedha.

Akizungumza katika Maonyesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), mchambuzi wa fedha kutoka Kurugenzi ya Kukuza Upatikanaji na Ujumuishaji wa Huduma za Kifedha ya BoT, Fanuel Kijoji, amesema jukwaa hilo linalenga kuongeza uwazi katika sekta ya fedha na kuwasaidia watumiaji kufanya maamuzi sahihi kwa kupata taarifa za bei za huduma kutoka taasisi mbalimbali kwa urahisi.

Amesema kupitia mfumo huo, mtumiaji anaweza kulinganisha gharama za bidhaa na huduma za benki moja dhidi ya nyingine au kupitia taasisi zote zinazoshiriki ili kubaini mtoa huduma anayetoa bidhaa inayokidhi mahitaji yake kwa gharama nafuu zaidi.

“Watumiaji sasa wanaweza kuchagua huduma zinazolingana na uwezo wao wa kifedha na mahitaji yao. Pia, ushindani unaoongezeka kati ya taasisi za kifedha utachangia kupatikana kwa huduma za kifedha kwa gharama nafuu zaidi,” amesema Kijoji.

Amesema jukwaa hilo kwa sasa linajumuisha bidhaa na huduma za benki, lakini BoT ina mpango wa kulipanua ili kujumuisha taasisi za fedha ndogo na watoa huduma za malipo.

Kwa mujibu wa Kijoji, hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za kuendeleza ajenda ya ujumuishaji wa kifedha nchini kwa kuwapatia wananchi taarifa zinazowawezesha kufanya uamuzi sahihi kuhusu huduma za kifedha.

Amesema gharama kubwa za huduma za kifedha, pamoja na uelewa mdogo wa wananchi kuhusu bidhaa zinazopatikana, bado ni miongoni mwa vikwazo vikuu vinavyozuia matumizi ya huduma rasmi za kifedha.

“Watu wengi wanafahamu aina chache tu za huduma za kifedha na hivyo kukosa fursa za kupata huduma bora na nafuu zaidi. Kupitia jukwaa hili, wanaweza kulinganisha huduma zilizopo kabla ya kufanya uamuzi,” amesema.

Aidha, amewataka wananchi wanaokusudia kukopa kuangalia gharama zote za mkopo badala ya kuzingatia kiwango cha riba pekee, akibainisha kuwa ada na tozo nyingine zinaweza kuongeza kwa kiasi kikubwa gharama ya mkopo.

“Ni muhimu kwa mkopaji kulinganisha gharama zote zinazohusiana na mkopo kupitia jukwaa hili ili kubaini mtoa huduma anayetoa masharti nafuu na yanayoweza kumudu,” amesema.

Wakizungumza na Mwananchi, baadhi ya wananchi wamesema jukwaa hilo litasaidia kuongeza uwazi katika sekta ya fedha na kuwaepusha na gharama zisizotarajiwa wanapotafuta mikopo au huduma nyingine za kifedha.

Mkazi wa Dar es Salaam, Anna Mushi, amesema mara nyingi wateja huchukua mikopo bila kufahamu tozo zote zinazohusika, hali inayosababisha baadhi yao kushindwa kurejesha mikopo kwa wakati.

“Kama tutakuwa na sehemu moja ya kulinganisha gharama za benki tofauti, itatusaidia kufanya uamuzi sahihi na kuchagua huduma zinazolingana na uwezo wetu,” amesema.

Kwa upande wake, mfanyabiashara mdogo, Juma Mhando, amesema mfumo huo utaongeza ushindani miongoni mwa taasisi za kifedha na kuzilazimisha kuboresha huduma zao.

“Benki zitajitahidi kutoa huduma kwa gharama nafuu zaidi kwa sababu wateja sasa watakuwa na uwezo wa kuona tofauti za bei na kuchagua huduma bora zaidi,” amesema.