Mapya mazishi ya mfanyabiashara Bosco
Muktasari:
- Bosco alikuwa mtu mwenye msimamo, aliyependa ukweli na kusaidia watu, licha ya baadhi ya watu kumfahamu kama mtu mkali
Moshi. Mfanyabiashara maarufu wa Moshi, Bosco Chuwa, amezikwa huku ikibainika kuwa aliwahi kueleza kuwa hakutamani kuugua kwa muda mrefu, bali alitamani kuondoka duniani ghafla.
Kauli hiyo imetolewa leo Julai 10, 2026 na Mchungaji Msaidizi wa Kanisa la Kilimanjaro Revival Temple (KRT), Willance Moshi, wakati akihubiri katika ibada ya kuaga mwili wa Bosco iliyofanyika nyumbani kwa marehemu, Mtaa wa Kambaita, Manispaa ya Moshi.
Mchungaji Moshi amesema Bosco alikuwa mtu mwenye msimamo, aliyependa ukweli na kusaidia watu, licha ya baadhi ya watu kumfahamu kama mtu mkali.
“Bosco alikuwa hapendi mambo ya kijinga, alikuwa mkali lakini alikuwa na upendo mkubwa. Watu wengi hawalijui hilo. Alipenda kitu cha kweli,” amesema.
Amesema alikuwa na uhusiano wa karibu na marehemu kwa miaka mingi na mara nyingi walikuwa wakizungumza kuhusu maisha na imani, huku Bosco akiwa mtu aliyependa kuuliza na kujenga hoja.
“Alikuwa anapenda neno la Mungu lakini kwa namna ya kubishana. Ukiwa umemweleza jambo anaweza kubisha, lakini kesho anarudi na kusema, ‘Mchungaji nimesoma maandiko, kile ulichoniambia ni kweli’,” amesema.
Amesema katika mazungumzo yao, Bosco aliwahi kueleza kuwa asingependa kuugua na kulazwa kitandani kwa muda mrefu kwa sababu hakutaka watu wamuone akiwa katika hali hiyo.
“Aliniambia, ‘Mchungaji sitaki niugue, sitaki nilale kitandani watu waje kunichora. Mimi nataka pap pap pap niondoke bwana’. Na kweli imetokea pap pap pap, akaondoka,” amesema.
Jeneza lenye mwili wa mfanyabiashara maarufu wa Moshi, Bosco Chuwa, likishushwa kaburini wakati wa mazishi yaliyofanyika nyumbani kwake, Mtaa wa Kambaita, Kata ya Soweto, Manispaa ya Moshi, Julai 10, 2026.
Akizungumzia siku ya kifo cha Bosco, Mchungaji Moshi amesema marehemu alitoka asubuhi kushughulikia majukumu yake mbalimbali na alikuwa akijiandaa kurejea nyumbani kusherehekea siku yake ya kuzaliwa pamoja na familia.
Amesema akiwa njiani alipata tatizo akiwa ndani ya gari, akalipaki pembeni ya barabara na kuwasha taa za tahadhari (hazard), jambo lililowafanya watu waliokuwa eneo hilo kusogea kuangalia kilichotokea.
“Mambo mengi yamesemwa mjini, lakini Bosco alitoka asubuhi akizunguka majukumu yake. Alikuwa amejiandaa jioni kusherehekea birthday yake,” amesema.
‘Hakutaka niwe mbunge’
Katika tukio hilo, Mbunge wa Moshi Mjini, Ibrahim Shayo, amesema Bosco alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa na shaka naye kuwa asingefaa kuwa mbunge, lakini si kwa sababu ya chuki bali kutokana na mtazamo wake kuhusu uongozi na ukweli.
Mchungaji Msaidizi wa Kanisa la Kilimanjaro Revival Temple (KRT), Willance Moshi, akihubiri wakati wa ibada ya kuaga mwili wa mfanyabiashara wa Moshi, Bosco Chuwa, iliyofanyika nyumbani kwa marehemu, Mtaa wa Kambaita, Kata ya Soweto, Manispaa ya Moshi, Julai 10, 2026.
Shayo amesema kabla ya kuingia kwenye nafasi hiyo, aliwahi kumtembelea Bosco nyumbani kwake na kumuuliza sababu ya kutotaka awe mbunge.
Aliniambia: “Mheshimiwa mbunge, unajua ni kwa nini mimi sitaki uwe mbunge wewe? Najua tabia yako.”
Amesema Bosco alimweleza kuwa alimwamini kwa bidii ya kazi, lakini alikuwa na hofu kwa sababu alikuwa mtu asiyejua kusema uongo.
Wasifu wa marehemu
Akisoma historia ya marehemu, mtoto wake, Junior Bosco, amesema baba yake alikuwa mtoto wa tatu kati ya watoto watano wa familia ya marehemu Benedict Chuwa na Victoria Malikia.
Amesema Bosco alianza elimu yake ya msingi katika Shule ya Msingi Korongoni kabla ya kujiunga na Kilimanjaro College ambako alipata mafunzo ya ufundi yaliyomsaidia katika utengenezaji na matumizi ya mashine mbalimbali.
Amesema alianza kujitafutia riziki akiwa na umri wa miaka 17 kwa kutumia ujuzi wa ufundi alioupata, huku akifanya kazi ya udereva wa teksi kabla ya kuingia kwenye biashara ya usafirishaji wa abiria.
Kwa bidii na kujituma, Junior amesema baba yake aliweza kuanzisha Kampuni ya Builders and Lime Works iliyojihusisha na ujenzi wa majengo, barabara na shughuli mbalimbali za uhandisi wa kiraia.
Amesema baadaye Bosco alianzisha Boby Lime Works iliyojikita katika uzalishaji wa chokaa na bidhaa zake, kampuni iliyotoa ajira kwa watu mbalimbali.
Amesema baba yake pia alikuwa mbunifu wa mashine na alitengeneza vifaa mbalimbali vya viwandani, ikiwemo mashine za kusaga mawe, kuchanganya zege na mitambo mingine ya uzalishaji.
Mapambano na ugonjwa
Junior amesema mwaka 2012 baba yake aligundulika kuwa na shinikizo la damu na baadaye Julai 5, 2021 alipata kiharusi kilichoathiri afya yake.
Amesema Bosco alipatiwa matibabu katika hospitali mbalimbali ndani na nje ya nchi, ikiwemo Nairobi Hospital na MP Shah Hospital nchini Kenya pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC).
Mbunge wa Moshi Mjini, Ibrahim Shayo, akitoa salamu za rambirambi wakati wa ibada ya mazishi ya mfanyabiashara Bosco Chuwa, iliyofanyika nyumbani kwa marehemu katika Kata ya Soweto, Manispaa ya Moshi, Julai 10, 2026.
Amesema baada ya kupambana na ugonjwa kwa muda mrefu, Julai 5, 2026 alipata tena kiharusi kilichosababisha kifo chake.
Bosco azikwa
Bosco amezikwa kando ya jengo la ibada alilolijenga na kulitumia kwa ajili ya maombi, likiwa na maandishi,Mungu ni Mkuu, yaliyowekwa juu ya paa lake.
Mazishi hayo yalihudhuriwa na familia, wafanyabiashara, viongozi wa dini na Serikali waliokusanyika kutoa heshima zao za mwisho.
Miongoni mwa waliohudhuria ni wawakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Mbunge wa Moshi Mjini Ibrahim Shayo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, madiwani, viongozi wa dini, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu.