Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Moshi ‘yasimama’ mamia ya wakazi wakimuaga Bosco Chuwa

Muktasari:

  • Mwili wa mfanyabiashara maarufu mjini Moshi, Bosco Chuwa (67), umezungushwa katika baadhi ya barabara za katikati ya mji leo Alhamisi, Julai 9, 2026, ikiwa ni sehemu ya heshima za mwisho kabla ya kupelekwa nyumbani kwake kwa ibada.

Moshi. Mwili wa mfanyabiashara maarufu wa Moshi Mjini, mkoani Kilimanjaro, Bosco Chuwa (67), leo Alhamisi Julai 9, 2026, umezungushwa katika baadhi ya barabara za katikati ya mji huo, ikiwa ni sehemu ya shughuli za kutoa heshima za mwisho kabla ya kupelekwa nyumbani kwake kwa ibada.

Msafara huo ulianza saa 9:30 alasiri baada ya mwili wa marehemu kutolewa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini ya Kilimanjaro (KCMC).

Gari la Jeshi la Polisi, lililoongozwa na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Kilimanjaro, Nassoro Sisiwaya lilikuwa mbele ya msafara huo, likifuatiwa na gari lililobeba mwili wa marehemu pamoja na magari ya ndugu, jamaa na marafiki.

Kutoka KCMC, msafara ulipitia Barabara ya Boma kuelekea katikati ya mji, maeneo ya Clock Tower, Barabara ya Njia Mbili (Double Road), Barabara ya Aga Khan na maeneo mengine kabla ya kuelekea nyumbani kwa marehemu.

Wananchi wengi wamejitokeza katika maeneo mbalimbali yaliyopitiwa na msafara huo, huku baadhi wakisimama kando ya barabara na wengine wakitoka katika maeneo yao ya kazi kutoa heshima za mwisho kwa mfanyabiashara huyo aliyekuwa akifahamika na kuheshimika mjini Moshi.

Bosco Chuwa alifariki dunia Julai 5, 2026, baada ya kuugua ghafla akiwa safarini. Kwa mujibu wa familia, alisimamisha gari pembeni ya barabara baada ya kujisikia vibaya na kuwasha taa za tahadhari.

Wasamaria wema walimjulisha mtoto wake, Junior Bosco, aliyefika eneo la tukio na kukuta baba yake akiwa katika hali mbaya.

Aliwahishwa Hospitali ya KCMC, ambako madaktari walithibitisha kuwa alikuwa ameshafariki dunia.

Akizungumza na Mwananchi leo, msemaji wa familia, Allen Chuwa amesema uamuzi wa kuuzungusha mwili wa marehemu katikati ya mji umelenga kuwapa wananchi fursa ya kumuaga na kumuenzi kwa mara ya mwisho.

Amesema Jeshi la Polisi limeshirikiana na familia kuratibu msafara huo ili kuhakikisha shughuli hiyo inafanyika kwa utulivu na usalama.

Baada ya kukamilika kwa msafara, mwili umepelekwa nyumbani kwa marehemu katika Mtaa wa Khambaita, Kata ya Soweto, Manispaa ya Moshi ulilopokelewa na ndugu, jamaa, marafiki na waombolezaji kabla ya kufanyika kwa ibada fupi ya kifamilia.

Allen amesema jioni ya leo kutafanyika kumbukizi maalumu iliyopewa jina la 'Bosco Night', itakayowakutanisha ndugu, jamaa, marafiki na wananchi kwa ajili ya ibada na kuendelea kutoa heshima za mwisho kwa marehemu.

Ameongeza kuwa mazishi ya Chuwa yatafanyika kesho, Julai 10, 2026, kuanzia saa 3:00 asubuhi itafanyika ibada ya kuuaga mwili kabla ya maziko yatakayofanyika nyumbani kwake, Mtaa wa Khambaita mjini humo.